Chalamila ataka taasisi za dini zikaguliwe mara kwa mara

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameitaka Serikali kuwa na utaratibu wa kuzifuatilia taasisi za dini ili zisitoe mahubiri yanayoweza kupotosha Taifa.

Amesema hiyo itasaidia kuziondolea usajili taasisi zenye mahubiri na mafunzo ambayo yanaweza kuwa sumu kwa Taifa.

Chalamila ameyasema hayo leo Juni 5,2025 wakati wa harambee ya ujenzi wa kituo cha watoto wenye uhitaji maalumu kilichopo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Kauli  ya Chalamila imekuja siku chache baada ya Serikali kulifutia usajili Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima kwa kile kilichoelezwa, mahubiri yake yana uelekeo wa kisiasa unaolenga kuichonganisha Serikali na wananchi, ikiwa ni siku moja tangu kiongozi huyo wa kiroho atangaze msimamo wake wa kuendelea kukemea vitendo vya utekaji na watu kupotea.

Kwa mujibu wa Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa ni kile kilichoelezwa kanisa hilo limekiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.

Chalamila akitolea mfano wa kanisa alilolitembelea hivi karibuni ambalo kiongozi wake alitoa mahubiri ya uongo.

“Nafikiri tuwe tunafanya vetting (uchunguzi) mara kwa mara kwenye hizi taasisi za dini ili kuhakikisha Taifa halipati sumu kupitia mahubiri yanayotolewa.”

Chalamila pia amezungumzia watu wanaopotosha umma na kumuhusisha Rais Samia Suluhu na familia yake na umiliki wa mali nyingi akieleza kuwa habari hizo ni za upotoshaji.

“Nikupe pole Rais kwa unachopitia, watu wachache wameamua kukusema wewe na familia yako kwamba mnajilimbikizia mali. Haya maneno wakati mwingine wanaoyasema hata hawaelewi.

“Siku moja nikiwa nafanya mazoezi nilikutana na mtu akaniambia kituo cha mafuta kilichopo katika eneo hilo ni cha mtoto wa Rais na akasisitiza huwa anakuja pale, bahati nzuri huyo mtoto wa Rais akapita nikamuuliza unamjua yule akasema hamjui nikamwambia huyo sasa ndio mtoto wa Rais.”

Chalamila amesema suala la kuhusisha familia ya  kiongozi aliyeko madarakani na ulimbikizaji mali i lilitokea pia kwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete lakini uvumi huo ulimalizika baada ya kutoka madarakani.

Related Posts