Makandarasi wazawa waula, Daraja Kigongo – Busisi kuanza kutumika Juni 19

Mwanza. Rais, Samia Suluhu Hassan anatarajia kufungua Daraja la Kigongo- Busisi (JP Magufuli) Juni 19, mwaka huu.

Daraja hilo lililojengwa na kampuni ya China Civil Engineering (CCECC) kwa Sh716 bilioni ni la kwanza Afrika Mashariki na kati likiwa na urefu wa Kilomita tatu na urefu wa mita 17 kutoka usawa wa bahari.

Litakuwa na uwezo wa kupitisha magari 20,000 kwa siku moja tofauti na vivuko ambavyo vilikuwa vinavusha magari 500 hadi 600 kwa siku, huku likiwa na uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa tani 160 za mizigo kwa pamoja.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Juni 8, 2025 na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika daraja la Kigongo- Busisi ukilenga kueleza mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita.

Amesema Rais Samia amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha ndoto hiyo iliyoasisiwa na hayati John Magufuli inakamilika kwani wakati huo lilikuwa limetekelezwa kwa asilimia 25 pekee na zaidi ya Sh200 bilioni zikiwa zimelipwa kwa mkandarasi, ambapo fedha zilizotumika kwenye daraja hilo zingejenga zaidi ya Kilomita 350 za barabara kwa kiwango cha lami.

Ulega amesema wizara itawaombea wananchi vibali maalumu kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili wafanye shughuli za kijamii ikiwemo kurekodi kwaya, picha na matukio ya kijamii kwenye daraja hilo, huku kukiwa na uangalizi wa karibu kuhakikisha usalama wao.

“Imefanyika kazi kubwa licha ya kupitia kipindi kigumu sana zaidi ya Sh500 bilioni zilikuwa zinahitajika zilipwe na Korona (Uviko 19) ilikuwa imeingia lakini Rais (Samia Suluhu Hassan) alisimama imara na kuhakikisha mambo yanaenda sawa,” amesema Ulega.

Ameongeza kuwa; “Hii ni ishara kwamba tukiendelea na utulivu wetu na kuheshimiana tutaendelea kupiga hatua na kutatua changamoto zetu sisi wenyewe. Hii itakuwa ni moja ya tunu zetu tumefanya wenyewe ni alama kubwa ya kujivunia kwani litadumu kwa zaidi ya miaka 100.”

Ulega amesema faida kubwa ambayo Taifa limeipata kupitia mradi huo ni wataalamu wazawa kushiriki kuanzia hatua ya kwanza hadi kukamilika kwake, na kuchota ujuzi mbalimbali ikiwemo teknolojia ya ujenzi wa madaraja makubwa na usimamizi wa miradi hiyo.

Amesema Serikali itaanza kuwaamini na kuwapa miradi mikubwa ya kimkakati makandarasi hao wazawa waliovunwa kwenye miradi mbalimbali badala ya kutegemea kampuni za kigeni.

“Wataalamu wazawa walifanya ushiriki kuanzia hatua ya mwanzo ya ubunifu, huko mbele ya safari tukiwa na miradi mikubwa kama huu watapata nafasi kwa sababu wamepata  elimu na utaalam wa kutosha,” amesema Waziri Ulega na kuongeza;

“Kwa mfano tunaye Mhandisi Kaswaga (Katelula) ambaye ni ofisa wa mradi huu amefanya kazi kuanzia mwanzo mpaka mwisho na pia anasimamia madaraja ya Simiyu na Pangani ni miongoni mwa wataalamu wazawa tunaowategemea. Huyu na wenzake wataaminiwa na kupewa miradi kwa sababu ipo mingi inayoendelea na inayokuja.”

Akilizungumzia hilo, mkandarasi mzawa aliyesimamia mradi wa Kigongo-Busisi, Katelula Kaswaga amesema hatua hiyo ni nzuri kwa wataalamu wazawa kwani wakiaminiwa wana uwezo wa kutekeleza miradi hiyo, huku wakihitaji uwezo wa kifedha, mitambo, vifaa na wafanyakazi.

Amesema Watanzania zaidi ya 2,000 wameshiriki katika mradi huo katika hatua mbalimbali wakiwemo wahandisi na mafundi.

“Mfano mwaka wa kwanza tulikuwa na wataalamu wazawa 1,016 na tumejifunza kuanzia usanifu wa mradi, ujenzi, teknolojia ya kusimika nguzo chini ya maji, mahesabu ya kuanza ujenzi, usalama, namba ya kujenga, kutazama ubora wa daraja na usalama wa mazingira wakati wa ujenzi,” amesema Kaswaga.

Baadhi ya wakazi wa Busisi wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, akiwemo Farida John amesema daraja hilo litasaidia kuondoa msongamano wa abiria uliopo kwa sasa kwenye vivuko.

“Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uthubutu wa kukamilisha huu miradi, utaokoa watu wengi waliokuwa wanapata tabu sana hapa,” amesema Farida.

Naye, Nyanda Michael ameiomba Serikali kuhakikisha mradi huo unasimamiwa vizuri ili ulete matunda yaliyokusudiwa kwa wananchi wa Kandaya Ziwa kwa sababu wamekuwa wakiteseka kwa muda mrefu kutokana na kuharibika mara kwa mara kwa vivuko vilivyopo.

Related Posts