Morogoro. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amesema tayari Serikali imenunua pikipiki 700 ambazo zitagaiwa kwa maofisa mifugo kwenye halmashauri zote nchini, ili maofisa hao wawafikie kirahisi wafugaji na kuwapa elimu ya ufugaji bora na wa kisasa, lengo likiwa ni kuboresha sekta ya mifugo nchini.
Dk Kijaji ameyasema hayo leo Juni 1, 2025 wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya maziwa ambayo kitaifa imefanyika mkoani Morogoro, ambapo pia amewataka maofisa mifugo kuhakikisha wafugaji wanazalisha maziwa salama na bora yatakayoweza kusindikwa na kuongezeka thamani kwa kutengenezewa bidhaa mbalimbali.
Waziri wa mifugo na uvuvi Dk Ashatu Kijaji akisalimiana na wamama wa kifugaji kutoka jamii ya kimaasai wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya maziwa ambayo kitaifa imefanyika mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff.
Aidha Dk Kijaji amesema kila mwaka Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya maofisa mifugo ambapo kwa mwaka jana iliwapatia pikipiki 1,400.
“Mwaka huu mbali na kutoa pikipiki 700 lakini pia imewekeza wafugaji kupata mbegu bora za malisho.”
“Juni 16 mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan atazindua shughuli ya chanjo na utambuzi wa mifugo litakalofanyika Bariadi mkoani Simiyu, na katika hatua hii ya utambuzi Serikali imeandaa heleni za kidijitali 36,323,300 kwa ajili ya utambuzi wa mifugo, tunataka tuutambue kila mfugo hapa nchini,” amesema Dk Kijaji.
Akizungumzia uzalishaji wa maziwa Dk Kijaji amesema, umeongezeka kutoka lita 3.7 milioni kwa mwaka 2023 /2024 hadi kufikia lita 4.02 milioni kwa mwaka 2024/2025 na Mkoa wa Morogoro unaongoza latika Mapinduzi ya sekta ya mifugo na maziwa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adamu Malima amesema mkoa huo una zaidi ya ng’ombe milioni mbili, hata hivyo wengi ni wa kienyeji wasiokuwa na uwezo wa kutoa maziwa zaidi ya lita mbili kwa siku.
Awali akitoa taarifa ya maadhimisho hayo msajili wa bodi ya maziwa nchini, Profesa George Msalya amesema tasnia ya maziwa ni jumuishi kwa kuwa maziwa ni lishe, uchumi, chakula, ajira na kiburudisho.
Profesa Msalya amesema kwa kuona umuhimu wa maziwa bodi ya maziwa imepanga kuanzisha migahawa ya maziwa kwenye mikoa mbalimbali ili kupanua soko la maziwa kwa kuwa ni asilimia tatu tu yanayozalishwa nchini, ndio yanapelekwa viwandani kwa ajili ya kusindikwa.

“Mbali ya kuanzisha hiyo migahawa ya maziwa kama ilivyokuwa kwa baa za vinywaji vingine, lakini pia tumepanga kuanzisha ATM za maziwa kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini,” amesema Profesa Msalya.
Kwa upande wao baadhi ya wafugaji wamesema kufanyika kwa maadhimisho hayo mkoani Morogoro kumewanufaisha kwa kuwa wameweza kupata elimu ya ufugaji bora na wa kisasa, lakini pia wameweza kukutana na wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, (TADB) ambayo imekuwa ikitoa mikopo kwa wasindikaji wa maziwa.