Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche amesema chama hicho kimeamua kwenda mahakamani kuishtaki Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikidai haina nia njema na chama hicho.
Ameeleza hayo leo Jumatano Juni 4,2025 wakati akisoma maazimio ya kamati kuu ya chama hicho iliyoketi jana kujadili barua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa.
“Kamati inaelekeza wanachama hadi kufikia Alhamisi Juni 9,2025 shauri liwe limepelekwa mahakamani na madai ya msingi tumejiridhisha kuwa msajili wa vyama siasa hana mamlaka ya kutafsiri katiba ya chama, kwa namna anavyoona yeye tofauti na uhalisia.
“Tunakwenda mahakamani kwa sababu Msajili amejipa jukumu kama mtafsiri wa katiba yetu na anajiona anajua nini katiba yetu inazungumza tofauti na sisi na wengine wote,”amesema Heche.
Heche amesema chama hicho kinakwenda mahakamani kwa sababu Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeamua kuzuia ruzuku ya chama hicho.
“Sheria ya Vyama vya Siasa anayoisimamia Msajili kifungu cha 18 (6), msajili ana uwezo wa kuzuia ruzuku ya vyama au kwa chama kingine chochote pale ambapo kuna dosari ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu ya Serikali (CAG)
“Sasa kama tungekuwa na hati mbaya au… kwa mujibu wa kifungu cha 18 (6) hapo msajili angepata mamlaka ya kuzuia ruzuku, kwa kutuandikia barua na kuonyesha sababu,” amesema Heche.
Hata hivyo, Heche amedai Msajili ameamua kujifanyia kwa kuchukua uamuzi huo, akisema Chadema kinakwenda mahakamani kupingia hatua hiyo.