Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaandaa sera mahususi itakayowalazimisha wawekezaji kutoa kiwango mahususi kwa ajili ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), badala ya kila mwekezaji kutoa kiwango anachotaka mwenyewe.
Mbali na sera pia Serikali ipo mbioni kukamilisha kanuni zitakazoainisha asilimia ya kiwango hicho kwenye miradi hiyo inayozunguka jamii husika.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano Juni 4, 2025 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Ali Suleiman Mrembo wakati akijibu maswali ya wajumbe wa Baraza la wawakilishi Chukwani Zanzibar kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff.
Mrembo amesema kupitia sheria ya uwekezaji nambari 10 ya mwaka 2023 kipengele mahususi kimewekwa.
“Ufafanuzi wake utaoneshwa kwenye kanuni juu ya kuwataka wawekezaji kuchangia asilimia fulani katika faida zao kwa jamii, pia Serikali inaandaa sera mahususi inayoelekeza na kusimamia masuala yote ya CSR,” amesema Waziri Mrembo.
Mwakilishi wa Chonga, Suleiman Masoud Makame amesema kwa kawaida sera huwa inatangulia halafu inafuata sheria na kanuni lakini katika mpango huo inaonekana Serikali imekwenda kinyume na kuanza sheria kisha kufuata sera na kanuni, huku akihoji kuchelewa kwa kanuni hizo kwani sheria imetungwa tangu mwaka 2023.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Mrembo amesema hawajaenda kinyume kwa sababu sheria iliyotungwa ni kwa ajili ya uwekezaji wote, lakini sera sio ya uwekezaji bali ni kwa ajili ya CSR ambayo imo ndani ya sheria hiyo na kanuni zake.
“Hatuoni na hatujaenda kinyume, hapa tumetunga sheria ya uwekezaji kwa hiyo haya masuala ya CSR ni sehemu katika sheria hiyo lakini kwa kuliona hili imebidi litungiwe sera yake, kwa hiyo bado hatujachelewa kwa sababu haya ndio yanaandaliwa,” amesema.
Kuhusu swali aliliuliza Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Suleiman Ali Othman aliyetaka kujua asilimia ngapi itakayotolewa na wawekezaji hao ambayo itawekwa kwenye kanuni.
Waziri amesema kwa sasa hawezi kutaja kiwango kwa sababu bado kanuni zinaendelea kuandaliwa hivyo asilimia ya mchango wao itaanishwa kwenye kanuni hizo zitakapokamilika.
Katika swali la msingi Dk Mohamed amesema pamoja na kuongezeka kwa uwekezaji ambapo visiwa vingi vimepata wawekezaji na wameanza kuwekeza, bado jamii haijafaidika na miradi ya CSR kutoka kwa wawekezaji hao.
Amesema haijachukua muda mrefu kwa sababu kuna vyombo vitatu vitakuwa vinasimamia jambo hili kwa masilahi mapana ya jamii kunufaika na uwekezaji unaofanywa.
Kwa sababu ya jambo hilo lilikuwa la hiari, waziri amesema ni vigumu kupata idadi kamili ya wawekezaji wanaochangia masuala ya CSR katika miradi 466 ambayo imesajiliwa kuanzia Novemba 2020 hadi Machi, 2025.