CCM Iringa walivyompokea Asas | Mwananchi

Iringa. Mfanyabiashara na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Salim Faraj Abri (Asas) apokewa rasmi na uongozi wa chama Mkoa wa Iringa kufuatia kuteuliwa kwake kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Asasi amepokewa leo Juni 2, 2025 akitokea Dodoma alikokwenda kuhudhuria mkutano mkuu baada ya kuteuliwa kuwa mjumbe wa kamati kuu ya CCM sambamba na makada wengine wa chama hicho.

‎Akizungumza katika hafla hiyo, mbele ya viongozi na wanachama wa CCM katika viwanja vya Ofisi ya CCM Mkoa, Asas amesema uteuzi huo ni heshima kubwa kwake na unadhihirisha imani ya chama juu ya uongozi wake.

‎Asas amekiri kuwa nafasi hiyo inahitaji umakini wa hali ya juu, akisisitiza kuwa CCM ni dira ya nchi na si chama cha kufanya dansi au sarakasi.

Mjumbe wa kamati kuu ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Salim Faraj Abri (Asas) akizungumza na wananchi katika viwanja vya ofisi ya CCM mkoa katika hafla ya kupokelewa na kupongezwa  baada ya kuteuliwa katika nafasi hiyo ya kitaifa CCM.

‎“Nafasi hii si ya mzaha, CCM ni chama makini, si cha kusema kitaendeleza dansi au sarakasi. Baada ya uteuzi huu, nasoma kipengele kwa kipengele, naamini kwa ushirikiano wenu nitaweza kwa busara na amani,” amesema Asas.

‎Ameongeza kuwa yuko tayari kuitumikia CCM kwa moyo wote, mchana na usiku, mvua au jua, akisisitiza kuwa atatekeleza majukumu yake kikamilifu.

Mkuu wa Mkoa  wa Iringa, Peter Serukamba akizungumza na Wananchi katika viwanja vya ofisi ya CCM mkoa katika hafla ya kumpokea na kumpongeza Salim Faraj Abri Asas baada ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa kamati kuu ya Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM Taifa.

‎Asas ana historia ndefu ndani ya CCM, amekuwa mdau wa maendeleo mkoani Iringa kupitia uwekezaji wake katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, usafirishaji na viwanda ambapo pia uteuzi wake unatarajiwa kuimarisha mchango wake katika maendeleo ya chama na Taifa.

‎Ikumbukwe kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), katika kikao chake maalumu kilichofanyika Mei 28, 2025 jijini Dodoma, iliwateua wajumbe wanne wa kamati kuu waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati Kuu akiwamo Namelock Sokoine, Dk Juma Abdallah (Mabodi)‎ na Hamad Hassan Chande.

‎ Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin amesema Rais Samia Suluhu Hassan anapaswa kupongezwa kwa kumteua Asas kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa.

‎ “Hakika Iringa tumeonwa kwani kupitia kiongozi huyu tunaona juhudi zake za kutosha katika maendeleo ya wananchi na hata CCM,” amesema Yassin.

‎Hata hivyo, Yassin ameeleza kuwa kuna utekelezaji wa ilani ya barabara ya mchepuko kutokea Kihesa Kilolo – Igumbiro na barabara ya kutoka Kalenga kwenda Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na miradi mingine ya afya na elimu mkoani humo.

‎ Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba amepongeza hatua hizo huku akisisitiza kuwa katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, wananchi wanapaswa kuwa makini na kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo chanya katika sekta mbalimbali.

‎ “Niwakumbushe na niwaombe wananchi katika kipindi cha uchaguzi mkuu, mzingatie kuchagua viongozi waadilifu, ndio watawafikisha kwenye maendeleo,” amesema Serukamba.

‎Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu amesema uteuzi huo wa Asas ni dhahiri amepewa kibali cha kutenda wema nchini kupitia chama hicho na hivyo ndivyo itakavyokuwa.

Mbunge wa Iringa mjini, Jesca Msambatavangu akizungumza na Wananchi katika viwanja vya ofisi ya CCM mkoa katika hafla ya kumpokea na kumpongeza Salim Faraj Abri Asas baada ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa kamati kuu ya Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM Taifa. 

“Na niseme tu kwamba, mtu ukipewa nafasi ya kutenda wema utatenda wema na utaonekana kwa watu, tuseme Rais Samia asante kwa nafasi hii,” amesema Msambatavangu.

Related Posts