Kukosekana mifumo ya umwagiliaji eneo kubwa la kilimo laachwa wazi

Unguja. Licha ya kilimo cha mpunga kuwa tegemezi kisiwani hapa, kukosekana kwa miundombinu ya umwagiliaji na kuendelea kutegemea msimu wa mvua umeendelea kuwa mwiba kwa wakulima na kuchangia kudorora kwa kilimo hicho.

Akizungumza leo katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi, wakati akijibu hoja za wajumbe wa baraza hilo leo Juni 5, 2025 Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis amekiri kwamba bado hakujawa na mifumo imara licha ya jitihada zinazochukuliwa na Serikali kuimarisha kilimo hicho.

Amesema Serikali imefanikiwa kuendeleza hekta 2,300 pekee kati ya hekta 8,200 sawa na silimia 26 tu hivyo hekta 5,900 bado zinahitaji uendelezwaji katika kilimo cha umwagiliaji.

Waziri alikuwa akijibu swali la mwakilishi wa Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe ambaye alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kukiimarisha kilimo cha mpunga nchini.

“Kilimo cha mpunga kinategemewa sana na wakulima wengi hapa kwetu Zanzibar, Serikali inalitambua suala hili kikamilifu, lakini bado wakulima walio wengi wanatumia kilimo cha kutegemea mvua kutokana na kuwa bado yapo maeneo mengi hayajaendelezwa kwa ajili ya huduma hii muhimu ya umwagiliaji,” amesema.

Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea na jitihada zake za kuongeza ukubwa wa maeneo na mifumo ya kilimo cha umwagiliaji ili kuwasaidia wakulima wengi zaidi na kupunguza utegemezi wa kilimo cha kutegemea mvua.

Kwa mujibu wa waziri huyo, ukubwa wa eneo la umwagiliaji kwa mwaka 2019 lilikuwa ni hekta 875 sawa na ekari 2,187.5 tu, lakini hadi kufikia Aprili 2025 tayari eneo hilo limefikia hekta 2,300 sawa na ekari 5,750.

Amesema kilimo cha umwagiliaji kimeongeza tija ya uzalishaji wa mpunga kutoka tani 1.5 kwa hekta kwa mwaka hadi wastani wa tani 11 kwa hekta kwa mwaka.

Pamoja na kuongeza tija umwagiliaji pia ni kisaidizi kizuri katika kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinasababisha kuongezeka kwa vipindi vya jua na mvua zisizo za uhakika, hivyo kuathiri uzalishaji.

Wakati huohuo wizara inafanya juhudi kuhakikisha wakulima wanalima kilimo cha kisasa na kutumia mbegu bora.

Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar (Zari) inaendelea na tafiti za uzalishaji wa mbegu bora na hivi karibuni imekamilisha tafiti zilizoibua aina tatu za mbegu mpya za mpunga, aina nne za mbegu mpya za muhogo na aina tatu za mbegu za viazi lishe.

Mbegu hizo kwa sasa zipo katika hatua ya kuzalishwa ili ziwe nyingi na zipelekwe kwa wakulima.

“Aidha, Zari kwa kushirikiana na taasisi ya World Vegetable Centre wamegawa vifurushi vya mbegu bora za mbogamboga kama vile mchicha lishe, nyanya chungu na mnavu kwa wakulima zaidi ya 2,000 ili kuendeleza uzalishaji wa mboga na upatikanaji wa lishe bora nchini,” amesema.

Waziri alikuwa akijibu swali la mwakilishi wa Chambani, Bahati Khamis Kombo ambaye alitaka kujua mipango ya Serikali kuwapatia wakulima hao mbegu bora kwani wanalima kilimo cha kisasa lakini mbegu wanazotumia hazileti tija.

Related Posts