Ukata unavyoweza kukwamisha maendeleo ya EAC

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni ushirikiano wa kikanda uliolenga kuimarisha mshikamano kati ya nchi wanachama katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Jumuiya hii ilianzishwa awali mwaka 1967 na nchi tatu za Kenya, Tanzania na Uganda, lakini ikavunjika mwaka 1977 kutokana na tofauti za kisera na kisiasa.

Hata hivyo, juhudi za kuifufua zilianza tena miaka ya 1990, na mwaka 1999, Mkataba wa kuanzisha upya EAC ulisainiwa rasmi, kisha kuanza kutekelezwa mwaka 2000.

Tangu wakati huo, EAC imepanuka na sasa inajumuisha pia nchi za Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia.

Malengo makuu ya EAC ni kuhimiza ushirikiano wa kikanda, kuendeleza maendeleo endelevu, na kuboresha ustawi wa wananchi wa ukanda wa Afrika Mashariki. Makao makuu ya EAC yako jijini Arusha.

Changamoto ya kifedha EAC

Pamoja na ukubwa na umuhimu wake kama moja ya jumuiya kuu za kikanda barani Afrika, EAC inakabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha ambayo inatishia kuathiri utendaji na ufanisi wake.

Mathalani Februari 7, 2025, Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Mueni Nduva, alitangaza rasmi kuahirishwa kwa vikao vya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa muda usiojulikana kutokana na changamoto kubwa za kifedha zinazokikabili chombo hicho.

Nduva amesema upungufu mkubwa wa fedha, umetokana na baadhi ya nchi wanachama kushindwa kulipa michango yao ya kifedha kwa wakati na kuathiri utekelezaji wa majukumu ya kisheria na ya usimamizi ya Bunge, ikiwa ni pamoja na kushindwa kufanyika kwa vikao vilivyokuwa vimepangwa kuanza Januari hadi Juni 2025.

Pia, Spika wa EALA, Joseph Ntakarutimana, alieleza kuwa amefanya majadiliano na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC, Beatrice Asukul Moe, na Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva, ili kuhimiza nchi wanachama ambazo bado hazijalipa michango yao kulipa haraka ili kuwezesha Bunge kuendelea na shughuli zake.

EAC inategemea kwa kiasi kikubwa michango ya kila mwaka kutoka kwa nchi wanachama ili kugharamia shughuli zake.

Athari za ukosefu wa fedha

Ukosefu huu wa fedha umekuwa kikwazo kwa utekelezaji wa majukumu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, hususan katika kutekeleza mikakati ya kukuza biashara ya kikanda ambayo ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi katika ukanda huu.

Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2024/2025, bajeti ya EAC imekadiriwa kufikia dola za Marekani 112.98 milioni.

Kati ya kiasi hiki, dola 67.79 milioni, sawa na asilimia 61 zinatarajiwa kupatikana kupitia michango ya nchi wanachama pamoja na mapato ya ndani ya jumuiya, huku dola milioni 43.94 (asilimia 39) zikitegemewa kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Katika kutekeleza bajeti hiyo, kila nchi mwanachama ilitarajiwa kuchangia dola milioni 7 kwa mwaka.

Hata hivyo, hadi kufikia Aprili mwaka huu, ni nchi waanzilishi pekee wa Jumuiya, yaani Uganda (asilimia 102), Tanzania (asilimia 100), na Kenya (asilimia 100) ndizo zilizokamilisha michango yao kikamilifu.

Wengine waliochangia ni Rwanda (asilimia 75), Somalia (asilimia 50), Burundi (asilimia 19), DRC (asilimia 14) huku Sudani Kusini ikichangia asilimia saba pekee.

Hali hii imeiweka pabaya zaidi kiuchumi EAC kiasi cha kuibuka kwa wasiwasi wa kushindwa kujiendesha.

Kutokana na hali hiyo, Jumuiya imelazimika kukopa fedha kutoka ndani ya taasisi zake ili kufadhili shughuli muhimu za uendeshaji, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa mgogoro wa kifedha unaoweza kutishia uaminifu na uimara wa ajenda ya ushirikiano wa kikanda.

