Mwanga. Serikali imesema itahakikisha Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro inakuwa na shule mbili za sekondari za ufundi ikilenga kuboresha mazingira ya elimu nchini ili vijana waendelee kupata ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira hivi sasa.
Hayo yamesemwa jana jioni Juni 7, 2025 na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati akizungumza na wananchi wa Tarafa ya Ugweno alipokuwa akikagua shule mpya ya Sekondari Kilaweni inayojengwa kupitia mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
“Rais ametoa kipaumbele kikubwa sana katika elimu, mtoto ataanza shule akiwa na umri wa miaka sita na ikifika 2027 shule ya msingi itakuwa miaka 6, lakini haruhusiwi kuondoka shuleni mpaka afike kidato cha nne kwa sababu elimu ya lazima itakuwa ni miaka 10,”amesema Profesa Mkenda.
Aidha, amewashukuru wananchi wa wilaya hiyo kwa kutoa sehemu ya ardhi yao kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo na kuwaahidi kuongeza kasi ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika shule hizo.
“Niwapongeze wananchi kwa kutoa maeneo yenu, tutatuma mafundi na wataalamu kwenye shule hizi mbili za ufundi kuja kufanya tathmini, lakini kwa kuwa shule hizi zitakuwa chache, wanafunzi watakuwa wanalala kwa ajili ya kujisomea,” amasema Profesa Mkenda.
“Wataalamu waje Kisanjuni, pia waangalie nini kitahitajika, tuangalie gharama na michoro, mlichokifanya ninyi ndugu zangu kutoa maeneo yenu ni kufanya wepesi wa utekelezaji wa maelekezo kwa wananachi wetu.”
“Nimefika hapa katika Shule ya Kisanjuni baada ya kupitia Shule ya Kilaweni, ninyi mmejitolea ardhi kubwa. Juhudi zinazofanywa na mbunge wetu ni kuhakikisha Mwanga inakuwa ya kwanza na kinara, sambamba na Veta, lakini pia iwe na shule mbili za sekondari za ufundi,” amesema Profesa Mkenda.
Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Mbunge wa Mwanga, Joseph Thadayo amesema kwa miaka mitatu na nusu, wilaya hiyo imepokea Sh8.56 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya madarasa, ujenzi wa mabweni, matundu ya vyoo na ujenzi wa shule mpya mbili.
“Naishukuru sana Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele kikubwa katika sekta ya elimu hapa Mwanga, kwa miaka mitatu na nusu imetupa Sh 8.56 bilioni kwenye sekta ya elimu,” amesema Thadayo.