Katika safari ya maisha ya ndoa au uhusiano wa kimapenzi, hakuna hisia kali kama zile zinazohusiana na upendo na chuki.
Mapenzi ni hisia inayoweza kukuinua hadi mawinguni, lakini chuki inaweza kukupeleka katika giza la hisia mbaya, kutoelewana na hata kutengana.
Lakini swali kuu ni: je, inawezekana kweli ukamchukia mwenza wako iwe ni mume au mke milele? Na kama chuki hiyo inaweza kuwepo milele, ni nini kifanyike ili uhusiano wenu usifikie kiwango hicho cha chuki hiyo ya milele?
Chanzo cha chuki katika ndoa
Chuki haitokei tu ghafla. Ni zao la matukio ya kujirudia, maumivu yasiyotibiwa, hisia zilizozimwa, au matendo yaliyoacha makovu yasiyopona.
Inaweza kujengwa kutoka kwa vitu “vidogo” kama kutopewa usikivu, kutothaminiwa, au mambo “makubwa” kama usaliti, uongo wa kudumu, au ukatili wa kimwili na kiakili.
Watu wengi wanapofikia hali ya kusema “Nimemchukia mume wangu” au “Siwezi hata kumuona mke wangu,” huwa hawajaanza na chuki hiyo; ni mchakato wa kihisia unaoendana na kukata tamaa polepole.
Hali hii hujengwa na ukosefu wa mawasiliano, kutoelewana kwa muda mrefu, au hisia za kuumizwa mara kwa mara bila kuwapo kwa suluhisho.
Binadamu ni viumbe wa hisia zinazobadilika. Watu wengi waliowahi kuhisi chuki kali kwa wake au waume zao, huja kubadilika baadaye, labda kwa sababu ya muda, uponyaji wa kiakili, au mabadiliko ya muktadha wa maisha.
Chuki ya milele inakuwepo pale ambapo mtu ameharibiwa sana kihisia au kimwili, kiasi kwamba haoni tena uwezekano wa kurekebisha.
Kwa mfano, mtu aliyepitia ukatili wa muda mrefu au usaliti mkubwa, anaweza kujenga ukuta wa chuki ambao haubomoleki hata baada ya muda mrefu.
Lakini ukweli ni kwamba hisia zina uwezo wa kubadilika. Kwa hiyo, hata kama mtu anahisi chuki kali leo, si lazima iwe milele.
Uwezekano wa kubadilika huwa mkubwa endapo kutakuwepo na mchakato wa uponyaji wa kweli na wa dhati.
Ili kuelewa kama chuki inaweza kudumu, tunapaswa kuelewa nini huchochea kudumu kwake:
Mosi, kutosamehe: Kukosa msamaha ni moja ya vyanzo vikuu vya chuki ya kudumu. Watu wengi hushikilia makosa ya wenzao kwa miaka mingi.
Pili, maumivu ya mara kwa mara: Ikiwa mwenza anaendelea kuumiza bila kubadilika, chuki huzidi kuimarika.
Tatu, ukosefu wa mawasiliano:Kutozungumza au kufunguka kuhusu hisia kunaweza kufanya maumivu yakue kimya kimya na kugeuka chuki.
Nne, kupoteza imani: Pale ambapo imani ikivunjika, hasa kupitia usaliti, ni vigumu sana kurudisha hali ya kawaida.
Tano, migongano ya maadili au matarajio: Wakati mwingine watu hujihisi wamefungwa na mtu ambaye hawana uelewano wa msingi, hali inayoweza kuleta hofu, hasira na hatimaye chuki.
Mbinu kuzuia chuki ya milele
Kuepuka kufika hatua ya kuchukiana milele kunahitaji juhudi, nidhamu ya kihisia, na mawasiliano ya mara kwa mara. Wataalamu wa masuala ya uhusiano wanataja mbinu kadhaa za kuzuia hali hii:
Mosi, kujifunza msamaha wa kweli.Msamaha hauhusu kusahau, bali ni kuamua kuachilia maumivu kwa ajili ya amani yako na ustawi wa uhusiano. Msamaha huondoa chuki kabla haijakomaa kuwa ya kudumu.
Pili, kujenga mazungumzo ya kila wakati
Wapenzi wengi hupotea kwa sababu wanazungumza tu mambo ya lazima kama bili za umeme, watoto, au kaziwakisahau kujadili hisia zao, matarajio yao na hata maumivu yao. Mawasiliano ya kina hujenga ukaribu na uelewa unaozuia kukua kwa chuki.
Tatu, kutafuta ushauri au msaada wa kitaalamu.Wakati mwingine uhusiano unaingia katika giza kiasi kwamba wenza hawawezi tena kuwasiliana au kusamehe.
Hapa ndipo mtaalamu wa ndoa au mshauri anaweza kusaidia kuvunja ukuta wa chuki na kurudisha hali ya kuaminiana.
Nne, kujichunguza na kukubali makosa
Wenza wengi huchukiana kwa sababu kila mmoja anaona makosa ya mwenzake pekee.
Kukubali kuwa umechangia matatizo na kujitahidi kujirekebisha, kunaweza kuwa njia ya kuokoa uhusiano.
Tano, kuhifadhi mapenzi kwa matendo madogo. Mapenzi hayatunzwi kwa maneno tu. Ni matendo ya kila siku kama kutuma ujumbe wa mapenzi, kusaidia kazi za nyumbani, au kuonyesha shukrani. Haya yanaweza kuzuia sumu ya chuki isijengeke.
Sita, kujua wakati wa kuondoka. Ingawa makala haya yanalenga kuzuia chuki ya kudumu, ni muhimu pia kutambua kuwa si kila uhusiano unaweza kuponywa. Kuna wakati kuendelea kung’ang’ania kunaongeza chuki na kuharibu maisha ya watu wote wawili.
Katika hali za ukatili wa majumbani, udhalilishaji wa kihisia, au usaliti wa mara kwa mara, kuachana kwa amani kunaweza kuwa njia bora ya kuzuia chuki kuwa ya milele.
Ikumbukwe kuwa chuki katika uhusiano haiji tu ghafla, bali ni matokeo ya mfululizo wa maumivu yasiyotibiwa. Ingawa inawezekana kumchukia mwenza milele, haipaswi kuwa hivyo.
Kwa kujenga utamaduni wa mazungumzo, msamaha, kuelewana, na kusaidiana kihisia, wenza wanaweza kuzuia uhusiano wa kuingia kwenye giza la kudumu la chuki.
Na kwa wale waliokwisha kufika huko, bado kuna tumaini ikiwa wote wawili wako tayari kuponya majeraha, kusamehe na kujifunza upya kupendana.