Songea. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema wanaotaka uchaguzi mkuu Oktoba 2025 uhairishwe, wahairishe mambo yao wenyewe.
Wasira amesema tayari CCM imeshajipanga kwa uchaguzi mkuu kwa kuwateua wawakilishi wa nafasi ya urais na makamu wa Rais ambao ni Rais Samia Suluhu Hassan na Dk Emmanuel Nchimbi.
Rais Samia na Dk Nchimbi wanasuburi kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa wagombea urais.
Licha ya Wasira kutotaja kwa jina wanaosema uhairishwe uchaguzi huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ndiyo chama kinachoendesha kampeni ya No reforms no election ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’ maeneo mbalimbali nchini.
Chadema inafanya mikutano ya hadhara sasa wapo kanda ya kati ya Morogoro, Dodoma na Singida wakielimisha wananchi juu ya kampeni hiyo wakisema hawatashiriki uchaguzi huo hadi mabadiliko yafanyike huku wakitaka uchaguzi huo uhairishwe.

Leo Jumatatu, Juni 9, 2025, Wasira amewasili mkoani Ruvuma kuanza ziara ya ujenzi wa chama.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Songea katika ofisi za CCM amesema ni ngumu kuhairisha uchaguzi.
“Wapo rafiki zangu wa ‘Tone Tone’ wanapita wanawaambia wananchi tusifanye uchaguzi, mimi nawauliza tusipofanya wananchi waongozwe na nani,” amehoji Wasira.
“Wanasema tuhairishe uchaguzi, hatuhairishi ng’o, hairisha mambo yako mwenyewe sisi tayari tumeshaweka wagombea.”
‘Tone tone’ ni kampeni maalumu ya Chadema inayolenga kuhamasisha Watanzania kukichangia fedha chaka hicho kuwezesha shughuli mbalimbali za chama hicho.
Mkoa huo wa Ruvuma unakuwa wa 12 kwa kiongozi huyo kutembelea tangu ashike nafasi ya umakamu mwenyekiti wa CCM Bara Januari 2025.
Katika mikoa yote aliyotembelea Wasira amesema chama hicho bado kipo imara na kinamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na utendaji wake.
Awali, akimkaribisha Wasira, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Odo Mwisho amesema mkoa huo upo salama na umejiandaa na uchaguzi mkuu.
Wasira atakuwa mkoani Ruvuma kwa siku nne kuanzia leo Jumatatu baadaye kuelekea mkoani Mwanza kwa siku nne na kuhitimisha ziara yake mkoani Geita Juni 23, 2025.