Dar es Salaam. Tatizo la harufu mbaya mdomoni liweza kusababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo kuoza kwa mabaki ya chakula, usafi duni wa kinywa, magonjwa ya fizi pamoja na maambukizi ya bakteria katika kinywa.
Hali hiyo huwakumba watu mbalimbali katika jamii. Wapo wanaojua na wasiojua kama vinywa vyao vinatoa harufu mbaya.
Hata hivyo, wataalamu mbalimbali wa afya wanasema kuwa pamoja na matibabu, uzingatiaji wa lishe unaweza kusaidia kupunguza au kuondoa kabisa tatizo hilo na kuimarisha afya ya kinywa kwa ujumla.
Mboga za majani na matunda
Kwa mujibu wa tovuti ya afya ya WebMD, matumizi ya mboga za majani matunda, yanaweza kusaidia kupunguza au kuondoa kabisa changamoto ya harufu kinywani.
Miongoni mwa mboga na matunda ambayo yamesisitizwa kwa mtu mwenye changamoto hiyo ni pamoja na tufaha (apple), machungwa, limao, karoti, majani ya mnanaa (Mint).
Inaeleza kuwa matunda na mboga vina virutubisho vingi kama vitamini A na C, ambavyo ni muhimu kwa afya ya fizi na tishu laini za mdomoni, Pia, vina nyuzinyuzi ambazo husaidia kuimarisha afya ya kinywa.
Majani ya mnanaa yanaelezwa kuwa na viambato vinavyosaidia kuondoa harufu mbaya kinywani na kukifanya kuwa na afya huku matunda yenye wingi wa Vitamini C kama vile machungwa, maembe na mengineyo katika kundi hilo, yakisaidia na kupambana na bakteria ambao wanaweza kusababisha harufu mbaya mdomoni.
Vyakula vyenye wingi wa kalisi
Kwa mujibu wa tovuti ya healthline vyakula vyenye wingi wa madini ya kalisi (calcium) kama vile maziwa na bidhaa zinazotokana nayo, samaki na vinginevyo husaidia kuimarisha meno na mifupa.
Meno yenye nguvu yanahitaji kiwango cha kutosha cha kalisi ili kuzuia kuoza au kupasuka kwa urahisi.
Meneja mradi wa afya ya mama na mtoto na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Word Vision, Dk Daud Gambo anasema unywaji wa maji kwa wingi angalau glasi kumi kwa siku, husaidia kusafisha kinywa na kuondoa mabaki ya chakula pamoja na bakteria. Pia, huzuia ukavu wa kinywa unaoweza kuchangia kuoza kwa meno.
Daktari wa binadamu, Shitta Samweli anasisitiza kuepuka aina ya vyakula vyenye sukari nyingi.
“Kula pipi, soda, keki, na vyakula vingine vyenye sukari nyingi mara kwa mara huongeza hatari ya matatizo ya meno, ”anasema.
Anaongeza kuwa ni muhimu kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya ya kinywa na meno angalau mara mbili kwa mwezi.