Moshi. Shughuli ya kuaga miili ya wanandoa Geofrey Motta (60) na Blandina Ngowi (53), wanaodaiwa kuuawa na mtoto wao inaendelea katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Msaranga Mandaka, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Wanandoa hao ambao ni wakazi wa Msufuni, Msaranga, wanadaiwa kuuawa kikatili kwa kukatwa shingo na mwingine kunyongwa usiku wa Mei 29, 2025 kisha miili yao kutelekezwa kwenye nyumba waliyokuwa wamepanga eneo la Msufuni, Msaranga, Manispaa ya Moshi.
Baada ya ibada ya mazishi kumalizika kanisani hapo miili hiyo itapelekwa katika mtaa wa Kariwa Chini, kata ya Rau, wilayani humo kilomita chache kutoka kanisani hapo kwa ajili ya maziko ambayo yatafanyika leo Jumatano, Juni 4, 2025.
Ndugu, jamaa na marafiki wamehudhuria ibada hiyo ya safari ya mwisho kwa wanandoa hao.

Majeneza yenye miili ya wanandoa Geofrey Mota (60) na Blandina Ngowi (53) yakiwa katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Msaranga Mandaka, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Mei 30, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo ambapo alisema wanandoa hao waliuawa Mei 29, 2025 ndani ya nyumba ya kupanga waliyokuwa wanaishi eneo la Msufuni.
Mpaka sasa Jeshi la polisi mkoani humo linaendelea kumtafuta mmoja wa kijana wa familia hiyo ambaye alitoweka baada ya kutokea mauaji hayo.
Kamanda Maigwa alisema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo cha mauaji hayo na kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Baadhi ya watoto wa marehemu, Geofrey Motta (60) na Blandina Ngowi(53) wakiaga miili ya wazazi wao katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Usharika wa Msaranga Mandaka, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
“Tukio hilo limetokea ndani ya nyumba ya kupanga waliyokuwa wakiishi wanandoa hao pamoja na kijana wao wa kiume (jina limehifadhiwa) ambaye ametoweka baada ya mauaji hayo kutokea,”alisema Kamanda Maigwa