Njia za watumwa kufufuliwa, vikao vyaanza SMT na SMZ

Unguja. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), zimeanza vikao vya mashauriano kwa lengo la kufufua na kuhifadhi historia ya njia ya biashara ya watumwa, iliyokuwa ikianzia Kigoma, kupitia Bagamoyo hadi Zanzibar, kama sehemu ya utalii wa kihistoria.

Historia inaonesha kuwa kila mwaka, takribani watumwa 50,000 walipitishwa Zanzibar, huku wengine wapatao 80,000 wakipoteza maisha njiani kabla ya kufika katika soko kuu la watumwa lililokuwa Kelele Square, na hatimaye Mkunazini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga, leo Juni 10, 2025, wakati wa Mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani, Zanzibar.

Waziri Soraga amesema, wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imeshaanza kazi ya kukusanya taarifa za maeneo yanayohusiana na njia zilizotumika wakati wa biashara ya utumwa kutoka Tanganyika hadi Zanzibar. 

“Tayari Serikali zote mbili zimeanza vikao vya mazungumzo kufufua njia za soko la watumwa kutoka Kigoma mpaka Zanzibar,” amesema. 

 Waziri alikuwa akijibu swali la msingi la mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir aliyetaka kujua jitihada za kuzifufua njia walizopita watumwa kama zina sura yoyote ya matumani akisema iwapo ikizifufua zitasongeza thamani na pato litakalotokana na sekta ya utalii.

Katika hatua nyingine, mwakilishi huyo amesema kuna taarifa katika Mji Mkongwe kuna mahandaki na upo mpango wa Serikali kuhakikisha mahandaki hayo yanaibuliwa na kuwa pia sehemu ya vivutio.

Waziri Soraga amesema tayari wanatafuta mshauri atakayeelekeza namna bora ya kufanya utafiti kulingana na mazingira ya eneo jinsi yalivyo kubaini maandaki hayo. 

“Tunatambua umuhimu wa jambo hilo, lakini niseme kwamba bado tunatafuta mshauri mwenye weledi ili kufanya utafiti huo kubaini maandaki na iwapo akipatikana tutafanya utafiti huo mara moja,” amesema.

Related Posts