Hivi karibuni, katika hatua isiyo ya kawaida, Baraza la Mawaziri la EAC liliidhinisha mkopo wa dola 660,960 za Kimarekani kutoka kwa taasisi tano za jumuiya hiyo ili kugharamia maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, pamoja na kufidia matumizi ya nyongeza kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na gazeti dada la The Citizen, mkopo huo unalenga kufadhili vikao vya mtandaoni vya Bunge la EALA, vikiwemo vikao vya Kamati ya Masuala ya Jumla na kikao cha Bajeti.

Baraza limebaini hali mbaya ya kifedha ndani ya Jumuiya, inayosababishwa na kutowasilishwa au ucheleweshaji wa michango kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama, alinukuliwa Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Forodha, Biashara na Masuala ya Fedha, Annette Mutaave Ssemuwemba.

Kwa mujibu wa maelekezo yaliyotolewa, taasisi tano za EAC zikiwemo Sekretarieti ya EAC, Tume ya Utafiti wa Afya Afrika Mashariki, Tume ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki, na Mamlaka ya Ushindani ya EAC, zimetakiwa kutuma michango yao moja kwa moja kwenye akaunti ya benki ya Bunge la EALA ifikapo mwisho wa mwezi Mei 2025.

Aidha, Baraza limeagiza Katibu Mkuu kuhakikisha kuwa fedha zilizokopwa zinarejeshwa kupitia mgao wa baadaye wa michango ya nchi wanachama kwa Bunge la EALA kwa awamu mbalimbali.

Mkakati huu wa kifedha ni sehemu ya mfululizo wa hatua za dharura zinazochukuliwa kusaidia Jumuiya kuendelea kujiendesha licha ya uhaba mkubwa wa rasilimali za kifedha.

Akizungumzia hali ya uchumi wa EAC, Rais wa Mahakama ya Jumuiya hiyo, Jaji Nestor Kayobera, alisema kuwa upungufu wa bajeti umekwaza shughuli za mahakama na kuathiri utendaji wake kama taasisi inayosimamia utekelezaji wa sheria katika nchi wanachama, pamoja na kutoa mfumo wa kutatua migogoro ndani ya Jumuiya.

“Kwa sasa, tuna zaidi ya kesi 260 ambazo bado hazijasikilizwa, na tatizo kuu ni kwamba majaji hawapo kwa muda wote kwa sababu wanahudumu kwa mkataba wa muda mfupi, hivyo kesi zimerundikana hapa, na hili ni tatizo kubwa,” alisema Jaji Kayobera.

Majukumu mengine muhimu ya Mahakama ni kujenga imani, kuvutia uwekezaji, na kuimarisha ujumuishaji wa kikanda kwa kuendeleza utawala wa sheria.

Hata hivyo, upungufu huu wa rasilimali umesababisha shughuli hizi kupungua, na hivyo kudhoofisha hata uwekezaji katika ukanda.

Kwa upande wake Rebecca Kadaga, Naibu Waziri Mkuu wa Uganda na Waziri wa Masuala ya EAC, alisema, uhaba wa fedha umechelewesha baadhi ya vikao vya Bunge na kukosekana kwa jukwaa muhimu ya kujadili maendeleo ya jumuiya hasa biashara na vikwazo mbalimbali.

 “Kwa sasa ufadhili wa EAC ni tatizo kubwa kwa sababu nchi nne zinabeba mzigo wa nchi wanachama wote. Hali hii inaathiri kazi yetu na kila kitu kinapaswa kupunguzwa kutokana na ukosefu wa fedha mimi nadhani uongozi uone namna ya kubuni tena vyanzo vya mapato, lakini iundwe chombo cha kushurutisha hizi nchi kutekeleza ahadi zao” alisema.

