Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump ameendelea kumuwashia moto mfanyabiashara na bilionea, Elon Musk baada ya kutamka hadharani kuwa atakumbana na adhabu kali endapo atawafadhili wagombea wa Chama cha Democrats.
Akizungumza jana Jumamosi kwenye mahojiano maalumu na NBC News, Rais Trump alisema kutakuwa na adhabu kali sana iwapo Musk atafadhili wagombea wa chama cha Democratic ili kupambana na wagombea wa Republican wanaoiunga mkono bajeti mpya ya chama hicho.
“Ikiwa atafanya hivyo, atalazimika kubeba matokeo ya hilo. Atalazimika kukabiliana na adhabu kali sana kama atafanya hivyo,” alisema Trump huku akigoma kufafanua ni adhabu gani zitamkumba bilionea huyo ambaye biashara yake imetikisika katika kipindi alichoingoza Doge.
Rais huyo pia alisema hana nia ya kurekebisha uhusiano wake na Musk baada ya ugomvi baina yao kuibuka wazi wiki hii.
“Hapana,” Trump alijibu alipoulizwa na mwandishi wa habari endapo analenga kerejesha uhusiano huo.
Alipoulizwa kama anadhani uhusiano wake na Mkurugenzi huyo wa Tesla na SpaceX umefikia mwisho, Trump alisema, “Nadhani ndivyo hivyo,”
Kauli za Trump zilikuwa pana zaidi tangu walipotishiana na kutupiana shutuma na Musk kwenye mitandao ya X na Truth Social mapema wiki hii.
Aliongeza kuwa anaamini Chama cha Republican sasa kimeungana zaidi kuliko hapo awali baada ya mvutano wao kuonekana hadharani.
Trump alienda mbali na kusena hana mpango wa kuzungumza na Musk siku za hivi karibuni.
“Nina mambo mengine mengi muhimu ya kufanya,sina nia yoyote ya kuzungumza naye,” alisema Trump huku akimshutumu Musk kwa kutweza na kutoheshimu ofisi ya Rais.
“Nadhani ni jambo baya sana, kwa sababu hana heshima. Huwezi kukosa heshima dhidi ya ofisi ya Rais.”
Alhamisi, Musk alichapisha mfululizo wa ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao wa X dhidi ya rais huyo, ukiwemo alioufuta baadaye uliodokeza uhusiano wa zamani kati ya rais na mtuhumiwa wa unyanyasaji wa kingono aliyefariki, Jeffrey Epstein.

“Hilo ni jambo la zamani sana, limezungumzwa kwa miaka mingi, hata wakili wa Epstein alisema sikuwa na uhusiano wowote. Ni habari za zamani,” alisema Trump.
Siku chache kabla ya mvutano wao kuibuka hadharani, Musk alikuwa akipinga vikali muswada wa matumizi wa Republican uliopitishwa na Bunge mwezi uliopita.
Alhamisi akiwa Ikulu, Trump alijibu shutuma za Musk kwa kuwaambia waandishi wa habari kuwa: “Nimesikitishwa sana kwa sababu Elon alikuwa akielewa vizuri undani wa muswada huu. Nimesikitishwa sana na Elon. Nimewahi kumsaidia sana.”
Muda mfupi baadaye, Musk alichapisha mfululizo wa ujumbe, ikiwemo alioufuta uliomtaka Trump ang’olewe madarakani, na mwingine uliodai kuwa mpango wa ushuru wa rais huyo utasababisha mdororo wa uchumi baadaye mwaka huu.
Trump naye alijibu kwenye Truth Social. Katika moja ya machapisho, aliandika, “Sijali kama Elon ananigeuka, lakini alipaswa kufanya hivyo miezi kadhaa iliyopita, Musk alifahamu yaliyokuwa kwenye muswada kabla haujapitishwa.”
Aliongeza: “Njia rahisi zaidi ya kuokoa pesa katika bajeti yetu, mabilioni na mabilioni ya dola, ni kusitisha ruzuku na mikataba ya serikali kwa Elon,” akimaanisha mikataba ya serikali na SpaceX. “Nilishangazwa kila mara kwamba Biden hakufanya hivyo!.”
Jumamosi, Trump alisema hajafikiria tena pendekezo hilo la kusitisha mikataba ya serikali kwa kampuni za Musk.
“Ningeweza kufanya hivyo, lakini sijalipa suala hilo uzito zaidi.”
Trump pia alijibu wito kutoka kwa washirika wake wa nje, kama mwanaharakati wa mrengo wa kulia, Steve Bannon, ambao wamependekeza uchunguzi wa shughuli za kibiashara za Musk na rekodi yake ya uhamiaji.
Rais huyo aliiambia NBC News kuwa hajawahi kufanya mazungumzo kama hayo. “Sidhani kama ni jambo lililo katika akili yangu kwa sasa,” Trump alisema.
Musk alitoa msaada mkubwa wa kifedha kwenye kampeni ya Trump ya urais mwaka 2024, akitumia zaidi ya dola milioni 250 (zaidi ya Sh665 bilioni) kumsaidia katika majimbo yaliyokuwa na ushindani.
Katika miezi ya mwanzo ya serikali ya Trump alimuweka Musk kuwa Mkuu wa Idara ya Ufanisi wa Serikali (Doge), ambako alisimamia kufukuzwa kwa maelfu ya wafanyakazi wa serikali na kufungwa ama kupunguzwa kwa bajeti ya mashirika kadhaa.
Hata hivyo, Trump alisema mvutano baina yake na Musk, umefanya wabunge kuona faida za muswada huo.

“Nadhani, kwa kweli, Elon ameibua nguvu za muswada huo kwa sababu watu ambao hawakuwa makini sasa wameanza kuufuatilia, na wanaona jinsi ulivyo mzuri,” Trump alisema.
“Hivyo kwa upande huo, amefanya jambo kubwa. Lakini nadhani Elon, kwa kweli ni aibu kwamba amekuwa mwenye huzuni na kuvunjika moyo kiasi hiki.”
Katika mahojiano kwenye kipindi cha “This Past Weekend w/ Theo Von” yaliyorekodiwa Alhamisi lakini kutolewa Jumamosi, Makamu wa Rais, JD Vance alieleza mashambulizi ya Musk dhidi ya Trump kama “ya nyuklia” na kusema huenda isiwezekane tena kwa Musk katika kundi lao.
“Daima nitakuwa mwaminifu kwa rais, na natumai kwamba hatimaye Elon atarudi kundini. Labda hilo haliwezekani sasa kwa sababu amevuka mipaka,” Vance alimwambia Theo Von.
Makamu huyo wa rais pia alisema kosa kubwa analolifanya Musk ni kuonyesha hasira zake waziwazi na kumshambulia rais kuhusu toleo la muswada lililopitishwa na Bunge.
“Nadhani kuna hasira tu upande wake. Lakini kwa kweli, kaka, nadhani ilikuwa kosa kubwa sana kumshambulia rais kwa namna hiyo,” alisema Vance.