Arusha. Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mercy Silla amezitaka asasi za kiraia nchini kuwa na mikakati ya kusogeza mbele ajenda za maendeleo ya nchi, ili kuhakikisha lengo la utoaji huduma shirikishi linatimizwa kwa wananchi wote.
Silla ameyasema hayo leo Juni 2, 2025 jijini Arusha wakati wa ufunguzi rasmi wa wiki ya asasi za kiraia iliyoanza ikiwa na malengo ya kujadili nafasi za asasi hizo katika maendeleo ya nchi lakini pia namna ya kufikia mafanikio ya dira ya maendeleo ya mwaka 2050 inayotarajiwa kuzinduliwa mwakani.
Silla amesema nchi bado ina changamoto nyingi ambazo asasi za kiraia hazipaswi kubaki nyuma katika utatuzi wake, bali zinatakiwa kujitafakari nafasi zao katika utatuzi wa changamoto hizo ikiwemo jinsi ya kufanikisha malengo ya dira ya maendeleo yanayowekwa.
“Kwa sasa tumemaliza kutoa maoni katika dira yetu lakini bado kuna maboresho yanafanywa kabla ya kuzinduliwa rasmi mwakani, niombe tusikae nyuma kutafuta upungufu pekee bali ni wakati wetu kutafakari na kutoa maoni na mikakati ya kufikia lengo,” amesema Silla ambaye pia ni mwenyekiti wa asasi za kiraia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa maandalizi ya Wiki ya CSO, Nesia Mahenge amesema wiki ya asasi za kiraia 2025 yenye kaulimbiu “Njia za Maendeleo,” inasisitiza dhamira ya asasi za kiraia katika kuendeleza maendeleo jumuishi na endelevu.
Kwa upande wake, Neema Bwaira, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, ameeleza kuwa asasi za kiraia zina nafasi ya kipekee katika kuendeleza maendeleo na kuhamasisha utekelezaji wa sera pamoja na dira ya taifa.
“Tutumie fursa hii kwa mazungumzo ya kina, kubadilishana suluhisho bunifu na kuanzisha ushirikiano wa kuvuka mipaka.
“Mitazamo yetu tofauti, lakini yenye kusudi la pamoja, hutuwezesha kukabiliana na changamoto tata za zama hizi kutoka mabadiliko ya tabianchi na ubunifu wa kiteknolojia, hadi haki za binadamu na maendeleo endelevu,” amesema.
Bwaira amesisitiza haja ya wadau wote kushiriki kikamilifu katika kuunda mustakabali wa Tanzania, kwa kuunganisha juhudi kuelekea malengo ya pamoja yaliyoainishwa katika Dira ya 2050.
Katika mjadala huo, Doreen Dominic, Mkuu wa Sekta ya Umma kutoka Benki ya Stanbic, ametoa wito kwa asasi za kiraia kuhakikisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi yanapewa kipaumbele katika mijadala ya maendeleo ya kiuchumi.
“Hatuwezi kuzungumzia ukuaji wa uchumi bila kugusia mabadiliko ya tabianchi, wala hatuwezi kuzungumzia biashara bila kuzingatia athari za kimazingira. Tunahitaji uchumi wenye akili na unaowajibika kimazingira,” amehitimisha.