Wanaomeza dawa kutibu kifua, mafua, kikohozi bila kupima waonywa

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na ongezeko la magonjwa ya mfumo wa upumuaji, hali hiyo imesababisha wimbi la watu kumeza dawa za viua vijasumu maarufu antibaotiki bila kupima au kufuata ushauri wa daktari, jambo ambalo limeonywa.

Hivi sasa kuna ongezeko la wagonjwa wa mafua, kifua na kikohozi katika maeneo mbalimbali nchini, hali inayosababisha baadhi ya watu kutumia dawa za hizo kiholela.

Wapo wanaotumia dawa hizo baada ya kusimuliana namna wanavyoumwa na kushauriana dawa za kumeza kwa kujiaminisha na historia kwamba fulani aliumwa hivyo, akatumia dawa fulani na kupona.

Wapo wengine hununua dawa na kumeza bila kupima wala kufuata ushauri wa daktari, wakiamini tatizo walilonalo linaponywa na dawa hizo, jambo lililoonywa kuwa hatari zaidi na huenda likamsababishia madhara zaidi mtumiaji.

Akizungumzia athari ya kumeza dawa hizo bila kupima na kufuata ushauri wa kitaalamu, aliyekuwa mkurugenzi wa kinga wa Wizara ya Afya, Dk Ali Mzige amesema suala la watu kununua na kunywa dawa kwa utashi linaongezeka hivi sasa na halifai.

Amesema dawa zote zinazofaa kutibu binadamu zinapaswa kutolewa na mtu mwenye taaluma ya udaktari, sio watu kuambizana vitu vya uongo vijiweni na kumeza dawa bila kufuata ushauri.

Mtaalamu huyo wa afya ya jamii, amesema mtu anaponunua na kumeza dawa kwa utashi kunaleta matatizo matatu.

“Kwanza unaingia gharama ya kununua dawa ambazo sizo, pili unapomeza dawa hizo unatengeneza mwili wako uwe na usugu, kwani unameza dawa ambayo hao wadudu hawapo.

“Tatu inawezekana ukawa na tatizo kubwa zaidi kuliko dawa unazozitumia, hivyo ukaishia kwenye matatizo ya ziada,” amesema.

Ameshauri kabla ya kumeza dawa, lazima mhusika apate ushauri wa daktari, kujua anaumwa nini na apate vipimo sahihi.

“Kuna wimbi la watu wanaambizana vitu vya uongo huko vijiweni, si madaktari lakini wanajifanya ni madakatari kwa kushauri kuhusu matumizi ya dawa, kuwasikiliza ni hatari na kutakupotezea maisha,” amesema.

Mwishoni mwa wiki, akizungumza na Mwananchi, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe alisisitiza wagonjwa wasitumie dawa za antibaotiki au za malaria kabla ya kupima.

“Watanzania wanapoona dalili ambazo zinafanana na malaria wakienda hospitali wakiambiwa hawana malaria, basi wasitumie dawa za malaria au antibaotiki kwa kudhani labda vipimo vimekosea au mtoa huduma akawalazimisha kutumia dawa hizo jambo linaloleta usugu wa dawa za malaria na antibaotiki,” alisema.

Takwimu zinaonyesha matumizi ya dawa dhidi ya vimelea nchini yanakadiriwa kufikia asilimia 62.3, sambamba na makadirio ya usugu kwa asilimia 59.8 huku utafiti ukionyesha wengi hutumia antibaotiki bila ushauri wa daktari.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) Moshi ulionyesha asilimia 92.3 ya wauzaji 82 walisambaza dawa hizo bila cheti cha dakktari mwaka 2017.

“Utafiti wa mwaka 2021 zaidi ulionyesha kati ya watumiaji watumiaji 960 jijini Dar es salaam, asilimia 70.6 walijibu kwamba waliacha kutumia antibiotiki baada ya dozi kukamilika, na asilimia 42.3 hutumia iwapo zilibaki nyumbani au kwenda kununua ikiwa ndugu au rafiki zilimsaidia,” alisema Profesa kutoka Idara ya Viuavijasumu Muhas, Mecky Isaac Matee.

Alisema asilimia 57 kati ya wanafunzi 374 wa vyuo vikuu viwili vya Moshi walinunua wenyewe dawa bila ushauri wa daktari kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2021.

Related Posts