Dar es Salaam. Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wanawashikilia baadhi ya waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
Kamanda Muliro amesema hayo leo Jumanne Juni 3, 2025 wakati akizungumza na Wasafi FM kuhusu kuwakamata waumini hao waliokaidi kanisa hilo kufungwa.
“Kutokana na hilo ilibidi kuna watu tuwachukue ili kuongea nao ili tujue ukweli walikuwa hawaelewi kilichokuwa kinatekelezwa na maofisa wa polisi au walikuwa wanafanya tu kukataa ili kusasabisha fujo,” amesema Kamanda Muliro.

Waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima lililopo Ubungo Dar es Salaam wakiwa wamekaa nje ya kanisa hilo.
Amesema wao wapo kwa ajili ya kusimamia sheria ambayo imeelekezwa kisheria kinatekelezeka kwa kutokuendelea kufanya shughuli zilizokuwa zikifanyika.
Aidha, amesema kama muhusika anataka kuendelea kufanya shughuli ya awali wanatakiwa kufuata utaratibu wa kisheria ikiwa ni pamoja na kukata rufaa kwenye mamlaka za kisheria.
“Wanaweza kukata rufaa kwa mamlaka za kisheria zilizowekwa na kama wakiruhusiwa na sisi tutakuwa kwenye mtazamo uleule wa kisheria na kutokuwa na pingamizi,” amesema Kamanda Muliro.
Jana Jumatatu, Juni 2, 2025, Serikali ilitangaza kulifuta kanisa hilo linalomilikiwa na Askofu Gwajima kwa madai limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.
Ni ulinzi eneo lote! Ndiyo hali halisi ilivyo kwenye Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima, Ubungo Dar es Salaam.

Kanisa hilo limezungushwa utepe wa njano wenye maandishi meusi huku askari polisi zaidi ya 20 wakiwa wamelizunguka kuimarisha ulinzi.
Askari hao wenye silaha wametanda katika maeneo mbalimbali kuzunguka kanisa hilo ambalo limefutwa.