Majaliwa aeleza sababu za kwenda Japan

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameeleza kilichompeleka Japan kuwa ni kueleza fursa zilizopo nchini na kuwashawishi  wawekezaji kuja kuwekeza.

Waziri Mkuu amesema soko la uwekezaji Tanzania ni kubwa na mazingira yake ni mazuri, kwani imezungukwa na nchi nane zinazotegemea soko hilo. Hivyo alikwenda nchini humo kuelezea fursa hizo na nafuu zilizopo kwenye sekta ya uwekezaji nchini.

Majaliwa amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi, Juni 5, 2025 wakati akijibu swali la mbunge wa Ushetu (CCM), Emmanuel Cherehani.

Katika swali lake kwa Waziri Mkuu, Cherehani ameuliza ni mkakati gani wa Serikali katika kufufua viwanda nchini ikiwemo kuvutia wawekezaji katika viwanda vya pamba, kahawa, korosho na mazao mengine.

Waziri Mkuu amesema Serikali imekuwa ikifanya mabadiliko yanayovutia wawekezaji ikiwemo kupunguza sharti la mtaji ambalo awali walitakiwa kuwa na mtaji usiopungua dola 100,000 hadi kufikia mtaji wa dola 50,000, kiwango ambacho kinawavutia wengi.

“Tumeendelea kurekebisha changamoto mbalimbali kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, ikiwemo kuwapunguza gharama na kupeleka miundombinu ya kutosha katika maeneo ya uwekezaji ikiwemo maji, umeme na barabara,” amesema Majaliwa.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Tanzania ikilinganishwa mataifa mengine ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) bado iko salama zaidi katika uwekezaji, hivyo Serikali imefungua milango kwani kila mwekezaji atanufaika na kile atakachokifanya.

Majaliwa alikwenda nchini Japan Mei 22, 2025 kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye maonyesho ya World Expo 2025 Osaka.

Aidha, akiwa Japan, Majaliwa alishiriki kongamano la biashara, uwekezaji na utalii ambalo lilihusisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na Japan.

Katika kongamano hilo, Majaliwa alisema Serikali itaendelea na mikakati ya kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wa mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Japan, ili kuwawezesha kunufaika na fursa zilizopo katika mataifa hayo.

Majaliwa alisema Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kushiriki katika makongamano mbalimbali ya kimataifa ambayo yamekuwa yakiwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji, ili kuongeza tija kwenye masuala ya biashara na uwekezaji.

Mei 26, 2025, Majaliwa alishuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano ya ujenzi wa kituo kikubwa cha kupandikiza figo pamoja na utoaji mafunzo kwa madaktari bingwa, ambacho kitakuwa ni kikubwa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kituo hicho ambacho kitajengwa kwenye Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma ni ushirikiano kati ya Shirika la Tiba la Tokushukai, Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo Kikuu cha Dodoma na kinatarajia kugharimu zaidi ya Sh28 bilioni ikiwa ni msaada usiokuwa na masharti yoyote.

Utiaji saini huo uliofanyika kwenye  kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii lililowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na wawekezaji wa Japan katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Westin, Osaka, Japan.

Mei 27, 2025 Majaliwa alikutana na Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafirishaji na Utalii wa Japan, Hiromasa Nakano kwenye makao mkuu ya wizara hiyo Tokyo Japan

Aidha, Majaliwa alifanya mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Wawekezaji katika Sekta ya Miundombinu la Japan (Jaida) Miyamoto Yoichi pamoja na ujumbe wake ambapo walijadiliana kuhusu masuala mbalimbali ya uwekezaji kwenye sekta za Ardhi, Miundombinu pamoja na Usafirishaji.

Mei 29, 2025, Majaliwa alikutana na Waziri Mkuu wa Japan, Ishiba  Shigeru ambaye alimuhakikishia nchi hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania jambo ambalo linalenga kuchochea ukuaji wa uchumi kutokana na fursa zitakazoendelea kupatikana kupitia mahusiano hayo.

Related Posts