Dar es Salaam. Mageuzi yaliyofanyika ndani ya mashirika ya umma ikiwamo kuunganisha na kufuta mengine, imetajwa kuwa na matokeo chanya kiasi cha kuongeza gawio litakalotolewa kwa Serikali.
Hadi sasa Ofisi ya Msajili wa Hazina imeshakusanya zaidi ya Sh900 bilioni huku ikitarajiwa kufikisha Sh1 trilioni kabla ya Juni 10 mwaka huu ambalo ndilo gawio litakalowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Juni 2, 2025 na Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari jijini hapa wakati akielezea safari ya mageuzi, mafaniko, mikakati na muelekeo wa ofisi yake.
Mchechu amesema tangu Februari 2023 hadi sasa, mageuzi 11 yamefanyika katika maeneo mbalimbali huku yakibeba matokeo chanya ndani ya mashirika ya umma ikiwamo yalitokuwa yakipata hasara zamani kutangaza faida.
Maeneo yaliyoguswa katika mageuzi hayo ni muundo wa ofisi ya msajili wa hazina, uhuru wa kujiendesha taasisi za kibiashada na kimkakati, kuunganishwa na kufutwa kwa taasisi, kuboresha mizania za taasisi na shughuli za Ofisi ya Msajili wa Hazina kujulikana zaidi.

Maeneo mengine ni uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji taasisi za umma, kuhuisha vigezo vya upimaji, ufanisi katika kutathmini bodi za wakurugenzi, ushirikiano wa kimkakati na taasisi ya uongozi, wawekezaji wapya watano katika viwanda vilivyobinafsishwa na tija ya uwekezaji wa Serikali.
Alitolea mfano wa eneo la uboreshaji wa mizania alisema mpaka sasa taasisi tatu zimenufaika huku tano zikiwa bado zina uhitaji.
“Kwa sasa Benki ya Biashara Tanzania (TCB) iliongezewa mtaji wa Sh131 bilioni na hii imeifanya kutengeneza faida ya Sh31.6 bilioni mwaka 2024. Kwa upande wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambao nao walikuwa wakirekodi hasara mfululizo tulibadili deni la Sh2.4 trilioni kuwa mtaji; na hii imewafanya kutengeneza faida kutoka Sh8.9 bilioni hadi kufikia Sh21.8 bilioni mwaka 2024,” amesema.
Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) nao walibadilishiwa deni la Sh2.7 trilioni kuwa mtaji na sasa wameshuhudia ongezeko la faida kutoka Sh159.6 bilioni hadi kufikia Sh306 bilioni mwaka 2023/24.
Akizungumzia mageuzi yaliyofanyika katika upande wa kuzifanya taasisi kujitegemea, Mchechu amesema kwa sasa zipo 57 ambazo zimepewa uangalizi wa karibu ili kuona matokeo yake kwanza kabla ya kuzipa uhuru.
Amesema wakati wanafikiria hilo, walikuwa wakiangalia namna ya kuzifanya kuwa na uongozi imara, kuwapa uhuru wa kuajiri, kuchukua hatua na kuwawezesha mitaji pale wanapohitaji na kuimarisha namna ya kuwapima katika malengo waliyokubaliana.
Katika uunganishaji wa taasisi 14 ambazo alitangaza awali, Mchechu amesema wako katika hatua za mwisho kwani mambo kadhaa huangaliwa ikiwamo mali wanazomiliki huku lengo likiwa ni kufanya mageuzi na pale jitihada hizo zitakaposhindikana ndiyo wataamua kuwa taasisi hiyo inahitajika au la.
Hali hiyo imefanya mwenendo wa utoaji michango kutoka kwenye taasisi na mashirika ya umma kubadilika kila mwaka kwani idadi ya taasisi na mashirika ya umma ambayo yamekuwa yakichangia katika gawio la Serikali imekuwa ikibadilika kila mwaka kwa kupanda na kushuka.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu kati ya mwaka 2021/22 hadi mwaka 2023/24 wastani wa taasisi na mashirika ya umma 146 ndiyo yamekuwa yakitoa michango sawa na
asilimia 59 ya taasisi zote.
“Hii imefanya mwenendo wa utoaji gawio, kwa wastani, umekuwa ukiongezeka kwa asilimia 50 kila mwaka. Pamoja na ongezeko hilo idadi ya kampuni ambazo zimekuwa zikilipa gawio ni chache ikilinganishwa na jumla ya kampuni ambazo Serikali ina hisa chache,” amesema Mchechu.
Licha ya hilo alizungumzia makadirio ya gawio la Sh1 trilioni linalotarajiwa kutolewa siku chache zijazo akisema itakuwa ni ongezeko la asilimia 30.4 ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita Sh767 bilioni zilikusanywa.
Ili kuhakikisha ofisi hiyo inafikia lengo la kukusanya Sh1 trilioni kutoka a Sh900 bilioni zilizokuwapo, Mchechu alizitaka taasisi ambazo bado hazijawasilisha gawio zifanye hivyo ndani ya wiki hii.
“Taasisi zote ambazo bado hazijawasilisha gawio kwa Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, zinapaswa kufanya hivyo ndani ya wiki hii ili ifikapo siku ya gawio, Juni 10 mwaka huu, asiwepo wa kudaiwa,” amesema.
Mchechu amesema ukuaji wa mapato yasiyo ya kodi umetokana na kuimarishwa kwa utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu wa gawio na michango katika mashirika ya umma na matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema ni vyema taasisi hizo zikaongeza bajeti zake za kujitangaza ili kufanya wananchi kujua kwa kina kile ambacho Serikali inafanya.