Dar es Salaam. Serikali imesema miongoni mwa jitihada zinazofanyika kulinda haki na ustawi wa wafanyakazi nchini ni pamoja na kupitisha Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2008 Dira 2023 inayopanua huduma za hifadhi ya jamii hadi sekta isiyo rasmi na kwa watu wanaojiajiri.
Akizungumza jana kwenye mkutano wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete amesema Serikali imefanya marekebisho ya sheria za kazi, yakiwemo masharti mapya ya likizo kwa mama waliyojifungua watoto njiti na mashauriano kati ya waajiri na wafanyakazi wakati wa majanga.
Ridhiwani ametaja jitihada nyingine kuwa ni uzinduzi wa mpango mkakati wa mageuzi ya uchumi wa Kidijitali uliofanyika Julai 2024 kwa lengo la kukuza uchumi wa kidijitali wenye ustahimilivu na uhai huku taasisi zinazohusika na usalama na afya kazini zikiboresha mifumo ya mtandaoni ili kuhakikisha usalama na afya kwa wafanyakazi.

“Tanzania imeonyesha ukuaji wa uchumi wa kudumu, huku Pato la Taifa (GDP) likikua kwa wastani wa asilimia 5 kwa kipindi cha miaka minne iliyopita. Ukuaji huu umeiwezesha serikali kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1 kuanzia Julai 2025,” amesema Ridhiwani.
Alidokeza kuwa Baraza la Mishahara ya Kima cha Chini linakamilisha mapitio ya amri ya mwaka 2022 kuhusu kima cha chini cha mshahara, jambo litakaloimarisha uhusiano kati ya ajira, haki, na ukuaji.
Katika nyanja ya Teknolojia, Kikwete amesema Tanzania ilizindua Mpango Mkakati wa Mageuzi ya Uchumi wa Kidijitali mwezi Julai 2024, unaolenga kukuza uchumi wa kidijitali wenye ustahimilivu na uhai.
“Mpango huu unakusudia kuunda ajira, kulinda haki za binadamu, na kuongeza tija. Mfumo wa kusimamia mashauri ya migogoro ya kazi kwa njia ya mtandaoni umeundwa ili kulinda haki za wafanyakazi na waajiri,” amesema.

Kuhusu, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) nchini Tanzania, Kikwete aliieleza ILO kuwa mfuko huo unatoa fidia ya juu kwa wafanyakazi waliojeruhiwa kazini, inayozidi viwango vya ILO na kutoa mafao ya maisha kwa wategemezi wa wafanyakazi waliopoteza maisha.
“WCF pia umeanzisha mpango wa kina wa kuwahudumia wafanyakazi walioumia ili kuwawezesha kurejea katika jamii na kushiriki tena kwenye uchumi,” amesema.
“Dhamira ya Tanzania kushirikiana na ILO ni kukabiliana na changamoto za kazi zenye staha na kuboresha viwango vya maisha na mazingira ya ajira kwa wananchi wake. Alitoa shukrani kwa msaada endelevu wa ILO na kuitaka kuendeleza ushirikiano huo,” amesema.
Juni 15, 2011, aliyekuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete alihutubia mkutano huo wa ILO na kueleza mikakati ya Tanzania kukabiliana na athari za utandawazi ambapo alieleza kuwa ni pamoja na uwezeshaji wa jamii juu ya namna ya kuutumia utandawazi kama fursa ya uzalishaji na ajira.