Bidhaa za plastiki bado mfupa mgumu

Dar es Salaam. Mageuzi ya kisera yatakayozuia uingizwaji wa plastiki Tanzania, kuanzisha mifuko itakayohamasisha urejelezaji wa taka zimetajwa kuwa njia zinazoweza kukomesha matumizi ya plastiki nchini.

Kwa sababu licha ya jitihada zinazofanywa na mamlaka mbalimbali lakini fedha nyingi bado zinatumika na zinaendelea kuongezeka katika kuagiza bidhaa za plastiki kutoka nje ya nchi.

Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa zaidi ya Sh2.12 trilioni zinatarajiwa kutumika katika kuagiza bidhaa za plastiki kutoka nje ya nchi mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh1.45 trilioni mwaka uliotangulia.

Ripoti hii ya tathmini ya hali ya uchumi ya Aprili mwaka huu inalitaja ongezeko hili kuwa kubwa kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka minne iliyopita tangu mwaka 2021.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2023 ndiyo awali ulikuwa ukiongoza kwa fedha nyingi kutumika kuagiza bidhaa za plastiki, ambapo Sh1.9 trilioni zilitumika ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka Sh1.7 trilioni mwaka 2022 na Sh1.1 trilioni mwaka uliotangulia.

Ili kukomesha suala hili, wadau wanapendekeza kuwapo kwa sera itakayodhibiti uingizwaji wa bidhaa za plastiki kutoka nje hasa ambazo haziwezi kurejelezwa sambamba na kuanzishwa kwa mfuko utakaosaidia vikundi vinavyobadilisha taka kuwa bidhaa.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utu na Mazingira (Hudefo), Sarah Pima amesema pamoja na jitihada ambazo tayari zimefanywa na Tanzania ni wakati sasa wa kuangalia namna sera zinavyoweza kutumika kudhibiti plastiki zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.

Hilo lifanyike kwa kutupia jicho mipakani ili kuhakikisha jitihada za ndani hazikwamishi na nchi jirani ili kulinda mazingira.

“Pia tuangalie ulazima wa hizo bidhaa zinazoingizwa kuwa kwenye plastiki, pia tuangalie namna wananchi watakavyonufaika na bidhaa hizo bila kuathiri mazingira,” amesema Pima.

Amesema njia nyingine inayoweza kutumika ni kuwekeza fedha na teknolojia ya kurejeleza mabaki au bidhaa za plastiki kupitia vikundi mbalimbali.

“Pia tuangalie ni kwa kiasi gani jambo hili lina soko, tukiangalia kwa jicho hilo tunaweza kumaliza matumizi ya plastiki, sheria kali nazo zinaweza kusaidia katika mapambano haya,” amesema Pima.

Suala hilo liliungwa mkono na Meneja wa Mradi wa Uchumi Rejeshi (circular economy) kutoka Catholic Relief Servses (CRS) Robert Muganzi ambaye amesema ni wakati sasa Tanzania kuja na sera inayodhibiti aina fulani za plastiki zisiingie nchini, bila kujali zimefunga bidhaa gani hasa ambazo haziwezi kurejelezwa.

“Aina hii ya plastiki ni zile ambazo hata ukiweza kuzirejeleza utatumia nguvu nyingi sana. Watengeneze sera bila kujali plastiki inatoka nchi gani na kuweka bayana kuwa bidhaa yoyote inayowekwa katika kifungashio cha aina hii hakitaingia nchini,” amesema Robert.

Hilo liende sambamba na kutengeneza ‘circular economy’ ambao utahamasisha urejelezeshaji na kutumia upya bidhaa hizo za plastiki baada ya matumizi yake ya awali (re-use) katika kufanya kitu kingine.

Ili kufanikisha hilo alipendekeza kuwapo kwa mfuko ambao utawezesha vikundi mbalimbali ikiwemo vya kina mama na vijana ambao wanafanya urejelezeshaji katika maeneo mbalimbali.

“Tuweke mfuko ambao utasaidia jambo hili pekee, kama hatujafikia hatua hii tutumie zile asilimia 10 za halmashauri kwa kuangalia angalau asilimia sita zinakwenda huku kwa ajili ya kulinda mazingira yetu,” amesema Robert.

Jambo lingine aliloshauri ni Serikali kuangalia namna ya kutambua waokota taka kwani hadi sasa ni ngumu kujua kiwango cha plastiki kinachozalishwa Tanzania au zinazoingia nchini.

“Kuna ombwe kubwa la takwimu hasa za upande huu wa plastiki, kinachotakiwa kufanyika kwa wanaokusanya plastiki mtaani wafanywe kuwa rasmi na utengenezwe mfumo wa kuchukua takwimu na kuangalia kiwango cha plastiki zinazokusanywa katika maeneo mbalimbali,” amesema.

Jambo hilo litasaidia kuwajua watu waliopo katika mzunguko wa uongezaji wa thamani wa plastiki na itasaidia kujua sehemu gani Dar es Salaam au Tanzania linaloongoza kwa kuwa na taka za plastiki nyingi.

Hilo litasaidia pia kujua tabia za kipato cha watu na matumizi ya chupa za plastiki ili kuweka urahisi katika kupambana na suala hilo, tofauti na sasa waokota chupa hizo wasivyoonekana kuwa na thamani mbele ya jamii.

Haya yanasemwa wakati ambao hata mifuko ya plastiki (Rambo) iliyopigwa marufuku nchi kuonekana kurejea kwa kasi jambo ambalo linakwamisha jitihada hizo.

Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Jamal Baruti alipozungumza na wanahabari Mei 26 mwaka huu alisema jumla ya tani 250 za mifuko haramu ya plastiki zilikuwa zimekamatwa ambapo kati ya hizo, tani 130 zimetoka Mkoa wa Pwani pekee.

Alipokuwa akizungumzia siku ya mazingira, Mei 26, 2025 Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dk Immaculate Semesi alisema baraza hilo linaendelea kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kushirikiana na kikosi kazi maalumu chenye taasisi saba, chini ya uratibu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, ambapo NEMC inashiriki kama Makamu Mwenyekiti.

“Matumizi holela ya plastiki ni changamoto kwa mazingira hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kuchukua hatua binafsi za kuyadhibiti, badala ya kusubiri utekelezaji wa sheria pekee hivyo ni vyema wananchi kutumia falsafa ya “punguza, tumia tena na rejeleza” kama njia bora ya kukabiliana na tatizo la taka za plastiki,” alisema.

Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa mwaka 2025 yanachagizwa na kaulimbiu isemayo. “Mazingira yetu na Tanzania Ijayo Tuwajibike Sasa, Dhibiti Matumizi ya Plastiki’ inayolenga kuikumbusha jamii kuwa mazingira na rasilimali zake ni msingi wa uhai na maisha.

Juni Mosi, mwaka huu, akiwa katika viwanja vya maonyesho ya siku ya mazingira jijini Dodoma, Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati, Novatus Mushi alitoa wito kwa Watanzania kupunguza matumizi ya plastiki na kuchakata taka ili kuunga mkono lengo hilo.

Alisema kupitia maonyesho ya siku ya mazingira, Baraza linatumia fursa hiyo kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kudhibiti taka za plastiki na fursa za kiuchumi zinazopatikana kupitia usimamizi huo.

“Hii ni sehemu ya jitihada zetu za kuendeleza uchumi rejelezi, ambao unalenga kubadilisha taka za plastiki kuwa bidhaa zenye manufaa. Kila mwananchi ana jukumu la kupunguza uchafuzi wa plastiki,” alisema.

Related Posts