Kibaha. Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, Kitte Mfilinge ametoa onyo kwa viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani humo, akiwataka kuepuka vitendo vya uonevu, chuki, na upendeleo dhidi ya wanachama wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.
Mfilinge ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Juni 4, 2025 wakati wa kikao maalumu cha viongozi wa UWT kilichofanyika Kibaha, mkoani Pwani.
Katika kikao hicho, Mfilinge amesisitiza umuhimu wa kuheshimu misingi ya demokrasia, haki, na usawa kwa kila mwanachama bila ubaguzi wowote.

Picha viongozi wa UWT Mkoa wa Pwani wakiwa kwenye kikao maalumu kilichofanyika leo Juni 4, 2025 Mjini Kibaha. Picha na Sanjito Msafiri
“Si jambo jema kwa kiongozi yeyote kutumia nafasi yake kuwanyanyasa au kuwazuia wanachama wengine wanaotaka kugombea kwa misingi ya chuki au makundi,” amesema.
Amesema kuwa chama hicho kina dhamira ya kuhakikisha kuwa kila mwanachama anapata haki yake ya kuchagua na kuchaguliwa bila kukiuka sheria za nchi au kanuni za chama.
Mfilinge ameongeza kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, viongozi wa UWT wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuimarisha mshikamano badala ya kugawa wanachama kwa misingi ya makundi au masilahi binafsi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Pwani, Zainabu Vullu amesema kuwa desturi ya CCM ni kujali utu, heshima ya kila mwanachama, hivyo viongozi hao wanapaswa kutembea na misingi hiyo muda wote, hasa wakati wa mchakato wa uchaguzi.
“UWT imejengwa juu ya msingi wa hekima. Viongozi wetu lazima wawe mstari wa mbele katika kutunza maadili hayo, kuhakikisha kila mwanachama anapewa nafasi ya kushiriki kwa haki na amani,” amesema Vullu.
Amesisitiza kuwa UWT itaendelea kuwa chombo cha kuimarisha ushiriki wa wanawake katika siasa kwa njia ya amani na mshikamano, huku ikilinda haki za kila mwanachama wa chama hicho.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa UWT kutoka wilaya zote za Mkoa wa Pwani, ambao kwa pamoja walikubaliana kuhakikisha uchaguzi ndani ya chama unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia taratibu rasmi.