Kamati yaitaka Wizara ya Maji kuongeza usimamizi wa miradi

Unguja. Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi imetoa wito kwa Wizara ya Maji Zanzibar kuhakikisha inapanga na kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi yake, kutokana na malalamiko ya wananchi kuhusu upungufu wa huduma muhimu kama maji, nishati na ardhi.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo leo Juni 3, 2025 katika Baraza la Wawakilishi, Waziri Shaibu Hassan Kaduara ameomba baraza hilo lihidhinishe Sh220.825 bilioni kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele 10 vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Kwa mujibu wa Kaduara, kati ya kiasi hicho, Sh2.438 bilioni ni kwa matumizi mengineyo, Sh2.920 bilioni kwa mishahara, Sh10.110 bilioni ruzuku ya mishahara na Sh205.356 bilioni kwa miradi ya maendeleo.

Waziri huyo amesema wizara itaendelea kufanya tafiti, kuboresha usambazaji wa maji safi na salama, nishati na huduma za madini kupitia uimarishaji wa miundombinu na uwezo wa taasisi zilizo chini yake.

Kuhusu huduma ya maji, Kaduara amesema hadi kufikia Machi 2025, uzalishaji wa maji kwa upande wa Unguja umefikia lita milioni 154 kwa siku wakati mahitaji ni lita milioni 190 kwa siku, hali inayoonyesha upungufu wa lita milioni 36 kila siku.

Kwa upande wa Pemba, uzalishaji wa maji umefikia lita milioni 56 kwa siku dhidi ya mahitaji ya lita milioni 87, hivyo kuwepo kwa upungufu wa lita milioni 31 kwa siku.

Kaduara amesema kuwa mpango wa kuboresha huduma ya maji unatekelezwa kwa kushirikiana na kampuni ya Rand Water Zanzibar, inayosimamia shughuli za Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa). Kampuni hiyo inatarajiwa kusimamia na kuendesha miundombinu ya maji, kutoa huduma, kukusanya mapato na kujenga uwezo wa watendaji wa mamlaka hiyo.

Amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/26, Rand Water inatarajia kutumia Sh13.289 bilioni kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake, kupitia mapato ya mauzo ya maji na huduma nyingine.

Kuhusu sekta ya nishati, Kaduara amesema wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2025, kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi ya nishati mbadala, kufanya tafiti za vyanzo vya nishati na kusimamia miradi kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Zanzibar (Zura) na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco).

Amesema kuwa Zeco inatarajia kukusanya na kutumia Sh265.326 bilioni kwa ajili ya kazi za kawaida na miradi ya maendeleo, fedha ambazo zinatokana na mauzo ya umeme, huduma mbalimbali na makusanyo ya madeni ya nyuma.

Akitoa maoni ya Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi, Mwenyekiti Yahya Rashid Abdalla amesema licha ya juhudi za wizara, bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji na umeme kwa wananchi.

Amesema huduma ya maji bado inakumbwa na matatizo ya usambazaji hafifu na upotevu mkubwa wa maji kutokana na uchakavu wa miundombinu, huku umeme ukikatika mara kwa mara au kuwa wa kiwango cha chini, hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi na kuathiri shughuli zao za kiuchumi na kijamii.

“Tunaomba wizara ijipange vyema na kuhakikisha vipaumbele vinavyopangwa vinatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya,” alisema.

Related Posts