Madeni ya Serikali kwa MSD yawaibua wabunge

Dodoma. Wabunge wameitaka Serikali kulipa deni la Bohari ya Dawa (MSD) linalofikia Sh739.2 bilioni ili kuulinda mnyororo wa ugavi na kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa utoshelevu.

Wabunge wameyasema hayo leo Jumatatu Juni 2, 2025 wakati Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Elibarick Kingu akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/26. 

Wizara hiyo imeomba kupatiwa Sh1.61 trilioni, kati ya fedha zinazoombwa Sh991.75 bilioni zimeelekezwa katika miradi ya maendeleo ambayo ni sawa na asilimia 61 ya bajeti inayoombwa.

Akisoma maoni ya kamati hiyo, Kingu amesema Serikali ilipe deni inalodaiwa na MSD la Sh434.2 bilioni.

Akitoa mchanganuo wa deni hilo, Kingu amesema Sh46.4 bilioni kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma vilivyopo chini ya Wizara ya Afya.

Pia amesema kati ya deni hilo la Sh83.1 bilioni ni kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma vilivyopo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Amesema pia Serikali inapaswa kulipa Sh305 bilioni za miradi misonge.

Aidha, Kingu ameishauri Serikali kutoa Sh300 bilioni kwa MSD ili kuongeza ufanisi na kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya na kusaidia uwekezaji kwenye viwanda.

“Kukosekana kwa mtaji huo kunasababisha Bohari ya Dawa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa ufanisi,” amesema Kingu.

Kamati hiyo, imeitaka Serikali kulipa mkopo wa Sh210.29 bilioni wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ili kuimarisha utendaji wa mfuko huo na kutokwamisha uendeshaji wa mfuko huo.

Kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Kingu amesema Serikali iwashirikishe wadau kutoka sekta binafsi katika kuchangia fedha za mfuko wa kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo.

Amesema hilo ni kwa lengo la kuongeza fedha za kusaidia matibabu kwa watu wasio na uwezo, wakati wa utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote nchini.

Aidha, Kingu ameshauri Serikali kukamilisha Sheria ya Kusimamia Huduma ya Uvunaji, Utunzaji na Upandikizaji wa Chembechembe na viungo vya Mwili wa Binadamu ili kuweka namna nzuri ya utoaji wa huduma hii kwa wananchi.

Kwa upande wa magonjwa yasiyoambukiza, Kingu ametaka ifanye tafiti kubaini ukubwa wa tatizo la magonjwa hayo nchini na kutoa elimu kwa jamii kuhusu vyanzo vyake  na namna ya kuyaepuka hususan kwa kuzingatia mazoezi na lishe.

“Ishirikishe sekta zingine katika utekelezaji wa afua za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza,” amesema.

Kuhusu usajili wa vituo vya afya, Kingu ameshauri Serikali iunde bodi moja ya kuvisajili kote nchini.

“Hatua hii itaweka ulazima wa vituo vya kutolea huduma za afya vinavyomilikiwa na Serikali kusajiliwa kwa kukidhi vigezo kabla ya kuanza kutoa huduma,” amesema.

Aidha, kamati hiyo imeshauri uimarishaji wa viwanda vya ndani vya kuzalisha bidhaa za dawa ili uweze kuleta tija kwa Watanzania.

Kingu ametaja mambo ambayo Serikali inatakiwa kufanya ni kuongeza kodi kwa bidhaa za dawa zinazotoka nje ya nchi, ambazo zinazalishwa na viwanda vya ndani na kufufua kiwanda cha dawa cha Arusha ambacho kina umiliki wa hisa za asilimia 40.

Pia ameshauri Serikali kuongeza kiwango cha uzalishaji wa dawa katika kiwanda cha dawa Keko kilichopo jijini Dar es Salaam, ambacho kina umiliki wa hisa za asilimia 70.

“Itoe msamaha wa kodi kwa malighafi zinazoingizwa nchini kwa ajili ya kuzalisha bidhaa za dawa,” amesema.

Akichangia makadirio hayo, Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospiter Muhongo ameshauri kuangalia mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) yanavyotaka na kutoa mfano upande wa madaktari kuwepo na uwiano wa daktari mmoja kwa watu 1,000.

Amesema itakapofika mwaka 2050 kama Watanzania watazaliana sana, Tanzania inatarajiwa kuwa na watu milioni 140 ambapo nchi itahitaji kuwa na madaktari 140,000 kwa mujibu wa mapendekezo hayo.

“Kingine cha kujipima nacho ni idadi ya wauguzi, napendekeza nesi mmoja kwa wagonjwa wanane. Tunafanya vizuri lakini tunapaswa kujipima. Na kwenye maeneo ya dharura na ya afya ya akili kama Mirembe inataka muuguzi mmoja kwa wagonjwa wanne,” amesema.

Profesa Muhongo amesema Watanzania wana safari ndefu na wameanza kutembea wasikate tamaa.

Profesa Muhongo amesema Serikali imefanya vizuri katika eneo la vifaatiba.

Mbunge wa Momba (CCM) Condester Sichalwe amesema kuwa wanatambua juhudi zinazofanywa na Serikali katika utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote lakini utaratibu huo hauwezi kusubiri.

“Wananchi wa Tanzania mmeamua kuwasubirisha ili mambo yakamilike lakini inawezekana mtu ameumwa leo na Mungu inawezekana amempa siku saba za kuishi, katika ugonjwa huo na sasa kama jambo hili litakamilika miezi mitatu ijayo ama mwaka ujao, mtu huyu anaendeleaje kupata huduma,” amesema.

Ameshauri wakati maboresho hayo yanaendelea kuruhusu vifurushi walivyoondoa katika mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) virejeshwe kwa sababu sio Watanzania wote wenye uwezo wa kumudu gharama za matibabu.

“Hata mtu anayekwenda kupima umeme kwenye moyo ana kadi ya bima, inabidi iongezwe, mtu amejinyima akalipia bima ili iweze kumsaidia kwa hiyo tunaomba vifurushi hivyo virejeshwe,” amesema.

Aidha, Sichwale amesema kuwa jitihada zimefanyika za kuongeza miundombinu na vifaatiba na kuomba wataalamu waajiriwe kwa wingi ili vituo vya kutolea huduma viweze kufanya kazi saa 24.

Pia Mbunge huyo ameomba kuwa matibabu kwenye kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo, yapewe msamaha ama kupunguzwa kwa gharama kwa sababu ni ghali.

Related Posts