Mfahamu Turbay mgombea urais aliyepigwa risasi, mama yake aliuliwa na Pablo Escobar

Bogota. Miongoni mwa habari zilizoteka vyombo vya habari ulimwenguni ni tukio la Seneta wa Colombi, Miguel Uribe Turbay kupigwa risasi akihutubia mkutano wa hadhara jijini Bogota nchini Colombia.

Hata hivyo maswali mengi yameibuka juu ya Turbay ni nani na kwa nini amelengwa na shambulizi hilo la kupigwa risasi?

Shirika la Habari la Associated Press limeripoti kuwa Uribe Turbay ambaye ni Seneta wa chama cha kihafidhina nchini Colombia, alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya wakati wa mkutano wa kampeni katika mji mkuu, Bogota.

Shambulio hilo la wazi, lililonaswa kwenye video, liliishtua taifa ambalo miongo kadhaa iliyopita lilizoea utekaji nyara na mauaji ya wanasiasa na watu mashuhuri.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Uribe Turbay (39) ambaye tayari ametangaza nia ya kugombea urais mwaka ujao (2026), hadi leo Jumatatu Juni 9, 2025, yuko kwenye hali mahututi baada ya kufanyiwa upasuaji jana Jumapili, siku moja baada ya kushambuliwa.

Madaktari wake wanasema anapigania uhai wake kutokana na shambulizi hilo.

Uribe Turbay ni mwanachama wa chama cha mrengo wa kulia cha Democratic Center (DC) na alitangaza rasmi nia yake ya kugombea urais Machi mwaka huu.

Mwanasiasa huyo amejipambanua kuwa sauti kuu ya upinzani dhidi ya Serikali ya Rais, Gustavo Petro ambaye ni mwanasiasa wa mrengo wa kushoto wa kwanza kuongoza Colombia. Petro haruhusiwi kugombea tena mwaka 2026.

Uribe Turbay, ambaye familia yake pia imeathiriwa na ghasia za kisiasa, alizindua kampeni zake rasmi Machi. Hata hivyo, Oktoba mwaka jana, alichapisha video kwenye mitandao ya kijamii akitangaza nia yake ya kugombea huku akidai kuwa milima ya Copacabana katika jimbo la Antioquia ndiyo mahali aliporekodia video hiyo.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Hatima ya mrithi wa Rais Gustavo Petro itajulikana Mei 31, 2026.

Pablo Escobar amuua mama yake

“Mahali penye maana kubwa sana kwangu,” alisema kwenye video hiyo ni hapa ambapo mama yangu alitekwa nyara na Pablo Escobar na kuuawa wakati nilikuwa karibu kutimiza miaka mitano,” alisikika akisema Uribe Turbay kwenye video hiyo.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Mama yake, ambaye alikuwa mwandishi wa habari, Diana Turbay, alitekwa na genge la Medellin lililokuwa linaongozwa na Pablo Escobar kisha kuuawa kikatili mwaka 1991, wakati wa kipindi kigumu zaidi cha ghasia nchini Colombia.

Pablo Escobar alikuwa mfanyabiashara haramu wa dawa za kulevya kutoka Colombia. Aliuawa  Desemba 2, 1993. Alikuwa kiongozi wa kundi kubwa la ulanguzi wa dawa za kulevya lijulikanalo kama Medellín Cartel, ambalo lilihusika na kusambaza kiasi kikubwa dawa za kulevya kwenda Marekani na sehemu nyingine za dunia katika miaka ya 1980 hadi mapema miaka ya 1990.

Shambulio dhidi ya Uribe Turbay Jumamosi lilishtua taifa na kufufua kumbukumbu za enzi ambapo ghasia za kisiasa zilitikisa maisha ya umma nchini Colombia.

Uribe Turbay alianza siasa mapema, alipochaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Jiji la Bogota akiwa na miaka 25 mwaka 2012. Mwaka 2016, aliteuliwa kuwa Katibu wa Serikali wa jiji hilo na aliyekuwa Meya Enrique Peñalosa.

Mwaka 2022, alichaguliwa kuwa Seneta baada ya kualikwa kugombea na Rais wa zamani, Álvaro Uribe Vélez, ambaye hawana uhusiano wa kifamilia.

Uribe Turbay alizaliwa katika familia mashuhuri ya kisiasa. Yeye ni mjukuu wa Rais wa zamani, Julio César Turbay Ayala, aliyekuwa madarakani kati ya mwaka 1978 hadi 1982, na pia ni mjukuu wa upande wa baba wa Rodrigo Uribe Echavarría, aliyewahi kuwa mkurugenzi wa Chama cha Liberal.

Hakuwa akipewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa mwaka ujao, kwa mujibu wa kura za maoni za karibuni, na alikuwa bado anakabiliana na ushindani kutoka ndani ya muungano wake wa kisiasa.

Miongoni mwa mambo ambayo Uribe Turbay anayatumia kama vipaumbele vyake kwenye kampeni ni pamoja na masuala ya usalama, akiwa na lengo la kuvutia wawekezaji na kukuza uthabiti wa kiuchumi.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Seneta huyo anaendelea kupitia kile ambacho mamlaka zimeelezea kama hali ya wasiwasi baada ya kufanyiwa upasuaji katika kliniki binafsi jijini Bogotá nchini humo.

“Amefanyiwa upasuaji; hizi ni saa nyeti na muhimu sana kwa ajili ya uhai wake,” alisema Meya wa Bogotá, Carlos Galán mapema Jumapili baada ya kupata taarifa kutoka kwa wahudumu wa afya wa kliniki ya Fundación Santa Fe anakopatiwa matibabu.

“Hali yake ni mbaya sana na hatuwezi kutoa utabiri wa uhakika,” kliniki hiyo iliongeza saa chache baadaye katika ripoti mpya ya kitabibu.

Tayari Polisi nchini humo wamethibitisha kumkamata mtoto (15) kwa tuhuma za shambulio hilo na wamemtaja kama mshukiwa mkuu. Hata hivyo, mamlaka hazijatoa sababu rasmi ya shambulio hilo.
 

Related Posts