Sheria ya NHC yawabana waajiri, adhabu zaongezwa

Dodoma. Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Shirika la Nyumba la Taifa ya Mwaka 2025, unaoongeza adhabu na kuondoa wajibu wa mwajiri kukata kodi ya nyumba pamoja na faini ya kuchelewesha kodi kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi, ambaye ni mpangaji.

Marekebisho hayo yamepitishwa leo, Jumatatu Juni 9, 2025 baada ya kuwasilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi na kujadiliwa na wabunge.

Kifungu cha 16 cha sheria hiyo kimebadilishwa ili kuweka adhabu kwa kauli za uongo zitakazotolewa na mwombaji mkataba wa upangishaji na ushirikiano au huduma yoyote.

Kwa mujibu wa muswada huo mwombaji wa mkataba wa upangishaji, ushirikiano au huduma nyingine yoyote ambayo kwa makusudi anashindwa kufichua taarifa au kwa makusudi hutoa taarifa ambayo anajua ni ya uongo atakuwa ametenda kosa.

Kwenye kesi ya mkataba wa upangishaji au ushirikiano kati ya shirika na mtu binafsi, atawajibika kwa faini isiyopungua Sh500,000 lakini isiyozidi Sh2 milioni au kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miezi 12 au vyote viwili.

Katika kesi ya mkataba wa upangishaji au ushirikiano kati ya shirika na kampuni, atawajibika kwa faini isiyopungua Sh1 milioni lakini isiyozidi Sh10 milioni.

Pia, kifungu cha 17, kifungu kidogo cha pili kimefutwa na kuwekwa kifungu cha pili ambacho mtu yeyote anayepinga au kumzuia mwanachama, ofisa wa shirika, askari polisi au mtu mwingine aliyeidhinishwa katika kutekeleza mamlaka yake chini ya kifungu hiki, atakuwa ametenda kosa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi akizungumza bungeni leo Jumatatu Juni 9, 2025.

Kwa mujibu wa muswada huo, mtu akipatikana na hatia atawajibika kwa faini isiyopungua Sh500,000 lakini isiyozidi Sh2 milioni au kifungo kisichopungua miezi sita lakini kisichozidi miezi 12 au vyote viwili.

Marekebisho ya kifungu cha 15 (2), yamelenga katika kuongeza adhabu hiyo kwa wavujishaji wa siri za shughuli za shirika kwa kifungo kisichozidi miezi sita.

Akiwasilisha maelezo ya muswada huo, Waziri Ndejembi amesema vifungu vya 15, 16 na 17 vinapendekezwa kurekebishwa ili kuongeza viwango vya adhabu vilivyopitwa na wakati kwa mtu atakayebainika kutoa siri za shirika.

Ametaja viwango vya adhabu vinavyoongezwa ni kwa kutoa taarifa za uongo na kujipatia manufaa kwenye shirika au anayezuia wafanyakazi wa shirika kuingia kwenye nyumba kufanya ukaguzi.

“Lengo la marekebisho haya ni kuwezesha adhabu kutolewa kulingana na hali halisi ya thamani ya fedha na uzito wa makosa pamoja na athari za makosa hayo,” amesema.

Aidha, amesema marekebisho hayo yanalenga kuviwezesha vyombo vya utoaji haki kutoa adhabu kulingana na kosa lililotendwa na mtu binafsi au kampuni.

Kwa upande wa kodi, Waziri Ndejembi amesema vifungu vya 12 na 13 vimerekebishwa kwa lengo la kuondoa wajibu wa mwajiri kukata kiasi cha fedha ya kodi ya nyumba pamoja na faini ya kuchelewesha kodi kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi, ambaye ni mpangaji wa Shirika.

“Kwa mujibu wa utaratibu unaopendekezwa, waajiriwa watalipa kodi ya pango kama ambavyo wapangaji binafsi wanalipa,” amesema.

Amesema lengo la marekebisho hayo ni kuongeza uwajibikaji wa moja kwa moja kwa mpangaji katika kulipa kodi ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi za nyumba za Shirika.

Kuhusu uteuzi wa mkurugenzi, Ndejembi amesema kifungu kifungu cha 18 kimerekebishwa kwa kuweka mamlaka ya uteuzi wa mkurugenzi mkuu kuwa ni ya Rais badala ya waziri pamoja na kuboresha masharti ya uteuzi wa mkurugenzi mkuu wa shirika.

“Lengo la marekebisho haya ni kuimarisha utawala bora na uwajibikaji katika usimamizi wa shirika,” amesema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava.

Aidha, waziri huyo amesema kifungu cha 20 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuwezesha posho na malipo mengine ya bodi kufanyika kwa mujibu wa miongozo inayotolewa na mamlaka husika.

“Lengo la marekebisho haya ni kuwianisha masharti hayo na taratibu na miongozo inayohusiana na posho na malipo ya bodi,”amesema.

Kamati yataka adhabu zaidi

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mzava amesema katika Ibara ya 8, Serikali inarekebisha kifungu cha 16 cha sheria kuu kwa kukifuta na kukiandika upya.

Amesema lengo la marekebisho hayo ni kuongeza viwango vya adhabu ambavyo vimepitwa na wakati.

Amesema kamati ina maoni, adhabu iliyowekwa kwa kampuni ni ndogo ukilinganisha na aina ya kosa linalowekwa na sheria ukilinganisha na kosa hilo linapotendwa na mtu binafsi.

“Kwa muktadha huo, ili kuweka uwiano wa adhabu unaolingana na kosa hilo, kamati inapendekeza adhabu kwa kampuni iwe ni faini isiyopungua Sh2 milioni na isiyozidi Sh10 milioni,” amesema.

Akichangia Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga amesema uteuzi wa mkurugenzi ambaye sasa atateuliwa na Rais utasaidia kuweka mizania sawa ndani ya wizara.

“Tunafanya taasisi hii, shirika hili liwe huru kwenye utendaji kazi wake usiweze kuingiliwa kimaamuzi na waziri,” amesema.

Mbunge wa Makete, Festo Sanga

Aidha, amesema kwenye vikao vya bodi wameona bodi inaweza ikawa na vikao vyake inavyotaka kuvifanya.

“Lakini vikao hivi kama mtu sio mwaminifu anaweza akaamua kikao kingine akaitisha kwenda kufanyika nchini China, sasa sisi kamati tuliliona hili kwenye Ibara ya 22, aya namba nane, tuliangalia kwamba ni muhimu sasa bodi inapotaka kufanya vikao iangalie waraka wa Msajili wa Hazina,” amesema.

Amesema waraka ule unaelekeza vikao vyote vifanyike ndani ya Tanzania na kwamba hayo mambo yanafanyika ili kuhakikisha wanaondokana na yale ambayo nyuma alikuwepo kwa bodi kwenda kufanya vikao nje ya nchi.

Naye, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Asha Abdallah Juma (Mshua), amesema:“Jambo ambalo lina tija zaidi katika kifungu namba 24 kinafuta mamlaka ya bodi kudhamini mikopo.”

Amesema kifungu cha 18 cha muswada huo kinaipa bodi mamlaka ya kuajiri na kusimamia ajira za watumishi wa shirika.

“Tunashukuru sana mheshimiwa waziri wa kukubaliana na kamati kwa mamlaka haya ya bodi yafanyike kwa kuzingatia sheria ya utumishi wa umma. Maboresho haya ni muhimu sana kwa ustawi na ufanisi wa shirika,” amesema.

Amesema maboresho ya sheria hiyo yanaenda kulipa nguvu Shirika la  Nyumba la Taifa katika utekelezaji wa kazi zake.

Related Posts