Maonyesho ya Kilifair kuanza | Mwananchi

Arusha. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maonyesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu Kili fair, yatakayofanyika jijini Arusha.

Maonyesho hayo yatafanyika kuanzia Juni 6 hadi 8, 2025,katika viwanja vya Magereza (Kisongo) mkoani Arusha.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 2,2025 na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda alipotembelea na kukagua maandalizi ya maonyesho hayo ambapo amesema  kuwa Dk Biteko atayazindua Juni 6, 2025 viwanjani hapo.

Makonda amewataka wadau wa utalii mkoani humo kutumia maonesho hayo kujifunza mbinu za uwekezaji kutoka kwa watoa huduma na wanunuzi wa utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vilivyomo nchini.

“Maonyesho ya mwaka huu ni tofauti na tumepanda viwango, ukiangalia kampuni zaidi ya 500 kutoka nchi zaidi ya 40 zitashiriki kuonyesha masuala mbalimbali ya mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya utalii, na tunatarajia Dk Biteko awe mgeni rasmi,” amesema Makonda.

“Hii ni fursa kubwa kwetu kiuchumi niwaombe wananchi na wadau wa sekta ya utalii kuchangamkia fursa hii. Kuanzia kwa bodaboda, bajaji, teksi, hoteli na watoa huduma wengine, tuhudumie wageni kwa ukarimu mkubwa ili tukuze uchumi wetu,” amesema

Awali Mkurugenzi wa kampuni ya Kilifair Promotion, Dominic Shoo, ambao ndiyo waandaaji wa maonyesho hayo, amesema hadi sasa maandalizi yamefikia asilimia zaidi ya 70.

Amesema lengo lake ni kukuza biashara ya utalii kimataifa kwa kutangaza vivutio vilivyopo nchini na fursa mbalimbali ambapo wadau na wanunuzi wa utalii watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

Amesema mbali na hivyo kupitia maonyesho hayo pia yamelenga kuinua mazao mapya ya utalii na kuuleta ulimwengu kwa pamoja kibiashara na kuwa mwaka huu maonesho ni makubwa kuliko mwaka jana kwani mwamko umezidi kukua.

“Mwaka huu tumeongeza eneo la maonyesho ambapo tutatumia eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 41,000 ukilinganisha na mwaka jana tulitumia eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 15, 000.Miaka yote hatujawahi kuwa katika hatua hii ya maandalizi, mwaka huu maonyesho yatakuwa makubwa sana ,”amesema

Shoo amesema katika maonyesho hayo wageni zaidi ya 15,000 wanatarajiwa kushiriki na kuwa yanatarajiwa kuongeza chachu ya mageuzi katika sekta ya utalii barani Afrika kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wawekezaji, wanunuzi na watoa huduma kutoka pande mbalimbali za dunia.

Related Posts