Raha, karaha ujenzi njia nne barabara ya Mbeya

Mbeya. Wakati Serikali ikiendelea kutekeleza  ujenzi wa barabara ya njia nne maeneo ya jiji la Mbeya, wananchi wameomba viwekwe vivuko vya muda ili kunusuru maisha yao.

Wamesema kando ya barabara hizo zinazojengwa, eneo kubwa limerundikwa vifusi huku baadhi ya maeneo yakichimbwa mashimo na kuachwa wazi, jambo ambalo ni hatari kwa waenda kwa miguu.

Lakini pia ni karaha kwa walio wekeza kwenye biashara ya maduka ya bidhaa za nyumbani na vifaa vya ujenzi.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Juni 5, 2025, baadhi ya wananchi wamesema licha ya ujenzi huo kuwa chachu ya maendeleo, wanaomba kero ndogo zifanyiwe kazi.

“Tunatambua barabara njia nne inakwenda kuleta suluhisho la kupunguza foleni ya magari katika barabara Kuu ya Tanzania na nchi jirani ya Zambia (Tanzam), lakini namna ilivyo tunahofia usalama wetu hususan nyakati za usiku,” amesema Daima Hussein mkazi wa Mbeya mjini.

Hussein amesema ipo haja ya wasimamizi wa mradi huo kutupia jicho kundi kubwa la jamii hususan watoto wakati mradi ukiendelea kutekelezwa.

Ameshauri maeneo yote hatarishi ni vema yakafungiwa utepe kuonyesha kuwa eneo hilo ni hatari kwa waenda kwa miguu, ili  wachukue tahadhari.

Naye mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi, Janeth Samson amesema mbele ya duka lake kimemwagwa kifusi kwa ajili ya ujenzi hali inayozuia wateja kuingia.

 “Hapa ninapofanyia biashara kuna kifusi kimekaa kwa muda mrefu, wateja hawawezi kuja, tusaidiane katika hili,” amesema Samson.

Akizungumzia kadhia hiyo, dereva bajaji, Boniface Mwainyekule amesema wanapokea mradi kwa mikono miwili ,lakini ujenzi wake umegeuka kero kwao.

“Yaani ujenzi wa barabara hii badala ya kuleta kicheko imekuwa kero, unaweza kutoka Kabwe saa 10 jioni mpaka ufike kituo cha mabasi  Nanenane utatumia zaidi ya saa tatu kutokana na  foleni na hakuna njia za pembeni na barabara ni finyu,” amelalamika dereva huyo.

Akitoa ufafanuzi wa changamoto hizo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mkoa wa  Mbeya, Mhandisi Matari Masige amekiri kuwapo kwa kero hizo.

Hata hivyo amesema tayari wameliona na wanalifanyia kazi, muda si mrefu adha hiyo itaisha.

“Mradi huu ulipaswa ukamilike Aprili, 2025 lakini kutokana na sababu mbalimbali Serikali imemuongezea muda wa miezi sita mkandarasi wa kampuni ya Chico anayeutekeleza,” amesema.

“Hivi karibuni waziri mwenye dhamana alitembelea kukagua mradi wa barabara njia nne na kutoa maelekezo ya kuhakikisha kasi inaongezwa,” amesema Masige.

Related Posts