Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imeukataa Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania kutumika katika kesi ya mgogoro wa ardhi inayolikabili kanisa hilo.
Upande wa utetezi katika kesi hiyo, kupitia shahidi wake wa pili, Katibu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Mchungaji George Lawi, uliiomba Mahakama ipokee Katiba ya Kanisa hilo ya mwaka 1970 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004.
Katiba hiyo ilikusudiwa kuwa sehemu ya ushahidi wake katika kuunga mkono ushahidi wake wa maandishi aliokwisha uwasilisha mahakamani kwa maandishi pamoja na ufafanuzi alioutoa kwa mdomo.
Hata hivyo Katiba hiyo ilipingwa na mawakili wa madai katika kesi hiyo, Deogratius Butawantemi na Gwamaka Sekela, kutokana na ukiukwaji wa taratibu za kisheria.
Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Arafa Msafiri anayesikiliza kesi hiyo, ameikataa Katiba hiyo baada ya kukubaliana na hoja za pingamizi la mawakili hao.
Kesi hiyo inatokana na mgogoro wa zawadi aliyopewa Askofu wa kwanza wa kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam, ambaye pia ndiye Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa Anglikana Tanzania, hayati John Sepeku.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi hiyo zilizoko mahakamani Sinodi ya Dayosisi hiyo katika kikao chache cha Machi 8 na 9, 1980 iliridhia na kumpatia Askofu Sepeku zawadi ya shamba lililoko Buza Wilayani Temeke, na nyumba eneo la Kichwere, Buguruni, wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Hivyo alipewa shamba la eka 20 mwaka 2010 shamba hilo ambalo kwa sasa linadaiwa kuwa na thamani ya Sh3.7 bilioni lakini baadaye uongozi wa sasa wa Dayosisi hiyo uliligawa kwa mwekezaji, kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Familia ya Askofu Sepeku ilibaini hilo baada ya mwekezaji huyo kuvamia na kufyeka mazao mbalimbali waliyokuwa wameyalima, mwaka 2023, kisha akajenga kiwanda na nyumba yenye thamani ya Sh165 milioni.
Hivyo mtoto wa Askofu Sepeke, Bernado Sepeku alifungua kesi dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes na mwekezaji huyo, Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Katika kesi hiyo Bernado ambaye ni msimamizi wa mirathi ya baba yao anapinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yao.
Anaiomba Mahakama iamuru alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.
Pia anaiomba alipwe Sh493.65 milioni kama fidia ya hasara ya mazao yaliyoharibiwa katika shamba hilo.
Kesi hiyo iko hatua ya utetezi ambapo wadaiwa wameanza kutoa utetezi wao jana Jumatano, Juni 4, 2025.
Shahidi huyo wa Pili wa utetezi akiongozwa na Wakili wa madai, Denis Malamba ameiomba Mahakama ipokea Katiba hiyo ya mwaka 1970 yenye marekebisho ya mwaka 2004, iwe sehemu ya ushahidi wake, ambapo ilipingwa kwani imekiuka uwasilishaji wa kisheria haikuwepo katika orodha ya vielelezo vya upande wa utetezi vilivyotarajiwa kuwasilishwa mahakamani, tangu mwanzo.
“Hivyo haiwezi kupokewa na Mahakama katika hatua hii kwa kuwa ni nyaraka mpya, kwa hivyo inakataliwa,” amesema Jaji Arafa.
Katika maelezo yake ya ushahidi shahidi huyo amedai kuwa ofisini kwake hakuna kumbukumbu zinazoonesha kuwepo kwa kikao kilichopendekeza Askofu Sepeku kupewa zawadi hizo.
Pia amedai kuwa vikao vya mamlaka zinazodaiwa kupendekeza na kumpa Askofu Sepeku zawadi ya ardhi inayobishaniwa yaani Kamati ya Kudumu na Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, hazina mamlaka ya kugawa mali ya kanisa.
Badala yake amedai kuwa hajawahi kuona kumbukumbu za kikao cha Wadhamini kilichopendekeza na kupitisha uamuzi wa kumpa zawadi hiyo Askofu Sepeku.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mashahidi wa upande wa madai wakiwemo maaskofu, mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa hilo na Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo mstaafu, Dk Valentino Mokiwa walikiri kutambua uamuzi huo.
Pamoja na kutambua kuona na kushiriki vikao vilivyoridhia na kupitisha pendekezo hilo la kumpa zawadi Askofu Sepeku, walisema kuwa Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam ina mamlaka ya kufanya hivyo.
Maaskofu hao walifafanua kuwa Sinodi ni Mkutano Mtakatifu wa Juu unaowahusisha Askofu wa Dayosisi, mapadri na waumini kwa ajili ya kufanya uamuzi wa kanisa na kwamba uamuzi wake hauwezi kupinga popote wala kutenguliwa na mtu yeyote.
Awali, shahidi wa kwanza wa utetezi, Ofisa Ardhi, wa Dayosisi ya Dar es Salaam, James Mtamakaya alitoa ufafanuzi wa maelezo ya ushahidi wake wa maandishi aliouwasilisha mahakamani hapo.
Katika maelezo yake pamoja na mengine amedai kuwa hajawahi kuona kumbukumbu kuwa wadhamini wamewahi kutakiwa au kuridhia uhamisho wa kipande cha ardhi kwa mtu yeyote.
Akihojiwa na Wakili Butawantemi shahidi huyo mara amedai mmiliki wa mali zinazobishaniwa ni kanisa na wakati mwingine akasema ni Bodi ya Wadhamini.
Wakili Butawantemi: Shahidi kikao Kikuu kwa Waanglikana kinaitwaje?
Wakili: Lini ulifahamu kuwa Kanisa la Anglikana linamiliki ardhi?
Wakili: Lini ulitambua kuwa Bodi ya Wadhamini inamiliki ardhi?
Shahidi: Baada ya kufika kanisani
Wakili: Sasa Mahakama ichukue lipi?
Shahidi; Mmiliki ni Bodi.
Wakili: Unafahamu kuwa Sinodi ya mwaka 1980 ilitoa ardhi kwa Askofu John Sepeku?
Wakili: Unaamini maamuzi yanayotolewa na Sinodi?
Shahidi: Sina cha kusema kwa sababu sijawahi kuwepo katika mkutano sisi tunapata taarifa kupitia kwa wajumbe.
Kesi hiyo itaendelea Juni 26, 2025.
