NDOTO za Mlandege kumaliza katika nafasi ya nne zimefikia tamati baada ya jana jioni kukandwa bao 1-0 na Uhamiaji, huku Mafunzo ikibanwa nyumbani na Hard Rock katika mfululizo wa mechi za lala salama za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).
Mlandege ilikumbana na kipigo hicho cha saba kwa msimu huu kwenye Uwanja wa Mao A, huku Maafande wa Kipanga na Hard Rock zilikabana koo na kutoka suluhu Uwanja wa Mao B mjini Unguja.
Kipigo hicho kilichotokana na bao la dakika ya 43 la Mohammed Said Abrahaman, limeiacha Mlandege ikiporomoka kwa nafasi moja kutoka ya nane hadi ya tisa ikisaliwa na pointi 33 zilizotokana na mechi 26, huku Uhamiaji ikichupa kutoka nafasi ya tisa hadi ya saba kwa kufikisha pointi 35 sawa na ilizonazo Kipanga, wakati Hard Rock ikifikisha 30 sasa na kupanda hadi nafasi ya 10 kutoka ya 12.
Matokeo hayo kwa Mlandege yamefuta ndoto za mabingwa hao wa zamani wa Zanzibar na wanaoshikilia taji la Kombe la Mapinduzi kwa misimu miwili mfululizo, kumaliza ndani ya Nne Bora ya ZPL, kwani kwa sasa imesaliwa na mechi nne ambazo hata ikishinda zote itafikisha pointi 45
zilizopitwa na KVZ yenye 47 ambayo imeng’ang’ania katika nafasi hiyo kwa muda mrefu.
Mlandege ilisaliwa na nafasi hiyo ya kumaliza kwa heshima kwenye ligi hiyo baada ya kujiengua mapema katika mbio za ubingwa msimu huu ambao upo mikononi mwa timu tatu kwa sasa ikiwamo kinara JKU, watetezi KMKM na Zimamoto zilizopo ndani ya Tatu Bora.
Hata hivyo, Mlandege ina nafasi ya kuwania tiketi ya CAF kupitia michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) kwani tayari ni kati ya timu nne zilizotinga nusu fainali sambamba na Uhamiaji, JKU na Zimamoto.
Bingwa wa Ligi Kuu ndiye anayeiwakilisha Zanzibar katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati anayetwaa Kombe la FA hushiriki Kombe la Shirikisho Afrika na kwa msimu huu, KMKM na JKU ndizo zilizopeperusha bendera ya visiwa hivyo, japokuwa zote zilitolewa mapema.
KMKM iling’olewa na St George ya Ethiopia katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 5-2, kwani awali ililala 2-1 nyumbani na kucharazwa tena 3-1 ugenini, wakati JKU iliotolewa pia raundi hiyo na Singida Fountain Gate kwa jumla ya mabao 4-3, ililala ugenini 4-1 kisha kushinda nyumbani 2-0, japo mechi zote zilipigwa Uwanja wa Azam Complex.
JKU ndio watetezi wa Kombe la Shirikisho kwa sasa, lakini ikiongoza pia msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi 59 na imesaliwa na alama 10 kupitia mechi nne ilizonazo ili kubeba taji linaloshikiliwa na KMKM iliyopo nafasi ya tatu kwa sasa ikikusanya pointi 51, mbili pungufu na ilizonazo Zimamoto iliyopo nafasi ya pili.
ZPL inatarajiwa kuendelea tena jioni ya leo kwa michezo miwili, ratiba ikionyesha New City itakwaruzana na Kundemba, huku Malindi itaumana na KVZ na mechi zote zikipigwa kuanzia saa 10:30 jioni.