Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limewataka vijana waliochaguliwa kujiunga nalo kuripoti katika Shule ya Polisi Moshi kuanzia Juni 12 hadi 14, 2025 kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo.
Vijana hao, ni wale waliofanya maombi na kufaulu katika usaili uliofanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Taarifa ya wito huo, imetolewa jana Jumapili Juni 1, 2025 na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camilius Wambura.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliofanyiwa usaili Dar es Salaam kwenye vikosi vilivyo chini ya makao makuu ya jeshi hilo wataripoti jijini humo, katika uwanja wa gwaride uliopo Kambi ya Polisi barabara ya Kilwa.
Vijana hao, taarifa hiyo inaeleza wanatakiwa kuripoti Juni 12, 2025 saa 12.00 asubuhi kwa ajili ya safari ya kwenda Shule ya Polisi Moshi.
Kwa upande wa waliofanyiwa usaili katika mikoa ya Tanzania Bara wanatakiwa kuripoti kwa makamanda wa polisi wa mikoa waliofanyia usaili, Juni 11, 2025 saa 2.00 asubuhi kwa ajili ya kupewa utaratibu wa safari ya kwenda Moshi.
“Vijana waliofanyia usaili Zanzibar kwa maana Unguja na Pemba, wanatakiwa waripoti makao makuu ya Polisi Zanzibar Juni 11, 2025 saa 2.00 asubuhi kwa ajili ya kupangiwa utaratibu wa safari,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, imeeleza kuwa vijana wote waliochaguliwa wanatakiwa kuripoti Shule ya Polisi Moshi wakiwa na traki suti rangi ya bluu yenye ufito mweupe, fulana nyeupe isiyo na maandishi, raba, soksi nyeusi na bukta mbili za bluu kwa ajili ya michezo na mazoezi pamoja na sanduku la chuma la rangi ya bluu.
Vingine wanavyopaswa kwenda navyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo ni chandarua cheupe cha duara na sio cha pembe nne, shuka za rangi ya bluu mpauko jozi mbili, pasi ya mkaa na blanket moja la kijivu lisilo na maua na sio duveti.
Pia, wanatakiwa kwenda na kikombe cha plastiki kilichotengenezwa kwa matirio ya mfupa, sahani moja, vifaa vya usafi, sururu moja lenye mpini, ndoo mbili ndogo na fagio la chelewa.
Taarifa hiyo inataka waende na kadi ya bima ya afya (NHIF) kama anayo au fedha taslimu Sh50,400 kwa wasio na kadi za bima ya afya.
Pia, wanatakiwa kwenda na vyeti halisi vya taaluma, cheti halisi cha kuzaliwa, kadi ya Nida au namba ya utambulisho wa Taifa (Nida), nakala za kadi za Nida au namba za utambulisho wa Taifa za wazazi na watu wa karibu upande wa baba na mama.
Wanatakiwa kwenda na fedha za kujikimu, simu za mkononi haziruhusiwi chuoni, hivyo ni marufuku.
“Yeyote atakayepatikana na simu itachukuliwa kuwa ni utovu wa nidhamu na adhabu yake ni kufukuzwa mafunzo mara moja. Shule itaelekeza utaratibu wa kupata mawasiliano,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Imeeleza kwa yeyote atakayeripoti shule baada ya Juni 14, 2025 hatopokelewa na atahesabika amejiondoa mwenyewe kwenye mafunzo.