Sakata la Lema, Uhamiaji lawaibua wanasheria, wanasiasa

Moshi. Hatua ya Idara ya Uhamiaji kumzuia Godbless Lema kusafiri kwenda nje ya nchi, imewaibua wanasheria wakitaka vyombo vya dola kufanya kazi kwa mujibu wa Katiba na sheria, bila kuacha maswali yasiyo na majibu wala kuchafua taswira ya nchi kitaifa na kimataifa.

Uhamiaji juzi ilimzuia Lema, kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, katika mpaka wa Namanga akiwa katika mchakato wa kuvuka kwenda Nairobi nchini Kenya, hatua aliyodai inawalenga viongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani.

Katika taarifa kwa umma, idara hiyo ilieleza kuwa zuio hilo haliwalengi viongozi wa Chadema nali ni ya kawaida katika utekelezaji wa majukumu, kauli ambayo imepingwa na makada wa chama hicho wakisema Lema ni kiongozi wa tatu kuzuiwa kwa nyati tofauti, bila sababu za msingi.

Wakili Peter Madeleka amesema Ibara ya 17 ya Katiba ya Tanzania inatoa haki na uhuru wa raia wa Tanzania kwenda popote duniani bila kuvunja sheria, akitaka Idara ya Uhamiaji ieleze ni sheria gani ambayo Lema ameivunja.

Kwa upande wake, Wakili Dk Rwezaula Kaijage amevitaka vyombo vya dola kuacha kukamata watu kwa hisia, bali vifanye uchunguzi na kukamata mtu kama ametenda kosa.

Liberatus Mwang’ombe, mwanasiasa na diaspora anayeishi Marekani, kupitia ukurasa wake wa X amesema huo ni mwendelezo wa hatua za kuwalenga viongozi wa Chadema, akiwataja wengine waliozuiwa kuwa ni Amani Golugwa, kaimu naibu katibu mkuu aliyezuiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jullius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Golugwa alikuwa akisafiri kwenda Ubelgiji kushiriki mikutano ya International Democracy Union (IDU) na alikamatwa usiku wa kuamkia Mei 13, 2025.

Kwa mujibu wa Mwang’ombe, Mei 15, 2025 Uhamiaji katika Uwanja wa JNIA pia ilimzuia kwa saa 10, kijana wa IT wa Chadema, Remsi Kassanda ili asitoke nchini kwenda Uganda kwa shughuli za kikazi.

Lema alitoa taarifa ya kuzuiwa kwake Juni 6, 2025 saa 7:06 kupitia ukurasa wake wa X akisema amezuiwa ofisi za Uhamiaji katika mpaka wa Namanga.

“Wakati nafanya process (taratibu) za uhamiaji, nimeambiwa na Idara ya Uhamiaji kuwa kuna zuio kwa viongozi wa Chadema kusafiri kutoka nje ya Tanzania. Niko ofisi za Uhamiaji nasubiri maelekezo kutoka juu,” alidai Lema.

Baadaye siku hiyohiyo saa 10:27 jioni, Lema kupitia akaunti hiyo aliandika: “Baada ya kusubiri masaa zaidi ya manne, sasa nimezuiwa rasmi kusafiri. Passport yangu imechukuliwa. Sasa napaswa kurudi nyumbani Arusha. Kwa maelezo zaidi niende makao makuu ya Uhamiaji Dodoma. Maumivu niliyonayo ni makali sana. Nilipaswa kutazama afya yangu zaidi kesho (07.06.2025) Nairobi. Sasa siwezi kuendelea tena na safari.”

Hata hivyo, Idara ya Uhamiaji kupitia kwa msemaji wake mkuu, Paul Mselle ilitoa taarifa kwa umma ikikiri kumzuia na kukanusha kuilenga Chadema.

“Idara ya Uhamiaji inapenda kuujulisha umma kuwa leo Juni 6, 2025 katika kituo cha uhamiaji cha mpaka wa Namanga mkoani Arusha, Godbless Lema alizuiwa kutoka nchini na pasipoti yake ya kusafiria kushikiliwa.”

Pia ilieleza kuwa Lema ametakiwa kuripoti ofisi za uhamiaji makao makuu kwa ajili ya mahojiano ambayo hata hivyo hayakuwekwa wazi.

“Utaratibu uliotumika kumzuia kutoka nchini ni wa kawaida na unatumika kwa raia yeyote pale ambapo idara imepata taarifa zinazohitaji mhusika kuhojiwa.

“Aidha, Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa za uongo zilizochapishwa na Lema kupitia mitandao ya kijamii kuwa zuio hilo linawalenga viongozi wote wa Chadema,” ilisema taarifa ya Uhamiaji.

Akizungumza na Mwananchi leo Juni 7, 2025 wakili mwandamizi mjini Iringa, Dk Rwezaula Kaijage amesema Tanzania inaongozwa na utawala wa sheria, hivyo vyombo vya dola visikamate watu kwa jambo ambalo halijawa kosa kisheria.

