Wanafunzi 867 wanakaa chini shule ya Mtambani Dar

Dar es Salaam. Kukosekana kwa madawati ya kutosha Shule ya Msingi Mtambani iliyopo Bunju – Kinondoni jijini Dar es Salaam kumesababisha baadhi ya wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa sakafuni, jambo linalowakosesha utulivu.

Kukosekana kwa madawati ya kutosha Shule ya Msingi Mtambani jijini Dar es Salaam imefanya baadhi ya wanafunzi kusoma wakiwa wamekaa sakafuni jambo linalowakosesha utulivu.

Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2002, hadi sasa ina wanafunzi 2,606 huku ikiwa na madawati 580 kati ya 865 yanayohitajika.

Idadi hii inaleta upungufu wa asilimia 33 wa madawati endapo wanafunzi watatu watachangia dawati moja na hiyo kufanya wanafunzi 867 kukaa chini.

Madawati mapya yaliyotolewa msaada kwa Shule ya Msingi Mtambani iliyopo Bunju – Kinondoni jijini Dar es Salaam

Hayo yamesemwa leo Juni 5, 2025 na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Venance Mwasamakwela, wakati akikabidhiwa madawati 65 kutoka kampuni ya ulinzi ya Gardaworld.

Amesema kwa muda mrefu wanafunzi wamekuwa wakikaa chini au kushirikiana madawati kutokana na uhaba mkubwa wa samani hizo.

“Tunashukuru sana wahisani wetu sisi kama shule ya msimgi Mtambani kwa kuzawadiwa madawati 65 kutoka Gadaworld ambapo itapelekea kupunguza msongamano darasani kwenye ukaaji kwani wanafunzi 195 watakuwa wamepata pakukaa,” amesema Mwasamakwela.

Mwasamakwela amesema msaada huo utakwenda kuongeza ari ya kujifunza kwa wanafunzi, huku akiahidi kuyalinda madawati hayo ili yatumike kwa muda mrefu.

“Sasa tuna upungufu wa madawati 224.”

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Kinondoni, Chitegese Dominic Ngaluku amekiri kupokea madawati hayo na kueleza kuwa manispaa ya Kinondoni bado ina uhitaji wa madawati, huku akiwataka wadau kujitokeza kusaidia Serikali katika kuchangia sekta ya elimu.

“Ni jambo jema lililofanywa na wahisani wetu kwani tunapenda kuona kila mtoto anasoma katika mazingira rafiki na yenye staha. Hili ni jukumu letu sote kama jamii na sio kuiachia Serikali pekee,” amesema Chitegese.

Mbali na hayo Chitegese amesema wilaya ya Kinondoni ina upungufu wa madawati lakini Serikali kupitia bajeti zake inajitahidi kupunguza uhaba huo.

Mkurugenzi wa kampuni ya Gardaworld, Goodluck Lukumani amesema samani za darasani zina mchango mkubwa kwa mwanafunzi kumsaidia katika masomo yake.

Related Posts