Monduli. Zaidi ya Sh17.7 bilioni zilizotolewa kwa ajili ya mradi wa skimu za umwagiliaji katika eneo la Mto wa Mbu, wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha zinatarajiwa kumaliza tatizo la mafuriko katika eneo hilo.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 5, 2025 na Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mto wa Mbu katika ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla aliyesimama eneo hilo kusalimia wananchi.

Amesema eneo la Mto wa Mbu lilikuwa likikabiliwa na mafuriko hali ambayo ilikuwa ikiathiri shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo na utalii na kuwa baada ya fedha hizo kutolewa, adha hiyo haitakuwepo.
“Mto wa Mbu ndiyo lango kuu la utalii Tanzania, bonde hili limeshika uchumi wa Wilaya ya Monduli ila adha ya mafuriko kwa miaka mingi sana imekuwa ikitusumbua,” amesema Mbunge Lowassa.
Hata hivyo, ameishukuru Serikali kwa kupeleka fedha hizo zaidi ya Sh17.7 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya umwagiliaji ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji kwa njia ya kilimo, shughuli za utalii na uvuvi.
Akisalimia wananchi wa eneo hilo, Makalla amesisitiza umuhimu wa amani huku akisifia ujuaji wa uchumi katika mikoa ya Kaskazini ambayo inazidi kukua kiuchumi kutokana na sekta ya utalii.
“Amani ni muhimu na ukiangalia mikoa ya Kaskazini inakua kiuchumi kutokana na utalii,lakini aliyeletwa katika mkoa huu(Makonda) mtu mwenye shughuli zake,amechagiza sana utalii na kuifanya Arusha ichangamke zaidi,” amesema.
Kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Makalla amesema Chama cha Mapinduzi kimejipanga kushiriki uchaguzi huo sambamba na kuendeleza miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini.
“Nimesimama hapa kwa heshima ya CCM kuwashukuru wana Monduli na Arusha kwa kukipa ushindi CCM na kuwakumbusha mwaka huu kuna uchaguzi mkuu, tutakuja kuomba kwenu ridhaa tena,” amesema Makalla.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema katika eneo la Engaruka wilayani humo, kunatekelezwa mradi wa uchimbaji magadi soda, mradi ambao utasaidia kukuza uchumi wa wilaya na mkoa kwa ujumla.
Amesema Serikali inaendelea kutoa fidia kwa wananchi na zaidi ya Sh14 bilioni zitatolewa katika mradi huo.
“Tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu nikumbushe kuhusu amani, ikipotea haya magari ya utalii yanayopita hapa hayatapita tena, amani ikitoweka hakuna taifa litakuja kwetu, tutunze amani kwa faida yetu sisi ambao hatuna hata pa kukimbilia,” amesema na kuongeza;
“Leo wana Arusha wanatarajia mawe mazito kutoka kwako sisi watumishi wa Serikali hatukuwa na shaka hata kidogo tulionaona wakipita, tukasema ngoja aje mwamba hapa. Monduli kazi iliyofanyika ni kubwa na tunatarajia kupitia mradi wa Engaruka uchumi wa mkoa utazidi kukua.”
Makalla akitokea wilayani Babati Mkoa wa Manyara, amepokelewa na viongozi wa CCM mkoa wa Arusha wakiongozwa na Mwenyekiti wa Arusha, Thomas Ole Sabaya na baadaye le atahutubia mkutano wa hadhara wilayani Karatu ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.