Los Angeles. Hali ya taharuki imeendelea kuongezeka jijini Los Angeles baada ya maelfu ya waandamanaji kumiminika mitaani wakipinga hatua ya Rais Donald Trump kuwafurusha wahamiaji wasio na vibali nchini humo.
Kufuatia hatua hiyo, Rais Trump aliamuru wanajeshi zaidi ya 2,000 kumwagwa maeneo yanapofanyika maandamano hayo, ili kukabiliana na waandamanaji na kuimarisha ulinzi dhidi ya majengo na ofisi za Serikali jijini humo.
Maandamano hayo yaliyoanza Ijumaa ya wiki iliyopita kama mzaha baada ya baadhi ya wanaharakati kudai kuwa Rais Trump amekuwa akitumia mamlaka yake kuendesha ukamataji holela wa watu kwa kisingizio cha uraia.

Waandamanaji walifunga barabara kuu za kuingia na kutoka jijini humo huku wakichoma magari yanayojiendesha hususan yanayotengenezwa na Kampuni ya Tesla, jambo lililowalazimu maofisa wa usalama kutumia mabomu ya machozi, risasi za mpira na baruti kuwatawanya.
Baadhi ya polisi wenye farasi pia wameonekana mitaani wakiendelea na doria huku wengine wakiwa wamevaa mavazi ya kukabiliana na ghasia nyuma ya wanajeshi waliotumwa kulinda majengo ya Serikali nchini humo, likiwemo la kituo kinachotumika kuwaweka kizuizini wahamiaji wasio na vibali vya kuishi nchini humo.
Polisi walitangaza kuwa maandamano hayo ni haramu na kufikia jana jioni, waandamanaji wengi walikuwa tayari wameondoka mitaani.
Hata hivyo, waandamanaji waliobaki walichukua viti kutoka bustani ya umma ya karibu na kujenga vizuizi vya muda, wakirusha vitu kuelekea walipo askari polisi na jeshi upande wa pili wa barabara walipokuwa.
Wengine waliokuwa juu ya barabara kuu ya 101 iliyofungwa upande wa kusini walirusha vipande vya zege, mawe, skuta za umeme na fataki kwa polisi wanaofanya doria eneo la California na magari yao yaliyokuwa yameegeshwa barabarani.

Polisi walikimbilia chini ya daraja kujificha baada ya kulemewa na mashambulizi hayo.
Kwa mujibu wa Associated Press, maandamano hayo yamechochewa na operesheni inayoendeshwa na Idara ya Uhamiaji (DEI) chini ya Rais Trump ambapo imekuwa ikiendesha msako mitaani dhidi ya inaowaita wahamiaji haramu.
Kitendo cha maofisa wa DEI kuingia mitaani na kukamata kinyemela wananchi hususan wenye asili ya Kilatino, kimeibua hasira na hofu kwa baadhi ya wakazi wa jiji hilo.

Maandamano ya jana hususan eneo la Paramound jijini Los Angeles, jiji lenye wakazi takriban milioni nne ambapo asilimia zaidi ya 84 ni Walatino, yalijikita katika maeneo kadhaa yaliyoguswa na kamatakamata hiyo.
Kuanzia asubuhi, wanajeshi wa National Guard walisimama bega kwa bega, wakiwa na bunduki ndefu na ngao za ghasia nje ya Kituo cha Metropolitan Detention Center.
Waandamanaji walipaza sauti wakiimba nyimbo zenye maneno kama…Oneni aibu…rudini nyumbani kwenu.
Baada ya baadhi yao kuwasogelea wanajeshi kwa karibu, maofisa wengine waliovaa sare walivamia kundi hilo na kurusha mabomu ya kutoa machozi barabarani.
Dakika chache baadaye, Idara ya Polisi ya Los Angeles ilifyatua risasi za kuutawanya umati, wakisema waandamanaji walikuwa wamejikusanya kinyume cha sheria.

Gavana kutoka chama cha Democrats, Gavin Newsom alimwandikia Trump barua Jumapili mchana akimtaka awaondoe wanajeshi hao, akiuita uamuzi wa kupeleka wanajeshi katika eneo hilo ni ukiukaji wa sheria za jimbo hilo.
Newsom, alikuwa mjini Los Angeles akikutana na maofisa wa usalama wa ndani. Haikujulikana kama alikuwa amezungumza na Trump tangu Ijumaa.
Upelekaji huo wa wanajeshi unaonekana kwa mara ya kwanza kwa miongo kadhaa ambapo walitumwa bila ombi la gavana wa jimbo, jambo lililoashiria hatua kubwa dhidi ya wanaopinga sera za kufukuza wahamiaji kwa wingi.
Meya wa Los Angeles, Karen Bass naye aliunga mkono msimamo wa Newsom.
“Kile tunachoshuhudia Los Angeles ni machafuko yanayochochewa na utawala. Hii ni ajenda tofauti kabisa, siyo kuhusu usalama wa umma,” amesema Bass katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo alasiri.
Hata hivyo, maneno yao hayajabadilisha msimamo wa Trump juu ya suala hilo.
“Madai ya Newsom kuwa hakukuwa na tatizo Los Angeles kabla ya Rais Trump kuingilia ni uongo wa wazi,” amejibu Msemaji wa Ikulu ya White House, Abigail Jackson.

Maofisa wa Serikali Kuu waliwakamata wahamiaji maeneo mbalimbali jijini humo ikiwa ni pamoja na eneo maarufu kwa biashara ya mavazi, maegesho na maeneo mengine kadhaa siku ya Ijumaa.
Siku iliyofuata, walionekana wakijikusanya katika ofisi ya Idara ya Usalama wa Ndani karibu na eneo la maegesho huko Paramount, hali iliyoibua hofu miongoni mwa waandamanaji walioamini ni mbinu ya kujipanga dhidi ya kamatakamata nyingine.
Kwa mujibu wa jarida la Brennan Center for Justice, mara ya mwisho wanajeshi kupelekwa kupambana na ghasia walitumwa bila ruhusa ya gavana ilikuwa mwaka 1965, wakati Rais, Lyndon Johnson alipotuma wanajeshi kulinda maandamano ya haki za kiraia huko Alabama.
Katika agizp, Trump alitumia kifungu cha kisheria kinachomruhusu kupeleka wanajeshi wa Serikali iwapo kuna uasi ama hatari ya uasi dhidi ya mamlaka ya Serikali ya Marekani.

Alisema ameidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi 2,000 wa Jeshi la nchi hiyo.
Trump aliwaambia waandishi wa habari alipokuwa akijiandaa kupanda ndege ya Air Force One huko Morristown, New Jersey, Jumapili kwamba kulikuwa na watu wanaoendesha vurugu jijini Los Angeles akitamka hadharani kuwa kutakuwa na hatua kali dhidi yao.
“Tutakuwa na wanajeshi kila mahali. Hatutaruhusu hili litokee kwa nchi yetu. Hatutaruhusu nchi yetu ichanwe vipande kama ilivyokuwa chini ya Biden,” amesema Trump.
Takriban wahamiaji 500 walioko katika kambi ya Twentynine Palms, takriban maili 125 (kilomita 200) mashariki mwa Los Angeles, nao walikuwa katika hali ya utayari wa kupelekwa eneo hilo.
Makamu wa Rais wa zamani, Kamala Harris, anayeishi Los Angeles, alisema ukamataji wa wahamiaji na upelekaji wa wanajeshi ni sehemu ya mpango wa kikatili na wa kusambaza hofu na mgawanyiko.