PPRA wataja siri ya mafanikio ya utunzaji mazingira

Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wametaja siri ya kupatiwa tuzo katika kilele cha siku ya Mazingira, wakigusia Mfumo wa Ununuzi wa Kidigitali (NeST), kwamba umekuwa mkombozi na unaendelea kuwabeba.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa PPRA, Mkurugenzi wa Tehama, Michael Mushilo amesema mfumo wa NeST umeonyesha mafanikio, siyo kwa ajili ya kuweka uwazi katika suala la ununuzi pekee, bali kwenye utunzaji wa mazingira kwa ujumla.

Jana, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliwakabidhi tuzo PPRA, akisema mchango wao umeonekana kwa vitendo katika kudhibiti na kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na karatasi huku akiwasifu kwa kupunguza gharama.

NeST inatoa fursa kwa wazabuni wadogo na wakubwa, makundi maalumu ikiwemo wanawake, vijana na kuongeza fursa za kiuchumi.

Mushilo amesema mfumo huo umejengwa na Watanzania wenyewe lakini umekuwa na mafanikio ndani na nje ya nchi kwa kuwa umekuwa sehemu salama na unatunza mazingira.

“Wengi hawajui tunaposema mfumo unatunza mazingia, zamani watu walikuwa wanachukua makaratasi mengi kuandika wanapohitaji kuomba tenda za Serikali lakini kwa sasa hilo halipo, walikuwa wanasafirisha makaratasi hayo kwenda mbali kuwahi muda wa mwisho lakini sasa haipo, kwa hiyo tumebana matumizi ya gharama za usafiri na hakuna makaratasi yanayoonyesha kuzagaa tena,” amesema Mushilo.

Amesema kwa sasa taasisi zote za umma zimeanza kuutumia mfumo huo na hivyo kupunguza kabisa matumizi ya makaratasi wala kuondoa kisingizio cha kwamba wamechelewa kwa sababu furani kwa kuwa mtu akiingia kwenmye mfumo unamwonyesha siku na muda aliotuma.

Mbali na hilo amesema wameongeza uwazi katika ununuzi wa umma na kupunguza muda kwenye shughuli nyingine za maendeleo ambao awali ulikuwa unatumika.

Machi 7, 2025, Mkurugenzi wa PPRA, Denis Simba alifungua mafunzo kwa maofisa ununuzi 184 yaliyolenga kuwajengea uwezo aliwagiza kuhakikisha manunuzi ya umma yote yafanyike kwa mfumo wa kidigitali (NeST) ili kuondoa mapungufu yanayojitokeza.