Wanakijiji wachanga mamilioni kujenga shule mpya

Musoma. Wazazi katika Kijiji cha Muhoji, Kata ya Bugwema  kwa kushirikiana na wadau wengine wamejitolea kuchanga Sh175 milioni kutekeleza mradi wa ujenzi shule mpya ya Sekondari ya Muhoji.

Akizungumza leo Jumatatu Juni, 9 2025 na  mkuu wa shule mpya, Joseph Ndalo amesema awali wanafunzi walilazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 20 na kurudi shule kila siku.

“Nimekuwa mkuu wa Shule ya Sekondari Bugwema kwa zaidi ya miaka 15 nilikuwa nashuhudia namna wanafunzi wanaotoka katika kijiji hiki cha Muhoji walivyokuwa wakipata shida kutokana na umbali kutoka hapa kijijini kwenda shule mama, wengi walikuwa wanakata tamaa na kushindwa kutimiza malengo ya kielimu,” amesema Ndalo.

Amesema kutokana na hali hiyo wanafunzi hao wamekuwa wakitafuta namna ya kuacha masomo huku baadhi yao wakiamua kufanya vibaya makusudi kwenye mitihani ya Taifa kidato cha pili kisha kuacha shule baada ya kushindwa kwenye mitihani hiyo.

Moja ya jengo lilojengwa kwa nguvu za wananchi, serikali na wadau wa maendeleo katika shule mpya ya Sekondari ya Muhoji wilayani Musoma. Picha na Beldina Nyakeke

Akizindua shule hiyo ambayo imeanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza Aprili mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya elimu ili kutoa fursa kwa watoto wote wenye sifa ya kusoma wapate fursa hiyo.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imetoa Sh1.7 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya tatu katika halmashauri hiyo katika kata za Bukima, Mugango na Nyamrandirira miradi ambayo tayari imekamilika na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa.

“Nikuagize mkurugenzi hakikisha mnakamilisha miundombinu yote muhimu katika mradi huu kwa wakati ili watoto hawa wawe na mazingira mazuri ya kusomea, Serikali itaendelea kuweka kipaumbele kwa suala zima la elimu na kuunga mkono jitihada za wananchi kama hawa wa hapa walioamua kuanzisha mradi huu muhimu kwa ustawi wa jamii ya hapa,” amesema.

Kanali Mtambi amesema suala la elimu ni kipaumbele kwa Serikali kutokana na umuhimu wake katika maendeleo na ustawi wa jamii, hivyo uwekezaji katika sekta ya elimu ni suala la lazima.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema wilaya hiyo imeandaa programu  maalumu kwa ajili ya kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila kujali jinsia zao.

“Mwezi uliopita tulifanya tathmini ya hali ya elimu na kuweka mikakati ya kuboresha elimu katika halmashauri yetu, tuliamua kuwa uwekezaji ulio bora na namba moja ni katika elimu ya watoto wetu hivyo tumekubaliana kuwa kila mtoto anapata elimu bora na hii itawapa fursa ya kujiunga na vyuo vikuu vya hapa nchini na nje ya nchi,” amesema Chikoka

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji wa Kijiji cha Muhoji, Samuel Owino amesema hadi sasa ujenzi wa shule hiyo umegharimu zaidi ya Sh175 milioni fedha ambazo zimetokana na michango ya wananchi, Serikali na wadau mbalimbali.

“Tayari shule imesajiliwa na hadi sasa kuna wanafunzi 56 wa kidato cha kwanza, muda si mrefu tunaanza ujenzi wa awamu ya pili,  utahusu miundombinu kama vile maabara, nyumba za walimu, maktaba na ofisi,” amesema Owino.

Owino amesema kutokana na changamoto ya umbali kutoka kijijini hapo hadi shule mama, wazazi kwa pamoja waliamua kuanza ujenzi wa shule hiyo hadi sasa wamekamilisha ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, vyoo na maboma kwaajili ya ofisi.

Mbunge wa Musoma Vijijini,  Sospeter Muhongo amesema mikakati tayari imewekwa kuhakikisha shule hiyo inakamilika kwa wakati na kutoa elimu bora na ilivyokusudiwa.

Amesema  tayari wamejiwekea malengo ya kuwa na shule za sekondari katika vijiji vyote 68 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa shule za sekondari katika kata zote 21 za halmashauri hiyo.

Mkazi wa Kijiji cha Muhoji, Prisca Manyama amesema umbali wa shule ya sekondari ulisababisha mtoto wake kaucha shule alipofika kidato cha pili.

Related Posts