Singida. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche amesema chama hicho kikiingia madarakani kitaweka sera na mazingira bora ya uwekezaji kwenye eneo la viwanda akisema ndio njia sahihi ya kumaliza tatizo la ajira kwa vijana.
Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Singida leo Juni 9, 2025, Heche amesema chama hicho kikipata ridhaa ya kuunda Serikali, kitaelekeza nguvu kubwa kwenye uwekezaji wa viwanda vinavyochakata na kutumia malighafi ya mazao ya kilimo, mifugo na samaki.
Amesema kwa kutambua ukweli umuhimu wa viwanda katika ajira na maendeleo ya kiuchumi kwa Taifa, Serikali ya awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere iliwekeza nguvu na fedha katika ujenzi wa viwanda vya kuchambua pamba, kutengeneza nguo na mazao mengine ya kilimo na mifugo, viwanda alivyosema vimekufa kwa kukosa sera na mpango mzuri wa usimamizi.
“Pale Arusha tulikuwa na kiwanda cha matairi cha General Tyres, tulikuwa na kiwanda cha zana za kilimo pamoja na viwanda kadhaa vya kuchakata zao la pamba. Viwanda hivi siyo tu vilitoa ajira kwa Watanzania, bali pia vilichechemsha uchumi wa nchi kwa kubakiza fedha nchini,” amesema Heche.
Amesema hivi sasa viwanda vingi vilivyojengwa wakati wa Mwalimu Nyerere vimebinafsishwa na kukabidhiwa mikononi mwa wageni ambao wamevigeuza maghala huku ajira za Watanzania zikipotea.
“Hivi sasa kuna pikipiki kila mtaa na kijiji nchini, lakini matairi hata ya baiskeli tunaagiza kutoka nje ya nchi. Lazima tufanye mabadiliko yatakayotuwezesha kupata viongozi wanaopatikana kwa kura ya wananchi ambao watawajibika kwa wapigakura,” amesema Heche.
Amesema kilimo chenye tija ni eneo lingine linalotakiwa kutumika kutengeneza ajira na kuboresha uchumi na maisha ya wananchi.
“Tanzania tumejaaliwa ardhi kubwa yenye rutuba, vipindi vya mvua, maziwa na mito inayotiririsha maji kipindi chote cha mwaka lakini bado tunatumia mabilioni ya fedha kuagiza mafuta ya kula na ngano kutoka nje ya nchi. Chadema tukiingia madarakani tutabadilisha hali hii kwa kuweka sera na mazingira bora ya uwekezaji kwenye viwanda,” amesema Heche.
Amedai kwa mujibu wa takwimu za Serikali, Taifa linatumia zaidi ya Sh260 bilioni kwa mwaka kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi, fedha ambazo zingetumika kutekeleza miradi ya maendeleo iwapo Taifa ingejitosheleza kwa mahitaji ya mafuta.
“Pamoja na mabonde mazuri yanayofaa kwa kilimo, bado Tanzania tunatumia zaidi ya Sh500 bilioni kuagiza ngano kutoka nje ya nchi,” amedai Heche.
Kiongozi huyo amewasihi Watanzania kuunga mkono madai ya mabadiliko yatakayorejesha nguvu na mamlaka kwa umma kuchagua na kuwajibisha viongozi tofauti na hali iliyopo sasa, ambapo wenye madaraka ndio huamua nani awe kiongozi.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ameushukuru umma kwa kuitikia kampeni ya ‘No reforms, no election’ ya chama hicho inayolenga kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi utakaoweka sawa uwanja wa siasa kwa wagombea wa vyama vyote.