Wawakilishi walia sheria ya uvuvi kuwanyanyasa wavuvi

Unguja. Wakati Wizara ya Uchumi wa Buluu ikisema ipo kwenye mchakato wa mwisho kufanyia marekebisho ya sheria ya uvuvi, wajumbe wa baraza la wawakilishi wametoa mapendekezo yao kuondoa vipengele ambavyo vimekuwa mwiba kwa wavuvi.

Malalamiko hayo ya  sheria hiyo namba saba ya mwaka 2010 ni pamoja na kuzuia wavuvi kuingia na viatu baharini, kutumia vioo na chupa za gesi wanapokwenda kuvua.

Wakichangia bajeti ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi leo Juni 2, 2025 wawakilishi wamesema ni vyema sheria hiyo imepitwa  na wakati kwani kwa sehemu kubwa haimnufaishi mvuvi mdogo ambaye ndio mlengwa mkuu.

Mwakilishi wa Jimbo la Kojani,  Hassan Omar Hamad amesema sheria hiyo haimpi nafasi mvuvi kufanya shughuli zake kwa uhuru, licha ya kwamba sekta hiyo ndio inaajiri watu wengi katika visiwa hivyo.

“Leo hii tukisema eti kuingia na kioo baharini kuvua ni haramu kwa kweli hatutendei haki mvuvi na wamekuwa wakiogopa kwa sababu ya kukumbana na changamoto hizi,” amesema.

Pia amesema kuingia na vifaa hivyo na chupa ya gesi kwa wavuvi wanajua kuwa vifaa hivyo ni kwa ajili ya kumlinda na hatari za baharini, na vifaa hivi sio haramu.

Ameishauri Serikali kujikita kwenye tafiti zaidi kubaini umuhimu wa vifaa hivyo na athari zake kwa wavuvi, badala ya kuweka sheria ambazo zinalenga kuwaumiza wavuvi.

Mwakilishi mwingine wa Mtoni, Ibrahim Makungu amesema mambo mengi yamebadilika tangu sheria hiyo itungwe kwa hiyo ipo haja ya kuleta sheria mpya ambayo itaendana na mazingira na teknolojia iliyopo kwa sasa.

Amesema wavuvi wengi wanalalamika wanapozuiliwa kufanya hivyo na kusababisha uvuvi wao kuwa wa mashaka.

Pia amezungumzia kuhusu leseni ambazo zinawabana hata kwenda katika maji mengine ya Tanzania bara.

Hoja hiyo imegusiwa pia na Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said ambaye pia amesema kuna changamoto ya kuvua samaki

Amesema ni aibu Zanzibar kuendelea kuagiza samaki nje ya nchi ilhali kuna rasilimali kubwa ya bahari, lakini bado haijawekewa mazingira wezeshi katika kuvua samaki wengi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Uchumi wa Buluu, Shaban Ali Othman, kiwango cha uzalishaji wa samaki kimeongezeka kwa asilimia 107.2 kutoka tani 38,107 zenye thamani ya Sh205.35 bilioni mwaka 2020 hadi kufikia tani 78,943 zenye thamani ya Sh618.18 bilioni mwaka 2024.

Hivyo, mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 4.1 mwaka 2023 hadi kufikia asilimia 5.7 mwaka 2024 kwa mujibu Ofisi ya mtakwimu Mkuu wa Serikali.

Pia sekta ya uvuvi imekua kwa asilimia 14.2 kwa mwaka 2024 kutoka asilimia 8.1 mwaka 2023.

Ongezeko hili linatokana na hatua mbalimbali za Serikali katika kuimarisha sekta ya uvuvi kwa kuwawezesha wavuvi, wakulima wa mwani.

Waziri wa Wizara hiyo, Shaaban Ali Othman amesema sheria hiyo ipo kwenye hatua za mwisho kufanyiwa marekebisho

Awali akiwasilisha bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo,  Shaaban  ameliomba baraza hilo kuidhinisha Sh172 bilioni, kati ya fedha hizo Sh157 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Baraza limeijadili na kupitisha bajeti hiyo kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele 12 na miradi 10 ya maendeleo.

Related Posts