Bwana Rémy Rioux, Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AfD), akizungumza mbele ya wajumbe wa Mkutano wa siku mbili wa Bodi ya Taasisi ya Ubia wa Elimu Duniani (Global Partnership for Education – GPE) unaofanyika mjini Paris, Ufaransa, leo tarehe 3 Juni 2025, chini ya uenyekiti wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Mkutano huo umewakutanisha wajumbe zaidi ya 40 wanaowakilisha makundi mbalimbali ya ubia huo, wakiwemo wawakilishi kutoka nchi saba tajiri zaidi duniani (G7), pamoja na nchi washirika kutoka kanda zinazoendelea kiuchumi, hasa Afrika na Asia. Vilevile, mashirika mbalimbali ya kimataifa yanashiriki katika mjadala huo muhimu wa elimu.
Katika kikao hicho, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Ali Jabir Mwadini, alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Ufaransa kwa ushirikiano thabiti uliopo kati ya Tanzania na Ufaransa. Alisisitiza utayari wa Tanzania kuendeleza na kukuza zaidi mahusiano hayo ya kidiplomasia na ya kimkakati kwa manufaa ya pande zote mbili, hasa katika sekta ya elimu.
Mkutano huo wa GPE unalenga kujadili namna taasisi hiyo inaweza kuhimili na kukabiliana na changamoto za sasa duniani, ikiwemo mabadiliko ya sera za kimataifa, huku ukibeba matumaini ya kuboresha usawa na ubora wa elimu katika nchi zinazoendelea.
