Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imepanga kuanzisha Chuo cha Usimamizi wa Fedha Zanzibar (ZIFA) ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha elimu ya juu na usimamizi wa rasilimali fedha nchini.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya, akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 leo Juni 4, 2025, amesema maandalizi ya kutunga sheria ya kuanzisha chuo hicho yameanza na chuo hicho kitasimamiwa na Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango.
Chuo hicho kitachukua nafasi ya Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Kwa mujibu wa Dk Mkuya, ZIFA imepangiwa ruzuku ya Sh915 milioni kwa mwaka wa fedha ujao kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na utekelezaji wa mikakati ya maendeleo.
Mikakati hiyo ni pamoja na kukamilisha sheria na nyaraka muhimu, kupitia na kuandaa mitaala ya mafunzo ya muda mrefu na mfupi, kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuajiri watumishi 80 wakiwemo wahadhiri 50 na wahadhiri wasaidizi 30, ili kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kushindana kimataifa.
Mbali na hilo, katika bajeti hiyo, Serikali pia imeweka vipaumbele vingine tisa vya utekelezaji, kikiwemo cha kuongeza mapato ya ndani kupitia vyanzo vipya.
Serikali inatarajia kukusanya Sh6.527 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ongezeko la asilimia 33 kutoka makadirio ya Sh4.901 trilioni ya bajeti ya mwaka uliopita.
Ongezeko hilo linatokana na maboresho ya mifumo ya ukusanyaji wa mapato, vyanzo vipya vya mapato, pamoja na mikopo ya ndani itakayotumika kugharamia miradi ya maendeleo.
Vipaumbele vingine ni usimamizi bora wa mapato ya Serikali, kubuni vyanzo mbadala vya fedha kama hati fungani zinazozingatia misingi ya Kiislamu (Sukuk), kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi kupitia mfumo wa PPP, kukamilisha Soko la Mitaji Zanzibar (ZSE), pamoja na kuimarisha mfumo jumuishi wa usimamizi wa miradi ya maendeleo Zanzibar (ZIPS).
Aidha, Serikali imepanga kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (ZADEP 2026–2031), mkakati wa mawasiliano, ufuatiliaji na tathmini, sambamba na kuendeleza bajeti inayozingatia jinsia na usawa wa kijinsia katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Kwa upande wa makusanyo ya mapato, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) inatarajiwa kukusanya Sh1.257 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 49 kutoka makadirio ya Sh845.979 bilioni ya mwaka uliopita. TRA upande wa Zanzibar inakadiriwa kukusanya Sh825.769 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 38 kutoka makadirio ya Sh600.082 bilioniza mwaka uliotangulia.
ZRA pia itapokea ruzuku ya Sh30.156 bilioni kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kugharamia mishahara na matumizi mengine ya ofisi.
Katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango imetenga Sh707 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26 kutekeleza programu tano na miradi saba ya maendeleo.
Miongoni mwa fedha hizo, Sh210.399 bilioni zitatumika kulipia fidia kwa miradi ya maendeleo na Sh312 bilioni kwa ulipaji wa madeni yanayohusiana na miradi hiyo.
Moja ya programu kubwa inayotarajiwa kutekelezwa ni Ukuzaji wa Uchumi Jumuishi Zanzibar (BIG-Z), inayolenga kuimarisha hali ya maisha na maendeleo ya kiuchumi kupitia ujenzi wa miundombinu, ambapo Sh32.5 bilioni zitatolewa kupitia mkopo kutoka Benki ya Dunia.
Akisoma maoni ya Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mwanaasha Khamis Juma amesema kuwa kiwango cha makusanyo ya mapato kwa mwaka 2024/25 hakiridhishi.
Hadi kufikia Machi 2025, ni Sh2.045 trilioni tu zilizokuwa zimekusanywa kati ya makadirio ya Sh4.901 trilioni, sawa na asilimia 42.
Aidha, mapato kutoka vyanzo vya mikopo na misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo yamefikia asilimia 20 pekee, huku gawio la mashirika ya umma likiwa asilimia 24.
Kamati imeishauri wizara kuongeza juhudi za ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha matumizi yanaendana na vipaumbele vya Serikali katika miradi ya maendeleo.