Ofisi ya Chadema Mara yageuzwa ya Chaumma, Mwalimu atoa maagizo

Mara. Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salumu Mwalimu ametoa maagizo kwa viongozi wa mikoa wa chama hicho hadi kufikia Julai 2025 mwishoni wawe wamepata wagombea wenye ushawishi watakaopeperusha bendera katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Amesema hicho ni kipimo chao na watakaoshindwa kuwapata wagombea watawekwa kando, kwa kile alichodai dhamira yao ni kwenda kushika dola, hivyo uongozi wa chama hicho hauwezi kuwavumilia wanaoshika nafasi kama kivuli.

Ametoa agizo hilo siku moja baada ya kusema kwamba wiki ijayo watafungua pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu za kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo wa Oktoba.

Akizungumza mkoani Mara leo Alhamisi, Juni 5, 2025 wakati anafungua ofisi mpya ya Chaumma mkoani hapo, Mwalimu amesema sharti la mgombea lazima awe kada anayekubalika na ushawishi na apatikane kwa kufanya utafiti.

“Hatutaki mtupatie mgombea ghalasa, natoa maelekezo nchi nzima kwa viongozi wote wa mikoa yote hadi kufikia Julai mwisho mwaka huu tuwe tumepata wagombea wa kupeperusha bendera kwenye uchaguzi mkuu kuanzia kwenye udiwani na ubunge atakayeshindwa atawekwa kando apishe wengine,” amesema Mwalimu.

Mwalimu amesema jukumu moja lililo mbele yao ni kukiandaa chama hicho kuingia kwenye uchaguzi mkuu, jambo hilo lisipotekelezeka hata yeye kwenye nafasi hiyo atakuwa hatoshi na atatakiwa kupisha wengine.

“Kabla sijaondolewa kwenye nafasi yangu nitahakikisha wale wote wa chini ambao hawakutekeleza wajibu wao wameondolewa, mwenyeviti wa mikoa lazima tunataka wagombea udiwani, waubunge  tukifika Dar es Salaam tutatoa waraka wa maelekezo,” amesema Mwalimu.

Amesema viongozi hao wa mikoa wanapaswa kuwasimamia viongozi wa wilaya kufanya shughuli hiyo katika maeneo yao kukiandaa chama kushiriki uchaguzi mkuu.

Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chaumma-Bara, Devotha Minja amesema atasimamia kila mkoa upate ofisi nzuri kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu.

“Chama ili kiwe endelevu na kufika kwa watu lazima kiwe na ofisi na wale wote wenye shida iwe sehemu ya kimbilio lao, Nitasimamia kabla ya uchaguzi mkuu kila mkoa lazima uwe na ofisi,” amesema Minja.

Amesema mchakato huo unaenda sambamba na kutafuta ofisi ya makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam kwani wanahitaji ofisi kubwa inayoweza kutosheleza watendaji wote.

Ofisi ya mpya ya Chaumma katika mkoa huo ipo katika mtaa wa Makongoro Mjini Musoma ambayo awali ilikuwa inatumiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Akizungumza aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Gimbi Doto amesema wamebadilisha ofisi hiyo baada ya viongozi waliokuwa wanasimamia na kulipia pango kuhamia Chaumma.

“Hii ni ofisi yetu mpya, ingawa mwanzoni ilikuwa inatumiwa katika shughuli za Chadema, waliokuwa wanalipia wamehamia Chaumma tumeamua kubadilisha na ni ofisi yetu ya mkoa ya Chaumma,” amesema Gimbi ambaye kwa sasa ni kada wa Chaumma.

Mwenyekiti wa chama hicho, Hashimu Rungwe amesema Chaumma tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013 wamekijenga kwa shida na raha hadi wamefika hapo lakini anashukuru kupata ongezeko la wapambanaji.

“Siri ya chama kukua ni kutokulala tunatakiwa kupambana kuwapigania wananchi kwa kuja na sera nzuri mbadala, ili raia watuelewe,” amesema Rungwe.

Amesema ili kuendeleza uhai wa chama hicho ni lazima kijikite kuangalia masilahi ya wananchi na kushikamana na kuacha kubaguana.

Chama hicho hicho kipo kwenye mikutano ya opresheni yake ya C4C iliyozinduliwa Juni 3, 2025 jijini Mwanza inatarajiwa kufika mikoa yote Tanzania.

Katika awamu ya kwanza ya ziara hiyo inayolenga kutambulisha uongozi mpya ngazi ya Taifa, kukiandaa chama kushiriki uchaguzi mkuu, kupokea wanachama wapya na kuziba ombwe la viongozi kwa maeneo ambayo hayana viongozi.

Operesheni hiyo kwa awamu ya kwanza itazunguka kwa siku 12 kisha watapumzika kabla ya kuendelea kwenye mikoa itakayokuwa imesalia.

Related Posts