Yuko wapi Askofu Gwajima? Waumini njiapanda, Polisi yatoa kauli

Dar es Salaam. Yuko wapi Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, kwa sasa ndilo swali ambalo waumini wake wanajiuliza baada ya purukshani za usiku wa Juni 2, 2025. Waumini wa kanisa walivamiwa na polisi wakati wakiendelea na ibada na kwamba, mpaka sasa hawafahamu mahali alipo kiongozi wao wa kiroho.

Purukushani baina ya polisi na waumini hao zilianza usiku wa kuamkia leo Jumanne, Juni 3, 2025 baada ya askari Polisi wakiwa na silaha kufika kanisani hapo wakati ibada ikiendelea na kuwataka waumini kuondoka.

Polisi walifika kanisani hapo baada ya Serikali kutangaza kulifuta kwa maelezo limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

“Baba (Askofu Gwajima) wakati vurugu na polisi zinatokea alikuwepo, katika vurugu zile hatujui yupo wapi,” amesema Mchungaji Christian Laisubira wa kanisa hilo.

Baadhi ya waumini wamekusanyika upande wa pili wa barabara wakilitzama kwa mbali kanisa lao ambalo limezingirwa na polisi wenye silaha huku ukiwekwa utepe kuashiria shughuli zimesimamishwa.

Hata hivyo, Mchungaji Christian amesema  hawataondoka eneo hilo hadi watakapofahamu hatima ya kiongozi wao huyo, ambaye wanadai hadi leo Juni 3, saa 2:50 asubuhi hawafahamu mahali alipo.

Akizungumzia tukio la kuvamiwa na polisi wakiwa katika maombi kanisani, Mchungaji Christian amesema lilikuwa ni tukio la kushangaza.

Polisi wakiwa wamekaa nje ya Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Ubungo Dar es Salaam.

“Askari walivamia kanisani na kuanza kukamata watu, kadri muda ulivyoongezeka zilitokea vurugu. Wamekamata watu zaidi ya 100, wamewapiga wengine, usiku wote tuko hapa, tutaendelea kuwa hapa kujua hatima ya baba yetu,” amedai.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akizungumzia tukio hilo kwenye kituo cha radio cha Wasafi leo asubuhi amesema wamawashikilia baadhi ya waumini wa kanisa hilo.

“Kutokana na hilo ilibidi kuna watu tuwachukue ili kuzungumza nao watueleze kwa undani kama walikuwa hawaelewi kilichokuwa kinatekelezwa na maofisa wa polisi au walikuwa wanafanya tu kukataa ili kusasabisha fujo,” amesema Kamanda Muliro.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro

Amesema wao wapo kwa ajili ya kusimamia sheria ambayo imeelekezwa kisheria kinatekelezeka kwa kutokuenedelea kufanya shughuli zilizokuwa zikifanyika.

Kamanda Muliro amesema kama muhusika anataka kuendelea kufanya shughuli ya awali wanatakiwa kufuata utaratibu wa kisheria ikiwa ni pamoja na kukata rufaa kwenye mamlaka za kisheria.

“Wanaweza kukata rufaa kwa mamlaka za kisheria zilizowekwa na kama wakiruhusiwa na sisi tutakuwa kwenye mtazamo uleule wa kisheria na kutokuwa na pingamizi,” amesema Kamanda Muliro pasipo kueleza kama wanashikilia Askofu Gwajima.

Jana Jumatatu, Juni 2, 2025, Serikali ilitangaza kulifuta kanisa hilo linalomilikiwa na Askofu Gwajima kwa madai limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima lililopo Ubungo Dar es Salaam wakiwa wamekaa nje ya kanisa hilo.

Mzizi wa hayo ni mkutano wa Askofu Gwajima na waandishi wa habari, alioutumia kueleza anavyochukizwa na matukio ya kutoweka na kutekwa kwa watu, huku akitoa mfano wa hali ingekuwaje iwapo matukio hayo yangewakuta watoto wa viongozi akiwemo yeye mwenyewe.

Uamuzi wa kulifuta ulitangazwa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa kupitia barua yake kwenda kwa Askofu Gwajima na nakala kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camilius Wambura.

Kwa mujibu wa barua hiyo inaeleza, katika siku za karibuni, Askofu Gwajima alionekana katika mimbari ya kanisa hilo, akitoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Barua hiyo inaeleza vitendo hivyo ni kinyume cha Kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, ikisomwa pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria Namba 3 ya mwaka 2019, kwa kuwa vinahatarisha amani na utulivu nchini.

“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 17(b) cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kikisomwa pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria Namba 3 ya mwaka 2019 kilichoifanyia marekebisho kifungu cha 2 cha Sheria ya Jumuiya.

Baada ya uamuzi huo, jana jioni kulifanyika Ibada kanisani hapo ya maombi ya siku saba ambapo Askofu Gwajima alisema katika maombi hayo watawaombea viongozi wa kisiasa akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na vyama vya siasa: “Ili jua la haki liweze kuzuka.”

Katikati ya maelezo yake, Askofu Gwajima baada ya nyimbo za kusifu akasema: “Nafikiri mmeona kwenye mtandao watu wanapitisha karatasi kwamba Kanisa la Ufufuo na Uzima limefungwa, hakuna wa kufunga kanisa la Mungu duniani, si kweli ni uongo ni wahuni hao wahuni…barua hiyo siyo ya Serikali, Serikali yetu haiwezi kufanya hivyo,” ameongeza:

“Serikali yetu ni nzuri haifanyagi mambo kama hayo. Tunaendelea na maombi katika makanisa yetu zaidi ya 2,000 yako mtandaoni leo tutaendelea, kesho mpaka siku saba tutafunga mchana tu, tunakunywa maji tu na tunamlilia Mungu kuwa jua la haki lizuke, amani itawale Tanzania na ushindi utawale.” 

Endelea kufuatilia Mwananchi

Related Posts