Karatu. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema matokeo ya tume mbili zilizoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuchunguza na kutoa mapendekezo kwenye masuala yanayolalamikiwa wilayani Ngorongoro, yatafanyiwa kazi na kumaliza masuala hayo.
Tume hizo mbili ziliundwa ambapo ya kwanza itachunguza na kutoa mapendekezo ya masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa Ngorongoro, huku ya pili ikiangalia utekelezaji wa shughuli nzima ya uhamaji kwa hiari kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Desemba Mosi, 2024, Rais Samia akiwa Ikulu ndogo Arusha alizungumza na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa kimila wa jamii ya kimasai (Malaigwanan) waishio Ngorongoro na maeneo ya jirani.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Juni 5, 2025 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mazingira Bora Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
“Hatua ya kwanza Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa, kwa haraka alisikiliza changamoto za Ngorongoro aliunda Tume mbili, zinafanya kazi na baada ya hapo tutapata matokeo yake. Wapo wafitini na wanawahadaa wafugaji kuwa Samia hawapendi wafugaji ila si kweli, Rais anawapenda watu wote na masuala hayo ya Ngorongoro baada ya Tume hizi kufanya kazi yake, mapendekezo yatafanyiwa kazi,” amesema.
Awali, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga, uamuzi huo wa Rais Samia kuunda tume hizo mbili, ulifanyika kwa lengo la kuwasikiliza viongozi hao kufuatia kuwepo malalamiko dhidi ya baadhi ya maamuzi ya Serikali yanayohusu eneo la Ngorongoro.
Akizungumza leo katika mkutano huo wa hadhara, Makalla amesema hali ya maisha ya wananchi wa Wilaya ya Karatu imebadilika na wameendelea kunufaika na matunda yatokanayo ya sekta ya utalii.
Amesema wananchi wa jimbo hilo waliteseka kwa kipindi cha miaka 25 ila kipindi cha miaka mitano kuanzia 2020 hadi 2025 jimbo hilo limekuwa na mafanikio ikiwemo sekta ya maji, afya, elimu na barabara.
CCM ilishinda jimbo la Karatu mwaka 2020 baada ya kuongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa miaka 25 tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1995.
Makalla ametolea mfano akiwa Naibu Waziri wa Maji, alitembelea wilaya hiyo ambapo kulikuwa na kiongozi mmoja (bila kumtaja) ambaye hakutaka kuwe na mamlaka ya maji ambayo Serikali ina mkono wake.
“Kwa sasa Karatu ni ngome ya CCM, Karatu mliteseka na maendeleo yalisimama kwa miaka 25 lakini katika miaka mitano hii mmeona kasi ya maendeleo, atakayekuja kuwadanganya kwamba miaka mitano Karatu bado iko nyuma mpelekeni hospitali ya vichaa Dodoma,”
Amesema kwa sasa wilayani humo kupitia mamlaka ya maji upatikanaji wake Karatu mjini ni asilimia 79.
Mchungaji Peter Msigwa amesema hana ugomvi na vyama vya siasa vya upinzani ila vinahitaji muda wakajipange ili viweze kuleta ushindani wa kweli.
“Baada ya kusepa nimekuja hapa hamna sababu ya kuendelea kuteseka tujiunge na jeshi hili( CCM), ili tuendelee kuijenga Tanzania. Sina ugomvi na vyama vya siasa vya upinzani lakini vinahitaji muda vikajipange ili vilete ushindani wa kweli ule ubabaishaji tuukatae,”amesema Msigwa.
“Na mimi nimekuja kuwakatisha tamaa waliobaki njooni CCM tujenge nchi yetu, CCM ndio chama pekee chenye watu wenye weledi, kina rasilimali watu, sera zinazoeleweka, rasilimali fedha na ujuzi,”amesema.
“Arusha ni miongoni mwa mikoa mitano inayochangia pato la Taifa, hapa Karatu utalii ndiyo chanzo kikuu cha mapato, siasa ni uchumi huwezi kupinga kila kitu. Kupinga siyo sera na chama cha siasa ili kijulikane lazima kieleze kinaamini nini na wanataka kufanya nini,”amesema.