Mtaalamu wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) James Manyika yeye anasema “Tatizo siyo ukosefu wa mawazo; ni ukosefu wa nia ya kisiasa. Hakuna nchi inayotaka kuonekana kama inabeba mzigo wa nyingine. Lakini hadi fikra hiyo ibadilike, EAC itaendelea kuchechemea”

Ili kulinda mustakabali wa jumuiya, wataalamu na viongozi wanaisihi nchi wanachama kulipa madeni yao haraka.

“Mzigo wa uhaba wa fedha hauziathiri tu shughuli za jumuiya, bali pia unadhoofisha imani na mshikamano ambao msingi wake ndiyo uliojenga EAC,” alisema mchambuzi wa siasa na mwanadiplomasia, John Silayo.

Silayo alisisitiza pia umuhimu wa kuwa na mfumo wa kifedha unaobadilika na unaozingatia uwezo tofauti wa kiuchumi wa kila mwanachama.

“Ingawa michango sawa inaonekana ya haki kwa maandishi, haizingatii uhalisia wa tofauti za kiuchumi. Mfumo unaopanda kulingana na uwezo wa kiuchumi unaweza kuipa EAC utulivu wa kifedha unaouhitaji kwa dharura,” alisema.

Kuhusu hali ya uchumi wa EAC Mbunge wa jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), James Ole Millya akizungumzia hali hiyo, amesema kuwa mwenendo mbaya unavyoelekea jumuiya hii inaweza kufa tena na itakuwa ngumu kuifufua upya.

“Unajua awali ilikufa kwa mambo ya kisiasa ambayo kikawaida diplomasia ndio dawa lakini ikiuliwa na uchumi itakuwa mbaya sana na hadi kuja kufidia na kusimama upya itachukua muda mrefu sana ukizingatia kila nchi inapambana kujijenga kiuchumi”

Amesema kuwa katika kunusuru hilo, nchi wanachama waendelee kuhimizwa uwajibikaji lakini pia mfumo wa michango hiyo iboreshwe upya.

“Kwa mfano tunaweza kusema asilimia 65 ya bajeti yetu itachangiwa kwa usawa na asilimia nyingine 35 ichangiwe kulingana na uwezo wa kifedha wa nchi husika maana sio ajabu tunalaumu kumbe baadhi ya nchi zinalemewa kifedha na bajeti zao” amesema.

Profesa Ali Makame Ussi, mtaalamu wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), yeye anasema “Wananchi wanapokosa kuona manufaa ya uunganishaji wa kikanda, na viongozi wanashindwa hata kuheshimu makubaliano ya bajeti, basi imani ya umma kwa EAC huporomoka na hilo ndilo hatari kubwa zaidi.”

Hata hivyo pamoja na changamoto hizo kwa mujibu wa taarifa za Ujumuishaji wa Kikanda Afrika (Africa Regional Integration Index – ARII), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inashikilia nafasi ya juu kama jumuiya iliyojumuika zaidi kiuchumi miongoni mwa Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda barani Afrika (RECs).

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inatarajiwa kupata ukuaji wa Pato Halisi la Taifa (GDP) kwa asilimia 5.8 mwaka 2025 Makadirio haya yametolewa na mabenki kuu ya nchi za ukanda huo, ambayo pia yameeleza matumaini chanya kuhusu hali ya uchumi wa jumla wa EAC.

Mwaka 2024, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilikuwa na Pato la Taifa (GDP) la Dola za Marekani bilioni 349.774 kutoka Dola za Marekani bilioni 296, sawa na ukuaji wa asilimia 5.4 .

EAC pia inatajwa kuwa miongoni mwa jumuiya zinazokua kwa kasi zaidi barani Afrika, kutokana na kuongezeka kwa biashara ya ndani ya ukanda na uwekezaji katika miundombinu.

Aidha mwaka 2025, jumla ya biashara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inakadiriwa kufikia thamani ya Dola za Marekani 27.98 bilioni, kutoka 26 iliyopo, huku mauzo ya nje yakitarajiwa kufikia dola bilioni 12.20, kwa mujibu wa TICGL. Hii inaashiria ukuaji thabiti wa biashara na ongezeko la uwezo wa kuuza bidhaa nje ya nchi ndani ya ukanda wa EAC.

Related Posts