Wanafunzi Serengeti walilia mabweni | Mwananchi

Serengeti. Baadhi ya wanafunzi wa kike katika shule za sekondari wilayani Serengeti wameiomba Serikali na jamii kuwaondolea vikwazo vinavyosababisha washindwe kutimiza malengo yao hasa ya kielimu, ikiwemo ukosefu wa mabweni katika shule za Serikali.

Wanafunzi hao wamesema licha ya Serikali kujitahidi kuboresha mazingira ya elimu bado wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwepo kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule, wakidai kuwa hali hiyo ni kikwazo kutimiza ndoto zao za kupata elimu.

Wakizungumza mjini Mugumu leo Juni 2, 2025 kwenye kongamano lililoandaliwa Shirika la Grumeti Fund kwa ajili ya kutoa elimu ya makuzi na hedhi salama kwao.

Wanafunzi hao wamesema changamoto zingine ni pamoja na vishawishi kutoka kwa watu mbalimbali hususan  bodaboda na hivyo kujikuta wakijiingiza kwenye masuala ya mapenzi.

“Kuna changamoto kubwa sana kwa hawa bodaboda, wamekuwa wakitumia suala la wanafunzi wa kike kutembea kwenda na kurudi shuleni kufanikisha malengo yao, wanatumia usafiri wao kuwarubuni na wao bila kujijua wanajikuta wakinasa kwenye mtego huo,” amesema Irene Kaitira.

Nora Marwa amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa taulo za kike kwa ajili ya kujisitiri nyakati za hedhi hali ambayo inasababisha kushindwa kushiriki kikamilifu katika masomo kwa kuhofia kudhalilika.

“Kuna wengine wanashindwa kabisa kuja shuleni wakiogopa fedheha watakazokutana nazo endapo watachafua nguo kwa sababu hawana pedi na kwa wale wanaojitahidi kufika, wanakuwa hawana amani kabisa darasani hivyo kushindwa kuwa makini kumsikiliza mwalimu,” amesema.

Akizungumza na wanafunzi hao kutoka shule mbalimbali, Mratibu wa Vijana kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria,  Mchungaji Emmanuel Sitta amesema wazazi na jamii wanapaswa kutoa kipaumbele katika malezi ya watoto wa kike ili kuwa na kizazi bora cha baadaye.

Amesema watoto wa kike wanakabiliwa na changamoto nyingi katika makuzi yao na endapo hazitapatiwa ufumbuzi mapema kuna hatari ya kushindwa kutimiza ndoto zao.

“Wazazi na jamii kwa ujumla tunatakiwa kutimiza wajibu wa malezi kwa watoto wetu, sasa hivi kila mzazi amejikita kwenye suala zima la utafutaji tunasahau kuwa sisi ni walezi hali ambayo inasababisha watoto wetu kuangamia, hebu turejee kwenye majukumu yetu tuache kujificha kwenye kivuli cha utafutaji,” amesema

Restuda Mruda ambaye ni mzazi amesema watoto wa kike wanahitaji msaada mkubwa wa malezi kutoka kwa wazazi ili kuwaepushia vikwazo  vinavyosababisha washindwe kutimiza malengo yao.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mugumu, Magreth Malongo amesema ushirikiano hafifu wa wazazi katika suala zima la elimu kwa watoto wa kike, bado ni changamoto inayosababisha wanafunzi hao kushindwa kufikia malengo yao.

“Asilimia 20 tu ya wazazi ndio wanakuwa tayari kushirikiana na kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni, hata ukiwaandikia barua mara nyingi hawaitikii wito wazazi wanapaswa kutambua kuwa malezi ya watoto ni ushirikiano baina yao na walimu,” amesema.

Amesema Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha mazingira kwa ajili ya wanafunzi, huku akitolea mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambayo imekuwa ikijitahidi kutenga bajeti kwa ajili ya taulo za kike kwa ajili ya wanafunzi kujistiri wakati wa hedhi.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Grumeti Fund, Frida Mollel amesema wameamua kuandaa makongamano ya aina hiyo baada ya kubaini uwepo wa changamoto zinazowakabili watoto wa kike na kuwa kikwazo katika safari yao ya elimu.

Amesema kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa wamewafikia wanafunzi zaidi 4,000 wa kike na kiume kutoka shule mbalimbali za sekondari wilayani humo, ambapo pamoja na mambo mengine wanalenga kuwajengea uwezo wa kupambana na changamoto zinazowakabili.

Amesema kupitia makongamano hayo wanatarajia kuwafikia wanafunzi zaidi ya 6,000 ambapo pamoja na elimu ya makuzi pia shirika hilo linatoa taulo  za kike kwa ajili ya kujistiri wakati wa hedhi.

Related Posts