Mradi wa Sh216 milioni utakavyonufaisha wakaanga samaki feri

Dar es Salaam. Mradi wa gesi itokanayo na mafuta (LPG) wa zaidi ya Sh216 milioni ulioendelea kufungwa Soko la Kimataifa la Samaki Ferry, Mtaa wa Kivukoni Kata ya Kivukoni jijini Dar es Salaam unatarajiwa kuwanufaisha wakaanga samaki 48 sokoni hapo.

Mbali na kuwanufaisha katika shughuli za kukaanga samaki, mradi huo unatajwa kuwaepusha wafanyabiashara hao na athari za matumizi ya nishati isiyo safi, ya ikiwemo kuni.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne Juni 3, 2025 wakati kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ali Ussi akikagua mradi huo uliopo sokoni hapo.

Hayo yanajiri wakati Serikali ikisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo inataka hadi ifikapo mwaka 2034, Watanzania wanne kati ya watano wawe wanatumia nishati safi.

Ussi amesema mradi huo wa gesi utawasaidia watumiaji kuepuka athari za matumizi ya kuni.  “Soko la feri mnatunza mazingira mradi wa kisasa wa gesi unaunga mkono kampeni ya Serikali ya kutumia nishati safi ya kupikia.”

“Mradi huu unatarajiwa kuwanufaisha wakaanga samaki, ambao kila mmoja atafungiwa mita na kulipia kwa kadiri anavyotumia na kupata manufaa,” imebainishwa.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema, mradi utaokoa kipato cha wakaanga samaki kwa kuwa watatumia gesi badala ya kuni.

Zikitajwa faida za mradi huo unatekelezwa kwa msaada wa Kampuni ya Oryx Gas una thamani ya Sh216 milioni miongoni ni kusaidia kuokoa misitu inayokatwa kutokana na matumizi ya mkaa na kuni.

Mradi huo ambao jiji jimeingia mkataba na kampuni hiyo, unatarajiwa kufanya kazi kwa muda wa miaka kumi na baada ya hapo utakabidhi kwa halmashuri ili iendelee kuendesha mradi kama moja ya vyanzo vyake vya mapato.

Mmoja ya wakaanga samaki sokoni hapo ambaye hakutaja jina lake, amesema ni hatua nzuri kwa kuwa anaenda kuachana na nishati isiyo safi badala yake atatumia gesi ambayo itamrahisishia shughuli zake hizo.

“Moshi pia tutaepukana nao, hivyo kusaidia afya ya macho na vifua vyetu. Suala la matumizi ya nishati safi si sokoni tu, hata majumbani haliepukiki,” amesema mfanyabiashara huyo.

Katika hatua nyingine ya ukaguzi wa mwenge wenye ujumbe usemao; Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 chini ya kaulimbiu “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu” umekagua mradi wa barabara wa Magengeni.

Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ya Magengeni-Chang’ombe hadi Senene wenye urefu wa kilometa 0.5 kwa kiwango cha lami wenye thamani ya Sh678 milioni fedha za ndani unatajwa kupunguza foleni kwa watumiaji.

Meneja wa Wakala wa barabara vijijini na Mijini (Tarura) Wilaya ya Ilala, John Chacha amesema barabara hiyo inaunganisha barabara zingine katika Kata ya Liwiti zinazolisha na kutoa katika barabara kuu ya Tabata- Segerea kama vile barabara ya Baracuda-Chang’ombe.

“Kukamilika kwa barabara hii kutapunguza msongamano kwenye barabara hiyo ya Tabata Segerea na Baracuda Chang’ombe , kurahisisha usafiri kwa wakazi na wafanyabiashara wa Mtaa wa Magengeni na kuwa sehemu ya kichocheo cha kukua kwa uchumi kwa wananchi wa Ilala.”

Hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 70 na fedha zilizotumika hadi sasa ni Sh385 milioni sawa na asilimia 52.

Amesema mradi huo umetoa ajira kwa wananchi wapatao 50, kurahisisha shughuli za usafiri na usafilishaji na kuongeza ukuaji wa uchumi katika Wilaya na Mkoa kwa ujumla, kwa kuwa unaunganisha mitaa yenye shughuli mbalimbali za uzalishaji.

“Aidha, mradi huu unatarajiwa Kupunguza msongamano wa magari katika barabara ya Tabata Segerea na Baracuda-Chang’ombe ambazo zinatumika muda wote usiku na mchana kwa kuwa Dar es Salaam ni kitovu cha Kibiashara katika nchi yetu,” amesema.

Related Posts