Pesa zinavyowapa wanaume wanawake ‘rahisi’

Dar es Saalaam. Pesa ni nguvu, na nguvu ni kitu muhimu kuliko kitu chochote hapa duniani. Hata kabla ya kuanza mfumo wa pesa za karatasi tunazotumia leo, pesa zilikuwa zinatumika.

Binadamu wa kale alitumia nguvu na maarifa kama pesa, ili apate chakula ilibidi atumie vitu hivyo viwili kuwinda sungura au kupanda juu ya mti kuangusha fenesi. Kwa wakati ule hiyo ndiyo ilikuwa pesa.

Ukiweka pembeni kazi za Mungu tu, pesa inaweza kufanya kila kitu kingine kinachobaki chini ya jua kama  kununua muda, kununua akili, kununua afya bora, kununua heshima, kununua pesa zingine,  yaani inaweza kufanya kila kitu.

Ukiwa na pesa utakuwa na marafiki wengi, utapendwa na kila mtu, utaheshimiwa na utathaminiwa. Lakini changamoto inayokuja ni kwamba, ukiwa na pesa kuna baadhi ya mambo huwezi kuyapata kiuhalisia. Kwa mfano, kupata mwanamke ambaye unatamani ni vigumu.

Kwanini? Kwa sababu pesa ina kawaida ya kutojificha, ukiwa na pesa lazima watu watafahamu kwa jicho la kwanza watakaloelekeza kwako. Hata ukijiweka katikati ya kundi kubwa la watu, pesa itakuchomoza juu na kusema nipo hapa, kwa huyu bwana.

Hii maana yake ni nini? Ni kwamba kila mtu uliyemzidi pesa atataka kuwa rafiki yako. Kila mtu ataigizia kukuheshimu, kila mtu ataigiza kupenda na kutamani kuwa karibu yako.

Maana yake ni kwamba hata kama leo hii ukimtaka mwanamke ambaye yeye binafasi hakuwa na sababu ya kuwa na wewe kwa maana ya upendo  atakukubali kwa sababu kuna kitu kingine anaweza kupata ambacho ni pesa zako.

Na hii ndiyo sababu tunasema pesa zinatupa wanawake wepesi. Mwanamke imara na mzuri ni yule ambaye anahitaji pesa sana sana sana, lakini hayuko tayari kufanya kinyume na matakwa yake au kufanya vitu visiyompendeza, ikiwemo kuwa na mtu ambaye hampendi ili tu apate hizo pesa anazozihitaji sana.

Mwanamuziki wa Tanzania, Wakazi aliwahi kuandika. ‘Mwanamke mzuri ni mwenye tabia njema na mapenzi ya dhati, na mapenzi hayanunuliki kwa pesa. Unaweza kununua tendo la kufanya mapenzi, lakini sio upendo’ huu ndiyo ukweli.

Hii sio kwamba tunawalaumu wanawake kwamba wanapenda pesa, hapana. Ukweli ni kwamba tunaongelea wanawake kwa sababu hii ni safu ya Tuongee Kiume, lakini hata wanawake wenye pesa pia, pesa zao zinawapa waanaume dhaifu. Wanaume walioshindwa kutafuta vyao, wanaotegemea kuhudumiwa.

Mambo  muhimu  kumalizia, si vibaya kuwa na mwenza mwenye pesa, lakini cha kujiuliza  je, uko hapo kwa sababu ya pesa zake, au una sababu iliyo mbali sana na hiyo nguvu yake kiuchumi?

Related Posts