UCHAGUZI MKUU 2025: Taasisi ya Nyerere yataka rushwa idhibitiwe

Dar es Salaam. Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imetaka vitendo vya rushwa vidhibitiwe katika chaguzi kuanzia kwenye michakato ya kuwapata wagombea ndani ya vyama hadi mchakato wa Oktoba 2025 utakaosimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Taasisi hiyo imeeleza kuwa jambo hilo likifanyika watakuwa wanamuenzi vema muasisi ya Taifa hili, hayati Julius Nyerere ambaye alikuwa mkali inapofika uchaguzi, akipinga vita vitendo vya wagombea kutumia rushwa ili kupata madaraka.

Raia hiyo imetolewa leo Jumapili Juni 8, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi hiyo, Mizengo Pinda katika kikao cha bodi kilichokuwa kikijali masuala mbalimbali ikiwamo namna taasisi hiyo itakayosonga mbele na masuala yanayohusu jamii ukiwemo uchaguzi mkuu.

“Moja ya jambo tunalotaka kuliona likisimamiwa na kudhibitiwa ni vitendo vya rushwa, hili likidhibitiwa na kusafishwa huko aliko Mwalimu ataona nimeliacha Taifa katika mikono salama,” amesema Pinda.

Pinda ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu amesema taasisi hiyo, inaamini kuwa hakuna Mtanzania anayebisha kuhusu umuhimu wa amani na utulivu wa nchi.

“Lakini pia hatuna mashaka yanayosemwa kuhusu demokrasia ambayo ni vizuri ikajionyesha zaidi kutokana na utaratibu tuliojiwekea. Isiwe unaimba mdomoni, lakini ukija katika utekelezaji mambo tofauti.”

“Hata hivyo, hadi sasa kuanzia ndani ya chama chenyewe jitihada zipo za kuhakikisha kunakuwa na utaratibu wa kuzingatia demokrasia katika uendeshaji wa mambo na haki itendeke pale katika uamuzi wa kuamua ni nani aingie,” amesema Pinda.

Pinda amewaambia Watanzania uchaguzi unakuja hivyo wajiandae kuimarisha amani na utulivu na kila mmoja atambue kuwa anayo haki ya kugombea ili apigiwe kura au kupiga kura ya kumchagua kiongozi.

“Sasa wale waliopewa dhamana ya kusimamia utaratibu mzima wahakikishe mwenye sifa stahiki za kupata, wapewe, asiyestahili kwa utaratibu ulivyo aambiwe hapana…naamini kabisa tutatoka vizuri na nchi itaendelea kuwa shwari,” amesema Pinda.

Pinda amefafanua kuelekea uchaguzi mkuu, taasisi imebeba kaulimbiu ya ‘chagua viongozi bora, kwa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu kwa Taifa letu.’

“Katika uchaguzi huu, tumesisitiza kuhusu ubora wa anayegombea, kwa sababu ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi hasa mnapokuwa mnatazama mwelekeo wenu mnapokwenda,” amesema Pinda.

Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Paul Kimiti katika kikao chao walichokifanya jijini Dodoma hivi karibuni na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango waliazimia kuwa miongoni mwa majukumu watakayoyafanya ni kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.

Hata hivyo, jana Jumamosi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa salamu za Serikali katika Baraza la Eid El Adh’haa aliwahakikishia Watanzania uchaguzi wa Oktoba 2025 utakuwa huru na haki.

Kwa mujibu wa Paul Kimiti, aliyewahi kuwa mbunge na waziri kwa nyakati tofauti amesema falsafa za Mwalimu Nyerere ni kwamba binadamu yeyote anapochaguliwa wajibu wake wa kwanza ni kujenga haki, amani, utulivu na umoja.

“Baada ya kikao hiki tutapanga namna ya kwenda mikoani, kutoa elimu kuhusu shabaha na madhumuni ya uchaguzi. Pia Baba wa Taifa alipenda vyama vya siasa, vinavyozungumzia sera na kukosoa chama tawala kwa ustaarabu bila lugha ya matusi,” amesema Kimiti.

Mjumbe wa bodi hiyo, Dk Maua  Abeid Daftari, ambaye pia aliwahi kuwa naibu waziri wa mawasiliano na uchukuzi, amesema hayati Nyerere alipenda sana vijana na alikuwa akiwashirikisha katika shughuli za chama na maendeleo.

“Kama ambavyo alivyokuwa akifanya hayati Nyerere, tunaona viongozi wetu wa sasa wanatoa msukumo zaidi kwa vijana kushiriki katika uchaguzi ili kuchagua na kuchaguliwa. Hiki ni kitu kizuri, kwa sababu vijana wanapata nafasi ya kutoa mchango ndani ya chama na maendeleo ya nchi yetu,” amesema Dk Daftari.

Related Posts