Alivyoepa kifungo miaka 20 jela kwa kupatikana na nyara ya Serikali

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Sumbawanga, imefuta hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela aliyohukumiwa Juma Mlambege baada ya kutiwa hatiani kwa kupaikana na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh239 milioni.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya kubaini kesi dhidi yake haikuthibitishwa pasipo kuacha shaka.

Awali, Mlambege alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda kwa kosa la kumiliki nyara ya Serikali kinyume cha kifungu cha 86(1) na (2) (c) (iii) cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori na Jedwali la kwanza la vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Udhibiti wa Uhalifu wa Kiuchumi na Kupangwa.

Hukumu iliyomwachia huru Mlambege ilitolewa Juni 5, 2025 na Jaji Thadeo Mwenempazi aliyesikiliza rufaa ya jinai namba 4215/2024. Nakala ya hukumu imewekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Upande wa mashtaka ulidai  Juni 16, 2023 katika eneo la Nsemulwa wilayani Mpanda mkoani Katavi, mrufani alikutwa na nyara ya Serikali bila kibali chochote kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Alipofikishwa mahakamani hapo alitiwa hatiani kama alivyoshtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 jela.

Katika rufaa alikuwa na sababu tatu alidai mahakama ilikosea kupokea vielelezo, hati ya ukamataji (kielelezo cha kwanza) na vitu vilivyokamatwa bila kutolewa risiti ya kukiri kukamatwa.

Sababu nyingine ni mahakama ilikosea kisheria kwa kuamua kesi bila kuzingatia utetezi wake na mahakama ilikosea kumtia hatiani kwa kosa ambalo upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka.

Aliomba rufaa ikubaliwe kutokana na sababu hizo na aachiwe huru. Hakuwa na uwakilishi wa wakili, huku mjibu rufaa akiwakilishwa na wakili Flavia Shiyo.

Wakili Shiyo alipinga sababu hizo akieleza kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa kwani kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuonyesha alikutwa na nyara ya Serikali.

Kuhusu hoja ya kwanza ya rufaa, alieleza wakati wa upekuzi ulifanyika ukikidhi masharti yote yanayohitajika na kuwa amri ya upekuzi ilitolewa na askari polisi wa Kituo cha Polisi Mpanda ambao walikuta nyara hizo kwenye mfuko wa salfeti.

Alieleza baada ya nyara hizo kukamatwa hati ya ukamataji iliandaliwa na mrufani alisaini na shahidi wa kujitegemea alisaini pamoja na mashahidi wengine, akisisitiza kuwa cheti cha kukamata kilikidhi masharti yote ya chini chini ya kifungu cha 38 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Alisema iwapo risiti ilitolewa au la, haiwezi kubatilisha ukweli kwamba mrufani alikutwa na nyara ya Serikali.

Kuhusu hoja ya kosa kutothibitishwa, alieleza sababu hiyo haina mashiko kwa sababu vipande 10 vya meno ya tembo vilikamatwa kutoka kwa mrufani na alisaini hati ya ukamataji.

Aliiomba Mahakama itupilie mbali rufaa hiyo kwa kuwa hakuna sababu za msingi za kutengua uamuzi wa mahakama iliyotoa hukumu hiyo.

Jaji Mwenempazi amesema baada ya kusikiliza mawasilisho yaliyotolewa na pande zote mbili na kuchunguza kwa kina rekodi za rufaa, hoja ni iwapo kesi dhidi ya mrufani ilithibitishwa bila kuacha shaka yoyote.

Amesema kimsingi jukumu la mahakama hiyo ni kutathmini upya ushahidi wote ulitolewa katika mahakama ya chini, akinukuu mashauri mbalimbali ikiwamo rufaa ya jinai namba 214/2006 kati ya Kasema Shindano dhidi ya Jamhuri na Salim Petro dhidi ya Jamhuri katika rufaa ya jinai namba 85/2004.

Amesema rekodi iliyoko mbele yake inaonyesha mrufani alikamatwa akiwa na meno 10 ya tembo kinyume cha sheria, tukio lililoshuhudiwa na shahidi wa kwanza hadi wa tatu wa upande wa mashtaka.

Amesema upande wa mashtaka ulitoa hati ya ukamataji inayopingwa na mrufani aliyesisitiza kuwa saini iliyokutwa ndani yake si yake, mahakama ya mwanzo ilitupilia mbali pingamizi lake.

Jaji Mwenempazi amesema katika utetezi wake, mrufani alisisitiza alikamatwa akiwa matembezini na kwamba akiwa kituo cha polisi alilazimishwa kusaini karatasi lakini hakuhojiwa.

Hata hivyo, alisisitiza wakati wa usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo, mrufani alikana saini zilizokutwa katika hati hizo mbili ambazo zilitofautiana.

“Ukiangalia kumbukumbu hizo, mwenendo ulioandikwa na mahakama ya mwanzo, hasa ambapo mrufani ametia saini na kulinganisha saini yake zinazopatikana kwenye kielelezo cha kwanza na cha pili, bila kuhitaji maoni ya mtaalamu, sahihi hizo tatu ni za watu tofauti kabisa,” amesema.

Jaji amesema mahakama ya awali iliyosikiliza kesi hiyo haikushughulikia tofauti hizo.

Amesema mbali na vielelezo hivyo viwili hakukuwa na ushahidi mwingine dhidi ya mrufani, hivyo haikuwa sahihi kwa mahakama ya chini kumtia hatiani na kumhukumu mrufani bila kushughulikia tofauti za saini katika vielelezo hivyo.

Jaji Mwenempazi amesema kutokana na dosari hizo anafuta vielelezo hivyo kwenye rekodi ya kesi na kwa kukosekana ushahidi mwingine wowote ambao ungethibitisha hatia ya mrufani ni wazi kesi hiyo haikuthibitishwa bila kuacha shaka.

“Kwa hiyo naruhusu rufaa hii na hukumu iliyotolewa dhidi ya mrufani inafutwa. Ninaamuru mrufani aachiwe mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali,” amehitimisha hukumu jaji.

Related Posts