“Nchi yetu inaongozwa na utawala wa sheria na inaheshimika sana. Katika nchi za Kiafrika sisi ni miongoni mwa nchi bora. Mambo ambayo yanafanyika inabidi yafuate misingi ya kisheria, si utashi au maelekezo tu ya kisiasa,” amesema.

“Zipo restrictions (mazuio) za aina mbili za mtu kusafiri kutoka nje ya nchi yake au kwenda nchi nyingine. Zuio la kwanza ni kama lile ambalo ameliweka Rais Trump (Donald) wa Marekani kuwawekea vikwazo watu wa mataifa fulani fulani.

“Hilo ni zuio ambalo huwa linawekwa na mamlaka ya nchi. Lakini kuna restrictions ambazo zinatoka ndani kwa ndani. Kwamba sisi wenyewe tunagundua mtu fulani ni hatari kwa nchi fulani fulani huko nje, hata kama huko nje wanamuona ni mwema,” amesema.

Amesema nchi inaweza kuona huyo mtu akiruhusiwa kwenda huko nje atavuruga mambo na lawama zikarudi kwa nchi, ndiyo anazuiliwa.

“Sasa kinachotokea, si wazi sana kiasi kwamba hao watu ambao wamezuiwa na Uhamiaji kwa shinikizo la mamlaka za nje wasisafiri au ni sisi wenyewe hapa ndani na bahati mbaya sana haijaelezwa wazi. Tuko gizani,” amesema.

Amesema vyombo vya haki jinai vya Tanzania vinaaminika, hivyo vinapaswa kuepuka kukamata watu ili kuzuia makosa ya kufikirika au kuhoji mtu kwa hisia tu kuwa kuna kosa anaenda kulitenda.

“Yaani tunamfikiria mtu kwamba akifanya hivi atafanya makosa. Ili nchi iwe salama, vyombo vyetu vya usalama kwa vile ni mahiri katika uchunguzi wafanye kazi kwa weledi.

“Tunapomkamata kwa sababu ya kuzuia, tunaacha maswali yanayotoka kwa watu, vyombo na taasisi za kimataifa ambayo hayana majibu. Vyombo vyetu viache kazi kwa kupiga ramli,” amesema.

Dk Kaijage ametoa mfano wa miaka ya 80 kulipotaka kufanyika jaribio la mapinduzi, wale wote waliokamatwa walikamatwa wakiwa tayari wanakwenda kutekeleza mpango wao, lakini leo tunakamata watu kwa makosa ya hisia.

Wakili Madeleka amesema ni muhimu ikaeleweka kwamba nchi inaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na sheria hivyo jambo lolote linalofanywa na Serikali au na taasisi zake, ili liwe halali linapaswa kufuata na sheria na Katiba.

“Kisheria, Jeshi la Uhamiaji halina uhalali wowote wa kumzuia Mtanzania yeyote ambaye amefuata taratibu za kusafiri nje ya mipaka ya Tanzania.

“Sababu zilizotolewa na Uhamiaji katika kuhalalisha kitendo chao cha kumzuia Lema asisafiri nje ya nchi, zimejaa mzaha,” amedai.

Amesema Ibara ya 17 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatoa haki na uhuru wa kwenda popote duniani kama hujavunja sheria.

“Hakuna mahali popote, kwenye taarifa yao, Uhamiaji wameeleza ni sheria gani Lema ameivunja na ambayo inamzuia asisafiri nje ya nchi,” amesema.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THDRC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema tukio hilo linasikitisha na kuchafua nchi.

“Kwanza ni masikitiko yetu kwamba tunaona mamlaka za kisheria zinazotakiwa kusimamia haki zinazidi kukandamiza haki za baadhi ya makundi ya Watanzania hasa wapinzani,” amedai.

Amesema: “Kwa kawaida kwanza, mamlaka ya uhamiaji haina uhusiano wowote na makosa ya ndani, ya uhalifu. Si kazi yao. Kazi yao ni kusimamia watu wanaoingia na wanaotoka nchini au wageni wanaofanya kazi au kuishi hapa nchini.”

“Kusema kwamba kuna vitu tunachunguza, maana kuna makosa ya uhalifu ambayo si kazi ya uhamiaji. Kuzuia watu kwa sababu kuna uchunguzi mwingine nje na uchunguzi unaohusiana na nyaraka za kuondoka, si majukumu yao,” amesema.

Ole Ngurumwa amesema: “Wao wanapaswa kujiridhisha kwamba huyu mtu anaondoka kwa taratibu zile ambazo ni za kisheria? Awe ana pasipoti au awe na viza. Nje ya mamlaka zinazohusika zilipaswa kumtafuta Lema au Golugwa kwa njia zingine.”

Amesema: “Si kusubiri wakati anaondoka. Mtu amepanga safari yake, ameingia gharama na muda wote yuko kwenye mikutano ya hadhara. Kwa nini hawakumuita? Hebu tujiulize kama asingekuwa anaondoka nchini, maana yake wasingemkamata?”

Related Posts